Apr 12, 2016 12:31 UTC
  • Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain 116

Assalama Aleikum wapenzi wasikilizaji na karibuni kusikiliza kipindi kingine katika mfululizo wa vipindi hivi vya Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain ambavyo hukujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka hapa mjini Tehran.

 Swali la kipindi cha juma hili linasema, je, kuna aya yoyote katika Qur'ani Tukufu inayoashiria kuwepo Imam aliyeteuliwa na Mwenyezi Mungu ili kuongoza umma wake katika kila zama? Tutajibu swali hili hivi punde kwa hivyo kuweni nasi hadi mwisho wa kipindi. 

**************

Ndugu wasikilizaji, kila mtu anayeirejea Qur'ani Tukufu akiwa ni muadilifu na aliye na insafu na bila ya kuwa na chuki ataona kuwa jibu la swali hili liko wazi kabisa. Hii ni kwa sababu aya hizo zinasema wazi kwamba Mwenyezi Mungu kutokana na rehema yake kwa waja, aliwajaaliwa katika kila zama na kaumu Imam wa kuwaongoza kwenye njia nyoofu kuelekea Kwake na hilo kuwa hoja Yake kwa waja hao. Kama kutakuwa na mambo yasiyoeleweka vyema kwenye aya hizo basi hilo litakuwa halitokani na aya zenyewe bali ni ufahamu mbovu wa watu wanaozisoma, kutokana na mitazomo tofauti ya kifikra na kisiasa ambayo iko mbali na mtazamo wa Qur'ani Tukufu. Mitazamo kama hiyo ambayo kwa kawaida hutokana na fikra potofu ndiyo hupelekea kufasiriwa aya za Qur'ani kwa njia isiyofaa na iliyo mbali na ukweli wa mambo. Kwa hivyo kuwepo kwa Imam mwema anayofuatwa na kuwaongoza waja kwenye njia nyoofu inayowaelekeza kwa Mwenyezi Mungu ni jambo ambalo limeashiriwa na aya nyingi za Qur'ani Tukufu ikiwemo hii ya 71 ya Surat al- Israa inayosema: Siku tutakapowaita watu kwa Imam wao. Basi atakayepewa kitabu chake kwa mkono wake wa kulia, basi hao watasoma kitabu chao wala hawatadhulumiwa hata chembe.

Kuna aya nyingine gani iliyo wazi kuliko hii katika uwazi wa maana? Aya hii inasema kuwa Mweyezi Mungu ataita kila kaumu, yaani kundi la watu, kwa Imam waliokuwa wakimfuata. Kwa hivyo kama Imam huyo atakuwa ni Imam mwema anayeongozwa na Mwenyezi Mungu bila shaka atawaongoza kuelekea Pepo na iwapo atakuwa ni imam mwovu na mpotovu ni wazi kuwa atawaongoza kwenye moto unaounguza. Kwa maelezo hayo, je, hoja hiyo ya Mwenyezi Mungu inaweza kutimia kama hakutakuwepo na Imam mwongofu katika kila zama, Imam anayeongoza na kuelekeza waja kwenye njia ya Mwenyezi Mungu kwa amri yake kama zinavyoashiria suala hilo aya nyingine za Qurlani Tukufu? Mfano wa aya hizo ni aya ya nane ya Surat ar-Rad inayosema: Hakika wewe ni mwonyaji tu. Na kila kaumu ina wa kuwaongoza. Na hili ni jambo ambalo linasisitizwa na kubainishwa na vitabu vingi vya hadithi vyenye kuaminika. Tutakunukulieni baadhi ya hadithi hizo hivi punde, hivyo basi endeleeni kuwa pamoja nasi.

***********

Imepokelewa katika Tafsiri ya Muhammad bin Mas'ud al-Ayashi (MA) akimnukuu Imam as-Swadiq (as) kwamba: 'Ardhi haiachwi bila ya kuwa na Imam anayehalalisha halali ya Mwenyezi Mungu na kuharamisha haramu Yake nayo ni kauli ya Mwenyezi Mungu inayosema: Siku tutakapowaita watu kwa Imam wao.' Kisha akasema: 'Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema: Mtu anayeaga dunia hali ya kuwa hana Imam, huwa amekufa kifo cha ujahili.'

