Jun 27, 2019 05:56 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 830 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 38 ya S’aad. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 44 ambayo inasema:

وَخُذْ بِيَدِكَ ضِغْثًا فَاضْرِب بِّهِ وَلَا تَحْنَثْ ۗ إِنَّا وَجَدْنَاهُ صَابِرًا ۚ نِّعْمَ الْعَبْدُ ۖ إِنَّهُ أَوَّابٌ

Na shika kicha cha vijiti tu mkononi mwako, kisha ndio upigie nacho, wala usivunje kiapo. Hakika tulimkuta mwenye subira, mbora wa waja, kwa hakika alikuwa mwingi wa kutubu.

Katika darsa iliyopita tulizungumzia habari za Nabii Ayoub (as) na tukaeleza kwamba Mwenyezi Mungu alimtahini Mtume wake huyo kwa kumpa maradhi thakili yaliyoudhoofisha mno mwili wake pamoja na kupoteza pia mali na watoto wake; lakini pamoja na masaibu yote hayo aliendelea kuwa na subira na kumshukuru Allah muda wote. Kwa mujibu wa mapokeo ya Hadithi, mkewe Nabii Ayoub hakumwacha mume wake peke yake katika muda wote wa kuumwa kwake, bali muda wote alikuwa pamoja naye kumuuguza na kumhudumia. Lakini siku moja alipokuwa amechoka taabani kutokana na kazi ya kumuuguza mumewe mgonjwa, alipatwa na wasiwasi wa shetani, akasema maneno yaliyomaanisha kuwa, Mwenyezi Mungu amemsahau Ayoub (as), na kwa hivyo ingepasa amuelekee mwengine asiyekuwa Allah ili kuweza kuokoka na tabu na matatizo yaliyomfika. Maneno hayo yalimtafiri mno Nabii Ayoub, akala yamini kwamba atakapopoa maradhi aliyonayo, atampa adhabu mkewe ya kumchapa. Lakini baada ya Mtume huyo kupata shifaa kwa rehma na fadhila za Mwenyezi Mungu kutokana na maradhi thakili yaliyokuwa yamemsibu, kwa kuwa mkewe huyo alijitolea kwa moyo wake wote kumuuguza na kuwa pamoja naye katika muda wote wa kuugua kwake, alighairi kutekeleza uamuzi alioulia kiapo wa kumpa adhabu. Aya tuliyosoma inasema: Allah SW alimhutubu Nabii Ayoub na kumwambia: Kwa kuwa umeapa, usihalifu kiapo chako, ili heshima ya jina la Mwenyezi Mungu uliloapia ilindwe; lakini kwa kuwa mkeo anastahiki kusamehewa, basi chukua kishuke kimoja cha ngano nzima au mfano wake, kisha mpige nacho kwa wepesi mkeo, ili yamini uliyokula uwe umeitekeleza, na yeye pia asiumie wala kupata machungu kwa kumpiga. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, kama ambavyo Siku ya Kiyama, Mwenyezi Mungu atampunguzia na kumhafifishia adhabu mtu kutokana na mema aliyofanya, kwa upande wa duniani pia anatuusia tuwafanyie tahafifu watu ya adhabu tunazowapa kutokana na mambo mema waliyofanya. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, jina tukufu la Allah lina heshima ya kipekee. Kwa hivyo haifai kuhalifu kiapo kinachoapiwa kwa jina hilo tukufu. Wa aidha aya hii inatuelimisha kwamba, kuwa na nasaba na ujamaa na Mtume hakumzuilii  mtu kutekelezewa sharia ya Allah.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 45 hadi 48 ambazo zinasema:

وَاذْكُرْ عِبَادَنَا إِبْرَاهِيمَ وَإِسْحَاقَ وَيَعْقُوبَ أُولِي الْأَيْدِي وَالْأَبْصَارِ

Na wakumbuke waja wetu, Ibrahim na Is-haqa na Yaa'qubu walio kuwa na nguvu na busara.

إِنَّا أَخْلَصْنَاهُم بِخَالِصَةٍ ذِكْرَى الدَّارِ

Sisi tumewakhusisha wao kwa sifa ya ukumbusho wa Akhera.

وَإِنَّهُمْ عِندَنَا لَمِنَ الْمُصْطَفَيْنَ الْأَخْيَارِ

Na hakika wao kwetu sisi ni wateuliwa walio bora.

