Jun 27, 2019 06:09 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 832 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 38 ya S’aad. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 59 hadi 61 ambazo zinasema:

هَـٰذَا فَوْجٌ مُّقْتَحِمٌ مَّعَكُمْ ۖ لَا مَرْحَبًا بِهِمْ ۚ إِنَّهُمْ صَالُو النَّارِ

Hili ndilo kundi litakalo ingia pamoja nanyi. Hapana makaribisho mema kwao. Hakika hao wanaingia Motoni.

قَالُوا بَلْ أَنتُمْ لَا مَرْحَبًا بِكُمْ ۖ أَنتُمْ قَدَّمْتُمُوهُ لَنَا ۖ فَبِئْسَ الْقَرَارُ

Waseme: Lakini nyinyi! Hamna mapokezi mazuri! Nyinyi ndio mliotutangulizia haya, napo ni pahala paovu kabisa!

قَالُوا رَبَّنَا مَن قَدَّمَ لَنَا هَـٰذَا فَزِدْهُ عَذَابًا ضِعْفًا فِي النَّارِ

Waseme: Mola wetu Mlezi! Aliyetutangulizia haya mzidishie adhabu mara mbili Motoni.

Katika darsa iliyopita tulizungumzia baadhi ya adhabu watakazopata Siku ya Kiyama madhalimu na wachupa mipaka ya Allah. Aya hizi tulizosoma zinasema: Watu watakaokuweko motoni hawatowakaribisha wenzao wapya, bali watawatolea maneno makali na kuwalaumu. Kwa mujibu wa aya za Qur'ani, vinara wa upotofu watawalaumu wafuasi wao, na wafuasi wa upotofu, nao pia watawaona viongozi wao hao ndio sababu ya wao kuingia motoni; na kwa hivyo wao pia watawaapiza na kuwalaani hao waliowaongoza kufuata upotofu. Malaika wa motoni watawaelekea viongozi wa shirki na ukafiri na kuwaambia: Hawa ndio wale wale wafuasi wenu wa duniani, ambao leo wanakufuateni na kuingia makundi kwa makundi pamoja na nyinyi motoni. Walipokuwa duniani walikuwa wakikufuateni nyinyi, na leo wako pamoja na nyinyi pia motoni, na nyote mtaungua na kuteketea kwa adhabu ya Moto. Ni utaratibu wa kawaida wa kila mahali, kwamba wakati watu wanapofika kwenye hadhara fulani, waliopo kwenye hadhara hiyo huwalaki na kuwakaribisha wenzao. Lakini viongozi na vinara wa shirki na ukafiri, watakaokuwa wametangulizwa motoni, watawaambia wale watakaofuatia baada yao kwamba: Hatukupeni makaribisho ya motoni! Na wale watakaokuwa wanaingizwa wakati huo, watawajibu viongozi wao hao: Na nyinyi wenyewe pia si wa kupewa makaribisho. Nyinyi ndio mliotufikisha sisi hapa na kutufanya tuingie motoni. Kisha watamwomba Mwenyezi Mungu awape viongozi wao hao adhabu maradufu kulinganisha na wao, kwa kuwa wao ndio waliosababisha kupotoka na kuhasirika wafuasi wao. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, watu wa motoni watalaumiana na kuchukiana. Kila kundi litalibebesha mzigo wa lawama kundi jengine, huku yakipapurana na kushutumiana yenyewe kwa yenyewe. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, Siku ya Kiyama ni siku ya kudhihiri hakika ya amali alizofanya mtu duniani. Siku hiyo mwanadamu atayaona matunda ya amali na matendo yake ya hapa duniani. Aya hizi zinatuelimisha pia kwamba, haiwezekani mtu kumbebesha mwenzake mzigo wa lawama wa madhambi yake. Hata kama waliowaongoza watu kwenye ukafiri na maasi wana hatia kwa hilo na watapata adhabu kali zaidi, lakini hilo haliwatoi lawamani na kuwaondolea dhima kwa namna yoyote ile wale waliowatii na kuwafuata. Watu wanaokubali kuwatii kibubusa viongozi wa dhulma na ukafiri, wao wenyewe pia wana makosa; na makundi yote hayo mawili yatapata adhabu ya Moto.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 62 hadi 64 ambazo zinasema:

وَقَالُوا مَا لَنَا لَا نَرَىٰ رِجَالًا كُنَّا نَعُدُّهُم مِّنَ الْأَشْرَارِ

Watasema: Tuna nini hata hatuwaoni wale watu ambao tukiwahisabu ndio katika waovu?

أَتَّخَذْنَاهُمْ سِخْرِيًّا أَمْ زَاغَتْ عَنْهُمُ الْأَبْصَارُ

Tulikosea tulipo wafanyia kejeli, au macho yetu tu hayawaoni?

إِنَّ ذَٰلِكَ لَحَقٌّ تَخَاصُمُ أَهْلِ النَّارِ

Hakika hayo ya kuhasimiana watu wa Motoni ni kweli.

