Alhamisi, 18 Aprili, 2019
Leo ni Alhamisi tarehe 12 Sha'aban 1440 Hijria, sawa na tarehe 18 Aprili, 2019 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 942 iliyopita , tarehe 12 Shaaban mwaka 498 Hijria Qamaria aliaga dunia Hassan bin Hafiz Andalusi, alyekuwa na lakabu ya Ghassani, mpokeaji hadithi na tabibu mashuhuri wa Andalusia, sehemu ya Uhispania ya leo. Ghassani alikuwa mwanafasihi mahiri na tabibu mweledi. Aidha alikuwa na hati za kuvutia sana na mwenye kipaji kikubwa cha kutunga mashairi. Kitabu cha 'Tamjiidul-Muhmal' ni moja ya athari za thamani za Hassan bin Hafiz Ghassani na ambacho kinazungumzia na kufafanua maisha ya wapokezi wa hadithi.

Siku kama ya leo miaka 80 iliyopita, alizaliwa Ayatullah Sayyid Ali Husseini Khamenei, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran katika mjini wa Mash'had huko kaskazini mashariki mwa Iran. Ayatullah Sayyid Ali Khamenei alikuwa mwana wa marhoum Hujjatul Islam wal Muslimin Hajj Sayyid Javad Husseini Khamenei na alikuwa mtoto wa pili katika familia. Maisha ya Sayyid Javad Khamanei, sawa na ya wanazuoni wengi yalikuwa sahaji sana. Ayatullah Khamenei alipata malezi bora katika familia ya kidini na kuanza kusoma akiwa na umri wa miaka minne. Akiwa na umri wa miaka 18, Ayatulla Khamenei alianza masomo chini ya usimamizi wa mwanazuoni na marjaa maarufu Ayatullahil Udham Milani. Sayyid Ali Khamenei alianza masomo ya dini chini ya usimamizi wa baba yake na kupiga hatua zaidi za maendeleo katika uwanja huo. Hatimaye alielekea katika mji mtakatifu wa Qum na kuendelea na masomo ya juu kwa wasomi wakubwa wa zama hizo kwa muda wa miaka saba. Wanazuoni kama Imam Khomein MA, Ayatullahil Udhma Burujardi na Allamah Tabatabai ni miongoni mwa wasomi ambao Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu alipata elimu kutoka kwao. Katika kipindi cha ujana wake Ayatullah Sayyid Ali Husseini Khamenei alijiunga na harakati za Imam Khomein MA za kuupinga utawala wa kidikteta wa Shah. Alieneza fikra za Imam Khomein na kufichua ufisadi wa viongozi waliokuwa katika utawala wa wakati huo. Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu alikamatwa na kutiwa gerezani mara kadhaa. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu alikuwa mwanachama wa Baraza la Mapinduzi na kisha baada ya hapo, aliwahi pia kuchaguliwa kuwa mbunge na pia mwanachama wa Baraza la Wataalamu wanamchagua Kiongozi Muadhamu. Aidha alikuwa Rais wa Iran katika duru mbili mfululizo na hatimaya mwaka 1989, baada ya kuaga dunia Imam Khomeini MA, alichaguliwa na Baraza la Wataalamu kuwa Kiongozi wa pili wa Iran.

Miaka 65 iliyopita katika siku kama ya leo, Gamal Abdel Nasser alifanya mapinduzi dhidi ya Muhammad Nagib na kuwa Rais wa nchi hiyo. Gamal Abdel Nasser ndiye aliyeitafisha na kuitangaza kuwa mali ya taifa Kanali ya Suez na alikuwa na nafasi muhimu katika juhudi za kukabiliana na ubeberu katika ulimwengu wa Kiarabu na barani Afrika. Aidha Rais huyo wa zamani wa Misri alikuwa na nafasi muhimu katika kuasisiwa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote NAM.

Katika siku kama ya leo miaka 65 iliyopita, mkutano wa kwanza wa wawakilishi wa nchi za Asia na Afrika uliojulikana kwa jina la Mkutano wa Bandung ulifanyika katika mji wenye jina hilo nchini Indonesia. Mkutano huo uliowashirikisha wajumbe kutoka zaidi ya nchi 29 za Asia na Afrika, ulikuwa na lengo la kujenga umoja wa nchi hizo za ulimwengu wa tatu katika kukabiliana na kambi kubwa mbili duniani za Mashariki na Magharibi. Mkutano wa Bandung ndio ulioandaa mazingira ya kuundwa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM).

Miaka 40 iliyopita katika siku kama ya leo yaani 29 Farvardin mwaka 1358, Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran lilimbai na kutangaza utiifu kwa Imam Khomeini MA, hayati Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran. Kulifanyika gwaride mbali mbali kote Iran kutangza hadharani utiifu huo, hatua ambayo iliunga mkono na kukaribishwa na wananchi Waislamu wa Iran. Kwa msingio huo 29 Farvardin au tarehe 18 Aprili kila mwaka huadhimishwa kama Siku ya Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Siku kama ya leo miaka 39 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 18 Aprili 1980, Zimbabwe ambayo wakati ule ilikuwa ikijulikana kwa jina la Rhodesia, ilipata uhuru. Zimbabwe ilikoloniwa na Uingereza mwishoni mwa karne ya 19. Mara baada ya Vita vya Pili vya Dunia na kufuatia kudhoofika Uingereza, zilianza harakati za wananchi za kupigania uhuru na hatimaye harakati hizo zilipelekea kuundwa makundi ya mapambano ya silaha. Zimbabwe ina ukubwa wa zaidi ya kilomita mraba 390,000 na inapakana na nchi za Msumbiji, Zambia, Botswana na Afrika Kusini.

Miaka 23 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani tarehe 18 Aprili 1996 , jeshi la anga la utawala wa Kizayuni wa Israel lilishambulia makao ya kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa katika kijiji cha Qana, kusini mwa Lebanon. Katika shambulizi hilo la kinyama la Wazayuni, takribani raia 110 wa Lebanon waliuawa shahidi wakiwemo wanawake na watoto. Licha ya hayo, Marekani ilizuia kupasishwa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa azimio la kulaani mauaji ya kijiji cha Qana yaliyofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel.