وَاذْكُرْ إِسْمَاعِيلَ وَالْيَسَعَ وَذَا الْكِفْلِ ۖ وَكُلٌّ مِّنَ الْأَخْيَارِ

Na mkumbuke Ismail na Alyasaa na Dhulkifli, na wote hao ni katika walio bora.

Baada ya aya zilizotangulia kuzungumzia habari za baadhi ya Mitume, aya hizi zinaendeleza maudhui hiyo kwa kuashiria kwa muhtasari habari za Mitume wengine sita wa Allah kwa kusema: Wao walikuwa waja safi wa Mwenyezi Mungu; na Yeye Mola aliwatakasa na kila aina ya dhambi na uchafu wa nafsi na batini na kuwafikisha kwenye daraja ya juu kabisa ya ikhlasi na utakasifu. Sifa ya mwanzo kabisa ya Mitume iliyoashiriwa katika aya hizi, ni kuwa kwao waja halisi wa Allah. Hii ina maana kwamba, Mitume, walifikia daraja hiyo kutokana na upeo wa juu wa kuabudu na kudhihirisha uja wao kwa Mola. Na wao hawakuwa wakimwabudu tu Allah, lakini pia walitii kwa maana halisi na kuyatekeleza maamrisho yake yote katika kila jambo la maisha yao. Ni kinyume na walivyo watu wa kawaida, ambao katika maisha yao ya kila siku, huwa kwa kawaida wanapigania kupata yale yanayozipendeza na yanayozitamani nafsi zao; na kama watafanya jambo lolote lile lisiloendana na matakwa yao, huona adha na kulifanya jambo hilo kwa ikrahi. Lakini waja wa kweli wa Allah, huwa siku zote wanatanguliza mbele matakwa ya Allah badala ya matakwa yao na wanajifaharisha na kuyatekeleza maamrisho ya Mola wao kwa hamu na shauku kubwa. Ni wazi kwamba kuifikia daraja hiyo kunahitaji juhudi kubwa za kujihini na kujibana mja batini ya nafsi yake; na watu wenye sifa hizo hupata ustahiki wa kupewa Utume na kuwa miongoni mwa waja wema na wateule wa Allah. Lakini mbali na sifa ya uja na kuabudu, Allah SW amewataja Mitume wake kuwa ni watu wenye ujuzi na basira pia. Kwa maana kwamba, kuwa na uwezo na uono mkubwa wa kutambua majukumu yao na kuutumia uwezo na suhula zao na za wafuasi wao kwa ajili ya kufanikisha na kufikia malengo yao, ni sifa nyingine waliyopambika nayo waja hao wateule wa Allah. Aya hizi pia zinaashiria faida ya kuikumbuka Siku ya Kiyama na taathira yake katika kumtakasa na kumvua mtu na mapenzi ya kuikumbatia dunia. Katika aya hizi aidha imetiliwa mkazo mara mbili nukta kwamba Mitume ni watu wema, bora na wateuliwa. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kutalii na kusoma habari za kaumu na Mitume waliopita na kuwaenzi na kuwaadhimisha wajumbe hao wa Allah ni moja ya taratibu zinazotumiwa na Qur'ani katika kuwalea na kuwajenga wanadamu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, daraja ya juu ya uja na kumwabudu Allah ndiyo asili ya ukamilifu wote wa kiutu wa Mitume. Kwa sababu hiyo, kuwa mja halisi na mwenye ikhlasi kwa Mola, kumetangulia kutajwa kabla ya sifa zao nyingine za ukamilifu. Kwa maneno mengine tunaweza kusema, Mitume wameifikia daraja hiyo kutokana na kuwa kwao waja na watumwa wa kweli wa Allah. Vile vile aya hizi zinatuelimisha kwamba, kujivua mapenzi ya dunia na kuifikiria muda wote akhera, humwezesha mtu kuwa mja safi na mwenye ikhlasi na kumtakasa na machafu ya kidunia pamoja na kumpa basira ya uono mpana, wa kina na wa mbali wa mambo. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 830 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah azivue nyoyo zetu mapenzi ya kuikumbatia dunia na atutie hima ya kuishughulikia na kujiandalia akhera yetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/

 

Tags