Feb 03, 2019 08:26 UTC
  • Qur'ani Katika Medani ya Mapinduzi ya Kiislamu (1)

Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji popote pale yanapokufikieni matangazo haya ya Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hususan huko nyumbani Afrika Mashariki. Katika siku hizi, wananchi wa Iran wanaendelea na sherehe za Alfajiri Kumi katika kona zote za nchi kwa ajili ya kuadhimisha miaka 40 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya mwaka 1979 nchini Iran.

 

Imam Ruhuullah Khomeini alirejea nchini Iran Februari Mosi 1979,  akitokea uhamishoni Ufaransa na kuongoza moja kwa moja Mapinduzi ya Kiislamu akiwa humu nchini. Kwa mnasaba wa siku hizi za maadhimisho ya Alfajiri Kumi nimekuandalieni kipindi maalumu ambacho kitatupia jicho nafasi ya Qur'ani Katika Medani ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, ambapo hii ni sehemu ya kwanza. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

 

Kwa hakika kila Mapinduzi huibuka na kutokea yakiwa na msingi wa kiidiolojia, kinadharia na fikra maalumu, idiolojia ambayo huwa nguzo na ngome ya mapinduzi hayo. Tajiriba ya kihistoria ya Mapinduzi muhimu yaliyotokea duniani inaunga mkono nukta hii kwamba, kabla ya kutokea Mapinduzi lazima kuweko kwanza maktaba mpya ya kifikra ambayo itayaongoza Mapinduzi husika, kuondoa mfumo uliopo na kutambulisha nidhamu mpya kuhusu nafasi ya mwanadamu katika jamii. Lengo la maktaba hiyo ni kuandaa mfumo wa kisiasa na kijamii unaofaa ambao utakuwa jiwe la msingi, utakaojenga na kuwa mhandisi wa Mapinduzi hayo baada ya kupata ushindi.Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalipata ushindi 22 Bahman 1357 Hijria Shamsia iliyosadifiana na tarehe 11 Februari 1979 kwa uongozi wa busara wa Imam Ruhulla al-Musawi al-Khomeini MA. Mapinduzi haya yalipata ushindi kwa msingi wa fikra maalumu ya kisiasa. Fikra hii ilikuwa ya Kiislamu na Kiqur'ani. Kama mnavyojua, Qur'ani ndicho chanzo muhimu kabisa  cha kuufahamu Uislamu pamoja na vyanzo vingine kama hadithi. Mafundisho ya Qur'ani mbali na kuwa hutumiwa katika maisha ya mtu binafsi na ya kiibada, maneno haya ya Mwenyezi Mungu ni mwongozo pia katika masuala ya kisiasa na kijamii na ni yenye kuainisha mambo ya jamii.

Wananchi Waislamu wa Iran walianzisha harakati na Mapinduzi dhidi ya Mfalme Shah pamoja na utawala wake wa kidikteta na kidhalimu wakipata ilhamu na muongozo wa mafundisho ya Qur'ani.  Aya ya 11 ya Surat al-Raad inasema:

إنَّ اللهَ لا یُغَیِّرُ ما بِقَومٍ حَتّى یُغَیِّروا ما بِأنفُسِهِم

Hakika Mwenyezi Mungu habadili yaliyoko kwa watu mpaka wabadili wao yaliyomo nafsini mwao.

Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yanaweza kutambuliwa kama harakati ya kurejea katika Qur'ani, harakati ambayo, miongozo ya Qur'ani iliondokea na kuwa utambulisho wake mkuu kkutokana na Mapinduzi hayo kuwa kwake ya kidini. Ukweli ni kuwa, kurejea katika Qur'ani Waislamu na kuchota na kunufaika kwao na mafundisho ya Qur'ani huwafanya wasimame na kupambana na ukoloni na udikteta na natija ya hilo ni kufikia izza, heshima na kuupata ushindi mbele ya adui, na muhimu zaidi ni kujikurubisha kwao na Mwenyezi Mungu.

Katika Aya ya 7 ya Surat Muhammad Mwenyezi Mungu anasema:

یَا أَیُّهَا الَّذِینَ آمَنُوا إِن تَنصُرُوا اللَّهَ یَنصُرْکُمْ وَیُثَبِّتْ أَقْدَامَکُمْ

Enyi mlio amini! Mkimnusuru Mwenyezi Mungu naye atakunusuruni na ataithibitisha miguu yenu.

