Feb 05, 2019 03:43 UTC
  • Jumanne tarehe 5 Februari 2019

Leo ni Jumanne tarehe 29 Jamadil Awwali 1440 Hijria sawa na tarehe 5 Februari 2019.

Siku kama ya leo miaka 40 iliyopita, Imamu Ruhullah Khomeini alitoa amri ya kuundwa serikali ya muda ya Mapinduzi ya Kiislamu; hatua ambayo ilichukuliwa muda mfupi kabla ya ushindi kamili wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini. Katika amri yake hiyo, mwasisi huyo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alitangaza malengo na mipango ya Mapinduzi ya Kiislamu na akaitaka serikali ya muda ifanye hima kwa ajili ya kutimiza malengo hayo. Vilevile katika amri hiyo aliainisha jukumu kuu la serikali ya muda ambalo lilikuwa kuitisha kura ya maoni kwa ajili ya kuainisha mfumo wa kisiasa utakaotawala hapa nchini, kuandaa uchaguzi na kuunda Baraza la Waasisi kwa ajili ya kutunga Katiba na kufanyika uchaguzi wa kwanza wa Bunge.

Kuundwa kwa serikali ya muda ya Mapinduzi

Miaka 40 iliyopita katika siku kama ya leo shirika la ujasusi la Marekani CIA lilikiri kwamba, limefeli katika kutazamia masuala na mkondo wa harakati za Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran. Maafisa wa CIA walikiri kwamba, shirika hilo la ujasusi la Marekani limeshindwa na kufeli katika kutoa utabiri kuhusu masuala ya Iran. CIA ilisema: Kitu ambacho hatukutazamia ni kuona mzee mwenye umri wa miaka 78 akiwaunganisha pamoja watu wa Iran baada ya kuwa uhamishoni kwa kipindi cha miaka 14.

Shirika la ujasusi la Marekani CIA

Siku kama ya leo miaka 138 iliyopita alifariki dunia mwanahistoria, mwanafalsafa na mtaalamu mashuhuri wa masuala ya mashariki wa Scotland, Thomas Carlyle. Mwanafalsafa huyo alizaliwa mwaka 1795 na mbali na lugha ya Kijerumani, alijifunza pia lugha ya Kiarabu. Katika safari zake nyingi katika nchi za Kiislamu, mwanahistoria huyo alijifunza utamaduni na ustaarabu wa Kiislamu na kuathirika mno na dini hiyo. Thomas Carlyle anasema kuhusu Qur'ani kwamba: "Qur'ani ni sauti isiyokuwa na wasita kutoka kwenye roho ya ulimwengu, na wanadamu wanapaswa kuisikiliza, la sivyo hawapaswi kusikiliza maneno mengineyo." Mwanafalsafa huyo wa Scotland anasema kuhusu Mtume Muhammad (SAW) kwamba: Mwenyezi Mungu alimfunza hikima na elimu shakhsia huyu adhimu. Alijiepusha kupenda jaha na ni miongoni mwa watu waliotakaswa na kupendwa mno na Mola Muweza."

Thomas Carlyle

Miaka 161 iliyopita alifariki dunia Abdul Baqi bin Sulaiman Farooqi anayehesabiwa kuwa miongoni mwa wataalamu na malenga wa lugha ya Kiarabu. Alikuwa na kipawa cha kutunga mashairi ya kuvutia tangu akiwa kijana. Abdul Baqi alikuwa miongoni mwa wapenzi wa kizazi cha mtukufu Mtume Muhammad (saw) na alidhihirisha mapenzi yake hayo katika mashairi yake. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo ni pamoja na kile alichokipa jina la "Al Baqiyatus Swalihat."

Na katika siku kama hii ya leo miaka 166 iliyopita alizaliwa alimu na mtaalamu wa lugha wa Kiirani Ayatullah Sheikh Muhammad Qasim Ordubadi katika mji wa Tabriz ulioko Kaskazini Magharibi mwa Iran. Baada ya kumaliza masomo yake ya kati alielekea Najaf nchini Iraq ambapo alipata elimu kwa maulama mashuhuri wa mji huo. Msomi huyo mkubwa baada ya kufikia daraja ya ijtihadi alirejea katika mji wa Tabriz na kuanza kufundisha. Ameandika vitabu kadhaa kikiwemo kile cha "Al Shihabul Mubin fii I'jaazil Qur'an." Alifariki dunia mwaka 1333 Hijria.

 

Tags