Wapenzi wasikilizaji, imepokelewa katika vitabu kadhaa vya kuaminika katika madhehebu tofauti za Kiislamu hadithi ya Mtume Mtukufu (saw) inayosema: 'Mtu anayeaga dunia hali ya kuwa hamjui Imam wa zama zake huwa amekufa kifo cha ujahili.'

Tunaona hapa kwamba Imam Swadiq (as) anaitumia hadithi hii kusisitiza juu ya maana ya aya tuliyotangulia kuisoma, kuthibitisha kutowezekana kuwepo kwa zama yoyote bila ya kuwa na Imam mwangozaji ambaye kufuatwa kwake huwa ni chanzo cha kuepuka kufa kifo cha ujahili duniani na kunusurika Siku ya Kiama, siku ambayo kila mtu ataitwa kwa Imam wake.

Na huu ndio uadilifu wa Mwenyezi Mungu. Kwa msingi huo kupinga kuwepo Imam mwongozaji katika kila zama kuna maana ya kupinga uadilifu wa Mwenyezi Mungu Mtukufu, na hili ndilo suala linaloashiriwa na Imam wetu Mtukufu al-Imam Ali ar-Ridha (as) katika riwaya ambayo imepokelewa kutoka kwake katika Tafisiri al-Ayashi kuwa amesema: 'Katika kauli ya Mwenyezi Mungu inayosema: Siku tutakapowaita watu kwa Imam wao. Akasema: Je, si ni katika uadilifu wa Mola wenu kuitawalishia kila kaumu mtu iliyojitawalishia yenyewe? Wakesema: Ndio. Akasema: Basi atasema: Jitengeni, nao watajitenga.' Yaani atawaambia simameni na Imam wenu nao watasimama naye.

******

Ndugu wasikilizaji, maana tuliyoibainisha imebainishwa hivyohivyo pia katika vitabu vya Ahlu Sunna. Kwa mfano, Suyuti anamnukuu Mtume Mtukufu (saw) katika kitabu cha ad-Durr al-Munthur kwamba amesema katika kufasiri maana ya aya tuliyosoma ya Surat al-Israa: 'Kila kaumu itaitwa kwa Imam wa zama zake, kitabu cha Mola wake na Sunna za Nabii wake.' Naye Imam Muhammad al-Baqir (as) amenukuliwa katika Tafsiri ya al-Ayashi katika kufasiri aya hiyo kuwa: 'Mtume (saw) atakuja kwenye kaumu yake, Ali (as) kwenye kaumu yake, Hassan (as) kwenye kaumu yake, Hussein (as) kwenye kaumu yake na kila mtu aliyeaga dunia katika kipindi cha Imam wake atakuja naye.'

Na Suyuti na vilevile al-Haakim wamenukuu riwaya inayosema: 'Mtume aliitisha maji huku akiwa na Ali bin Abu Talib. Aliushika mkono wake baada ya kutawadha na kuuweka kifuani kwake (kwa Mtume) na kisha kusema, 'Hakika wewe ni mwonyaji,' akimaanisha yeye mwenyewe Mtume. Kisha aliurejesha kwenye kifua cha Ali na kusema, 'na kila kaumu ina wa kuwaongoza.' Kisha Mtume (saw) alimwambia: 'Ewe Ali! Wewe ni taa ya viumbe, mwisho wa wongofu na kiongozi wa wasomaji. Naapa kwa jina la Allah kwamba wewe uko hivyo.'

************

Wapenzi wasikilizaji, kuna hadithi nyingi mno katika madhehebu zote za Kiislamu zinazozungumzia na kuthibitisha suala hili. Hadithi hizi ni nyingi sana kiasi kwamba zimepita kiwango cha kutiliwa shaka. Ishaallah tutataja baadhi yazo katika kipindi chetu kijacho.

Kwa muhtasari tu ni kwamba Qur'ani Tukufu inabainisha wazi kuwa Mwenyezi Mungu haiachi dunia katika zama zozote zile bila ya kuwa na Imam mwongofu ambaye kumjua, kumfuata na kumtii ni sababu za kumuepusha mwanadamu kufa kifo cha ujahili humu duaniani.

Na kwa maelezo haya machaceh ndio tunafikia mwisho wa kipindi chetu cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain kwa juma hili, kipindi ambacho kimekujieni moja kwa moja kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Basi hadi tutakapokutana tena juma lijalo panapo majaaliwa, tunakuageni nyote wapenzi wasikilizaji kwa kusema, kwaherini.