 

Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran uliowashangaza walimwengu, ni mfano wa wazi auni na msaada wa Mwenyezi Mungu na matunda ya kujitolea maisha yao wananchi Waislamuu wa Iran katika njia ya kupatikana utawala wa haki na wa uadilifu wa Qur'ani. Harakati hii adhimu ilikuwa na kiongozi na shakhsia mkubwa aliyekuwa akiifahamu Qur'ani na kuifanyia kazi. Harakati ya Imam Ruhullah Khomeini (MA) ilikuwa na ilhamu na mwongozo wa Qur'ani na ilikuwa imesimama na kujengeka juu ya msingi wa mafundisho wa Qur'ani huku ikiwa imechukua rajua, matarajio na idiolojia zake kutoka katika kitabu hicho Kitakatifu cha Mwenyezi Mungu. Imam Khomeini daima alikuwa akifanya hima na idili kubainisha misingi ya Qur'ani katika kuuongoza nchi na kuiongoza jamii katika uwanja huu.

Imam Khomeini MA, mwasisi na mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu alikuwa akitilia mkazo juu ya kuweko mahudhurio ya Qur'ani katika sehemu zote za maisha na alikuwa akiamini kwamba, kuzifanyia kazi ahkam na sheria za kisiasa za Uislamu ambazo zimeakisiwa na kuja ndani ya Qur'ani,  kutawafanya Waislamu wapate saada na ufanisi na lau kama tawala za Kiislamu na wananchi wa mataifa ya Kiislamu wangetoa kipaumbele na kuyapa umuhimu mafundisho yanayong'ara na yenye ukombozi ya Qur'ani, badala ya kutegemea madola makubwa ya kikoloni, basi leo wasingekuwa watumwa wa madola ya kibeberu kama Wazayuni wavamizi na dola la kibeberu la Marekani. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Imam Khomeini MA aliwataka Waislamu wa Iran na wa dunia kwa ujumla kuelekea upande wa kushikamana na Qur'ani na kukifahamu vyema Kitabu hicho ambacho ni Wahyi na Ufunuo kutoka kwa Mola Muumba. Hii ni kutokana na kuwa, kutoifahamu Qur'ani na mafundisho yake yenye kujenga maisha, ni jambo litakaloandaa uwanja wa kukengeuka kifikra na kivitendo katika jamii ya kidini.

Qur'ani Tukufu

Ni kwa kuzingatia ukweli huo, ndio maana baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, kulishuhudiwa hapa nchini kukiongezeka harakati za Kiqur'ani. Harakati kama kuandaliwa vikao vya visomo vya Qur'ani, mashindano ya Qur'ani, kuwalea na kuwandaa watu kwa ajili ya kufundisha Qur'ani na kutumwa wasomaji wa Qur'ani Tukufu katika maeneo mbalimbali ya Iran kama wahubiri, kuchapishwa na kusambazwa nakala za Qur'ani Tukufu na kadhalika, ni mambo ambayo kwa hakika yalishika kasi na kuongezeka mno baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran. Hii leo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran baada ya kupita miaka 40 tangu kupatikana ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu,  inajifakharisha kuwa, imekuwa na harakati kubwa za Kiqur'ani na kushiriki pakubwa katika mashindano ya kimataifa ya Qu'rani ambapo wawakilishi wa Iran katika mashindano hayo wamepata takribani tuzo 180.

Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kutokana na kuwa kwake na mvuto katika naara, shaari na malengo yake, yaliiondoa Qur'ani katika hali ya kuwa kitu cha pembeni na cha kando na kuirejesha katika uga wa maisha na kuitoa katika hali ya kumjenga mtu na kuivuta upande wa kuijenga jamii na hii leo kuwa moja ya matukio muhimu na athirifu ulimwenguni.

 

Qur'ani ambayo ilikuwa msingi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, iliipatia jamii ujumbe huu kwamba, izza, heshima na hadhi ni ya waumini na waja wema watendao mema. Kwa hakika, wapinzani wamefanya njama kubwa kwa ajili ya kutia doa utajiri huu wa mafundisho ya Mwenyezi Mungu, lakini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutokana na kuizingatia na kuifanyia kazi Qur'ani Tukufu, imeweza kusimama kidete na kukabiliana na hatua za utumiaji mabavu za madola ya mabeberu kwa miaka takribani 40.

Katika kipindi hiki Iran imepiga hatua kubwa katika nyanja mbalimbali na kuzidi kuwa na nguvu zaidi kuliko ilivyokuwa huko nyuma. Hii leo katika ulimwengu wa ulahidi na kuwa tegemezi, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa mnadi na mlinganiaji wa risala ya imani na kujitawala na kutokubali kupiga magoti au kusalimu amri mbele ya mataghuti na madhalimu, ambayo hili nalo ni katika mafundisho ya Qur'ani Tukufu.

Wapenzi Wasikilizaji, muda wa kipindi hiki maalumuu cha sehemu ya kwanza ya 'Qur'ani Katika Medani ya Mapinduzi ya Kiislamu' kilichokujieni kwa mnasaba wa maadhimisho ya Alfajiri Kumi kuelekea katika kilele cha sherehe za Mapinduzi ya Kiislamu, umefikia tamati. Ninakuageni nikikutakieni mafanikio mengi katika shughuli zenu za kila kila siku.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh