Sura ya S’aad, aya ya 67-74 (Darsa ya 833)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani.
Hii ni darsa ya 833 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 38 ya S’aad. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 67 hadi 70 ambazo zinasema:
قُلْ هُوَ نَبَأٌ عَظِيمٌ
Sema: Hii ni khabari kubwa kabisa.
أَنتُمْ عَنْهُ مُعْرِضُونَ
Ambayo nyinyi mnaipuuza.
مَا كَانَ لِي مِنْ عِلْمٍ بِالْمَلَإِ الأَعْلَى إِذْ يَخْتَصِمُونَ
Sikuwa na ilimu ya ulimwengu wa juu walipo kuwa wakishindana (kuhusu kuumbwa kwa Adam).
إِن يُوحَى إِلَيَّ إِلاَّ أَنَّمَا أَنَا نَذِيرٌ مُّبِينٌ
Haikufunuliwa kwangu isipo kuwa ya kwamba hakika mimi ni mwonyaji tu alie dhaahiri.
Katika aya tulizosoma kwenye darsa kadhaa zilizopita zilizungumziwa habari za Pepo na Moto na hali za watu wa Peponi na Motoni. Aya tulizosoma zinasema: Hayo ni mambo ya ghaibu, ambayo haiyumkiniki kuyatambua isipokuwa kwa njia ya wahyi; na wahyi huo umebainishwa kwa sura ya maandiko ya Qur'ani baada ya kuteremshwa kwa Bwana Mtume Muhammad SAW. Kwa hivyo kwa kuanzia, aya zinasema: Ewe Mtume waambie washirikina, hii Qur'ani ni habari kubwa ambayo nyinyi mnaipa mgongo kwa kumkufuru na kumkanusha kwenu Mwenyezi Mungu na kwa kutokuwa tayari kuyasikiliza na kuyatafakari maneno ninayokuambieni. Ilhali haya niyasemayo, hayatokani na mimi mwenyewe, bali yote haya yamefunuliwa kwangu ili nikuonyeni na kukupeni indhari kuhusu mustakabali na yaliyoko mbele yenu. Mimi kwa nafsi yangu sina elimu ya ghaibu, na kama mlivyo nyinyi sijui chochote kuhusu mambo ya ghaibu, isipokuwa kama Mwenyezi Mungu ataniteremshia wahyi. Ni kama ilivyokuwa kuhusu kuhoji kwa malaika wakati wa kuumbwa kwa Adam, ambapo sikuwa mimi mwenye kujua chochote kuhusu hilo; ni Yeye Allah SW ndiye aliyenijulisha. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, katika masuala ya itikadi, kukubali au kukataa watu si ishara ya kuwa ni haki au batili fikra na itikadi hiyo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, wahyi utokao kwa Allah ndicho chanzo cha elimu na utambuzi wa Mitume juu ya mambo ya ghaibu. Ni jambo lisilo shaka kuwa, elimu na ujuzi wa Mitume kuhusu mambo ya ghaibu si wa ukamilifu, bali ni wa kiwango anachotaka Allah SW kuwafunulia waja wake hao wateule.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 71 na 72 ambazo zinasema:
إِذْ قَالَ رَبُّكَ لِلْمَلائِكَةِ إِنِّي خَالِقٌ بَشَرًا مِن طِينٍ
Mola wako Mlezi alipowaambia Malaika: Hakika Mimi nitaumba mtu kutokana na udongo.
فَإِذَا سَوَّيْتُهُ وَنَفَخْتُ فِيهِ مِن رُّوحِي فَقَعُوا لَهُ سَاجِدِينَ
Na nitakapomkamilisha na kumpulizia roho inayo tokana nami, basi muangukieni kwa kusujudu.
Aya zilizotangulia ziliashiria mjadala na mazungumzo ya malaika kuhusu maudhui moja muhimu. Aya tulizosoma zinaeleza kwamba mazungumzo na majadiliano hayo yalikuwa kuhusu kuumbwa kwa Adam (as). Kadhia yenyewe ni kwamba, wakati wa kumuumba Adam, Allah SW alilibainisha suala hilo kwa malaika wake kwa kuwaambia: Mimi nimekusudia kuumba kiumbe mpya kutokana na udongo na maji, ambaye anatafautiana sana na viumbe wengine wenye uhai pamoja na wanyama; na nitapulizia roho yangu ndani ya kiumbe huyo. Kwa hivyo itakupaseni msujudu mbele ya kiumbe huyo mpya na mumkubali kuwa yeye ni mbora zaidi kuliko nyinyi. Ni jambo wadhiha na lililo wazi kwamba kiwiliwili cha mwanadamu kimetokana na maji na udongo. Kwa sababu chembechembe zote za vyakula zinazojenga kiwiliwili zinatokana moja kwa moja au kwa namna isiyo ya moja kwa moja na mimea ambayo humea kwenye udongo na kustawi kutokana na maji. Lakini ukweli ni kwamba mbali na kiwiliwili chake kinachotokana na udongo, mwanadamu ana roho pia inayotoka kwa Mola Muumba; na suala hilo linadhihirisha utukufu wa kiumbe huyo na hadhi maalumu aliyonayo katika mfumo wa ulimwengu, kwa sababu ni mbeba amana ya kitu alichojaaliwa na Allah katika ujudi wake. Pamoja na hayo, kupuliziwa roho ya Mwenyezi Mungu ndani ya ujudi wa mwanadamu, maana yake si kwamba kuna kitu kilichotenganika na Allah SW na kuingizwa kwa mwanadamu, hasha! Madhumuni yake ni kuelezea chimbuko na asili ya roho ya kiumbe huyo, kwamba inatokana na ulimwengu uliotukuka wa mbinguni na si huu wa ardhini. Kwa maneno mengine ni kuwa, baadhi ya sifa za Mwenyezi Mungu, ambazo mwanadamu anao utayari na uwezo wa kupambika nazo, amewekewa katika ujudi wake. Kwa mfano, kwa kuzingatia mpaka wa uwezo wa mwanadamu, Allah SW amemtunukia kiumbe huyo baadhi ya sifa zake kama elimu, nguvu na uwezo, huruma na pia kuwa na irada na hiari ya ufanyaji mambo. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, malaika walitangulia kuumbwa kabla ya mwanadamu, kwa sababu Allah SW alizungumza na malaika kabla ya kumuumba kiumbe huyo. Lakini kwa kuwa ustahiki una umuhimu zaidi kuliko utangulizi, mwanadamu katika asili yake, ni kiumbe bora zaidi kuliko malaika. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, mwanadamu ni kiumbe wa pande mbili za kimaada au kimwili na kimaanawi au kiroho. Mwanadamu amesujudiwa na malaika kutokana na upande wake wa kiroho, si kwa sababu ya mwili na dhahiri yake. Aya hizi aidha zinatuelimisha kuwa, haijuzu kumsujudia yeyote asiyekuwa Allah, isipokuwa kama kufanya hivyo kutatokana na idhini na amri yake Yeye Mola. Kwa kuwa kumsujudia Adam kulifanywa kwa amri ya Mwenyezi Mungu SW, malaika walidhihirisha uja wao kwa Yeye Mola, na si kwa Adam (as)!
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 73 na 74 ambazo zinasema:
فَسَجَدَ الْمَلائِكَةُ كُلُّهُمْ أَجْمَعُونَ
Basi wakasujudu Malaika wote pamoja.
إِلاَّ إِبْلِيسَ اسْتَكْبَرَ وَكَانَ مِنْ الْكَافِرِينَ
Isipo kuwa Iblisi; alijivuna na akawa katika makafiri.
Kwa mujibu wa aya za Qur’ani tukufu, malaika ni viumbe watiifu, ambao katu hawakhalifu na kukaidi kutekeleza amri za Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kwa hivyo baada ya kupewa amri ya kumsujudia Adam, wote kwa pamoja na bila ajizi waliitii amri hiyo ya Mola kwa unyenyekevu. Kiumbe pekee aliyeasi na kukaidi kufanya hivyo ni Iblisi, ambaye kutokana na kiburi na kujiona bora hakuwa tayari kuonyesha unyekekevu mbele ya mwanadamu; kwa sababu alijihisi ana utukufu zaidi kuliko kiumbe huyo. Uasi huo aliofanya Iblisi ukawa sababu ya yeye kuporomoka na kupoteza hadhi ya juu aliyokuwa amepewa na kuishia kwenye safu ya makafiri na waasi. Ni wazi kwamba kama Iblisi angekuwa ana asili ya malaika asingeweza kukhalifu amri ya Allah. Kwa hivyo, huko kuasi kwake kunaonyesha kuwa hakutokana na malaika, bali, kama ilivyobainishwa katika aya nyingine za Qur’ani, asili yake yeye alikuwa ni jini. Na jini, kama alivyo mwanadamu ana uwezo wa kuasi na kukhalifu amri. Kwa mujibu wa Hadithi, Iblisi alifikia daraja ya kuwa kwenye safu moja na malaika kutokana na kumwabudu na kumtii Allah SW kwa kipindi kirefu, na ndiyo maana aliunganishwa na malaika katika amri waliyopewa ya kumsujudia mwanadamu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, ghururi na kiburi vinaweza kumporomosha mtu hata kama amepitisha kipindi kirefu cha umri wake katika njia sahihi. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kuchanganyika na kuwa pamoja tu na watu wema hakutoshi kumfanya mtu aokoke, bali inapasa yeye mtu mwenyewe ajitahidi kuwa mwema. Na ndiyo maana kuna watoto na watu wa karibu wa Mitume na mawalii wa Allah waliokengeuka njia ya haki, wakaporomoka kwa kutumbukia kwenye lindi la maovu na ufisadi. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 833 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah azitakase nyoyo zetu na maradhi machafu ya ghururi, majivuno na kiburi. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/