Wakati watu wa motoni walipokuweko duniani, walikuwa wakijiona wana shakhsia na hadhi kubwa katika jamii. Wakiwachukulia waumini wengi kuwa ni watu duni na wanyonge katika jamii, wasio na elimu wala ujuzi wa lolote la kumpa hadhi mtu. Na kila walipopata fursa, walikuwa wakiwafanyia kejeli na stihzai waja hao wateule kwa maneno na vitendo. Kutokana na hayo, aya tulizosoma zinasema: Huko akhera pia, watu hao watadhani, kwa vile wao wameishia motoni, basi lazima na waumini pia wawemo humo na waweze kuwaona. Lakini kwa kuwa hawatowaona ndipo watasema: Ina maana ilikuwa haitustahikii sisi kuwafanyia kejeli na stihzai, na wao hivi sasa wako peponi, au wako motoni kama sisi, lakini hatuwaoni tu?  Leo hii hata hapa duniani pia, viongozi wa mfumo wa ubeberu na madola ya kiistiimari, wanategemea kwamba, kutokana na dhulma na uonevu wanaofanya katika pembe mbali mbali za dunia, mataifa wanayoyanyongesha yasichukue hatua yoyote kukabiliana na dhulma zao, bali yasalimu amri kufuata mfumo na utamaduni wao. Na kama watatokea baadhi ya waumini na wapigania haki na uadilifu wakasimama dhidi ya madola hayo ya kibeberu kwa kupambana na dhulma na kutetea haki za wanaodhulumiwa, basi madola hayo huwaita watu hao waovu, wakorofi na waasi wanaovuruga nidhamu ya dunia. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, si hasha wanaokejeliwa na kudharauliwa duniani, Siku ya Kiyama wakawa miongoni mwa wenye kufuzu na kuokoka. Wao wakaingia Peponi, na wale wanaowakejeli wakaishia motoni. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, tusiwahukumu watu hapa duniani kwa sababu ya dhahiri yao. Si ajabu yule anayeonekana kidhahiri hapa kuwa ni mtu duni, Siku ya Kiyama akawa mtukufu na mwenye hadhi ya juu.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 65 na 66 ambazo zinasema:

قُلْ إِنَّمَا أَنَا مُنذِرٌ ۖ وَمَا مِنْ إِلَـٰهٍ إِلَّا اللَّـهُ الْوَاحِدُ الْقَهَّارُ

Sema: Hakika mimi ni mwonyaji tu; na hapana mola ila Mwenyezi Mungu Mmoja, Mtenza nguvu,

رَبُّ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَمَا بَيْنَهُمَا الْعَزِيزُ الْغَفَّارُ

Mola Mlezi wa mbingu na ardhi na vilivyomo baina yake, Mwenye nguvu, Mwingi wa maghufira.

Katika aya hizi za mwisho zinazozungumzia adhabu ya watu wa motoni, Mwenyezi Mungu Mtukufu anamwambia Bwana Mtume Muhammad SAW ya kwamba: Waeleze washirikina, makafiri na wakubwa wao kuwa: Mimi pia nakuonyeni kwa kukutakeni mjifunze na kupata ibra kwa waliotangulia na kuachana na shirki na ukafiri. Jueni kwamba, hakuna mwabudiwa mwengine yeyote wa haki ghairi ya Allah, Mola pekee wa ulimwengu. Mola ambaye nguvu na uwezo wake hauna kikomo na hakuna yeyote mwenye uwezo wa kukabiliana naye. Yeye, aliye Muumba wa mbingu na ardhi ni Mwendeshaji wa mambo yote ya ulimwengu; na tab'an pamoja na nguvu na uwezo wake usio na mfano na usioshindika, Yeye ni msamehevu mno pia na mwenye huruma kwa waja wake waliomkosea, kama watatubia na kurejea kwake. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, sambamba na utoaji bishara, yanahitajika pia maonyo na indhari ili kusafisha vumbi la mghafala na kujisahau ndani ya moyo wa mtu. Kwa kuwa mwanadamu anakabiliwa na baadhi ya hatari na mambo ya upotoshaji katika maisha yake, ukumbusho na maonyo humwamsha na kumzindua, na kumuondoa kwenye mkondo wa dhalala na upotofu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, ulimwengu mzima uko chini ya irada na uendeshaji mmoja; na uwezo na tadbiri ya Allah SW, Muumba wa ulimwengu imetawala ulimwengu mzima na kukizunguka kila kitu. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mwenye nguvu zisizo na mpaka na rehma zisizo na kikomo. Ni kinyume na mifumo ya kidunia, ambapo wenye nguvu na madaraka katika mifumo hiyo, kwa kawaida huwa si watu wenye upole na huruma. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 832 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atupe mema duniani, na atupe mema akhera na atulinde na adhabu ya Moto. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/

Tags