Sura ya S’aad, aya ya 75-78 (Darsa ya 834)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani.
Hii ni darsa ya 834 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 38 ya S’aad. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 75 hadi 76 ambazo zinasema:
قَالَ يَا إِبْلِيسُ مَا مَنَعَكَ أَن تَسْجُدَ لِمَا خَلَقْتُ بِيَدَيَّ ۖ أَسْتَكْبَرْتَ أَمْ كُنتَ مِنَ الْعَالِينَ
Mwenyezi Mungu akamwambia: Ewe Iblisi! Kipi kilicho kuzuia kumsujudia yule niliye muumba kwa mikono yangu? Je! Umejiona mkubwa, au umekuwa katika wakuu kweli?
قَالَ أَنَا خَيْرٌ مِّنْهُ ۖ خَلَقْتَنِي مِن نَّارٍ وَخَلَقْتَهُ مِن طِينٍ
Akasema: Mimi ni bora kuliko yeye. Umeniumba kwa moto, naye umemuumba kwa udongo.
Katika darsa iliyopita tulisema kuwa, baada ya kuumbwa mwanadamu wa mwanzo, Allah SW aliwaamuru malaika wote wasujudu kwa ajili ya kiumbe huyo na wote wakafanya hivyo isipokuwa Iblisi ambaye alikataa. Aya tulizosoma zinasema: Mwenyezi Mungu alimsaili Iblisi na kumuuliza, kwa nini umekataa kumsujudia Adam? Ni kwa sababu cheo na hadhi yako ni ya juu mno, mpaka umehisi amri ya kumsujudia Adam haingepasa kukujumuisha na wewe? Au ni kwa sababu ya kuathiriwa na kiburi, ghururi na majivuno hukuwa tayari kuonyesha khushuu na unyenyekevu mbele yake? Hata hivyo badala ya Iblisi kukiri kwamba kitendo alichofanya hakikuwa sahihi na hivyo kuonyesha majuto kwa aliyoyafanya na kutubia, alionyesha kuwa katika mtazamo wake, Adam ni kiumbe duni kulinganisha na yeye, hivyo hakustahiki kusujudiwa. Na ili kuthibitisha madai yake alifanya mlinganisho kwa kusema: Asili yangu mimi, ambaye ni jini ni moto, na asili ya Adam ni udongo; na ni dhahiri kuwa moto ni bora kuliko udongo! Kuhusu mlinganisho huu uliofanywa na Iblisi, kuna nukta kadhaa ambazo inapasa tuziashirie hapa: Kwanza ni kuwa, ulinganishaji huo haukuwa na msingi wowote unaokubalika kwa sababu hakuna hoja yoyote ya kiakili na kimantiki ya kuthibitisha kwamba moto no bora kuliko udongo. Lakini pili, na tujaalie kuwa yeye Iblisi ni mbora; lakini wakati Mwenyezi Mungu anapotoa amri ya kusujudu na kunyenyekea mbele ya Adam, kuacha kufanya hivyo ni kuhalifu na kukaidi amri ya Muumba, ambako hakuwezi kuhalalishika wala kutetewa kwa mantiki yoyote ile. Na tatu ni kwamba, amri ya kumsujudia Adam haikutolewa kwa sababu yeye ametokana na udongo, bali ni kwa sababu ya roho aliyopuliziwa na Allah ambayo imemfanya awe bora kuliko viumbe wote. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, mhalifu na mkosa, naye pia inapasa apewe fursa ya kujieleza ili kuweza kubaini chanzo na sababu ya uhalifu wake. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, uumbwaji wa mwanadamu unatofautiana na wa viumbe wengine. Na si wanyama tu na viumbe wengine wenye uhai wa ardhini, lakini hata malaika wa mbinguni na majini wasioonekana pia hawaifikii hadhi na daraja ya mwanadamu. Wa aidha aya hizi zinatuelimisha kwamba, tunapokutana na amri wadhiha ya Allah SW, wajibu wetu ni kutii na kuitekeleza; na si kutoa hoja batili na zisizo na mantiki za kuasi amri ya Mola. Vile vile aya hizi zinatutaka tuelewe kuwa, uasi na ukaidi unaofanywa na watu wasio tayari kumnyenyekea Allah na kutii amri yake, chimbuko lake ni kiburi na kutakabari mbele ya Mola wa ulimwengu. Aidha tunajifunza kutokana na aya hizi kwamba, ubaguzi wa rangi na tabia wanayokuwa nayo watu wa asili fulani kujiona bora kuliko watu wa asili nyingine ni aina mojawapo ya fikra na mwenendo wa kishetani.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 77 na 78 ambazo zinasema:
قَالَ فَاخْرُجْ مِنْهَا فَإِنَّكَ رَجِيمٌ
Akasema: Basi toka humo, kwani hakika wewe ni mwenye kufukuzwa.
وَإِنَّ عَلَيْكَ لَعْنَتِي إِلَىٰ يَوْمِ الدِّينِ
Na hakika laana yangu itakuwa juu yako mpaka Siku ya Malipo.
Japokuwa Iblisi asili yake ni jini, lakini kutokana ibada na utiifu alioonyesha kwa muda wa miaka mingi aliwekwa kwenye safu moja na malaika. Pamoja na hayo kuasi na kukataa kwake kumsujudia Adam kulionyesha kwamba, hakika yake si mwenye kujisalimisha na kutii amri za Allah bali ni mwenye kufanya lile analolitaka yeye mwenyewe. Kisa chake ni mithili ya mtu aliyefanya bidii na juhudi kubwa, mpaka akaweza kwa tabu na mashaka kuupanda mlima mrefu na kufika hadi kileleni; lakini mara akajisahau, tahamaki ghafla akateleza na kuporomoka moja kwa moja hadi chini. Iblisi, naye pia kutokana na kuasi kwake amri ya Allah, aliporomoka kutoka kwenye daraja aliyokuwa amefikia na kuwekwa mbali na rehma za Mola. Kwa mujibu wa aya hizi, mbali na kuwekwa mbali na rehma za Mwenyezi Mungu, Iblisi alilaaniwa pia na Mola, laana ambayo inaendelea hadi Siku ya Kiyama. Huenda mtu hapa akapitikiwa akilini mwake na suali kwamba, adhabu kubwa kama hiyo inastahiki kweli kwa kosa la kuasi mara moja tu, tena basi kwa sababu ya kutomfanyia Adam na si mwenyewe Allah SW? Jibu la suali na shaka kama hiyo ni kwamba: Kuasi na kukataa kutii amri ni jambo baya, lakini lililo baya zaidi ya hilo ni kujaribu kutetea na kuhalalisha uasi wenyewe. Adam (as) pia aliyekuwa amewekwa kwenye bustani inayofanana na Pepo, aliasi amri ya Allah kwa kula tunda alilokatazwa. Lakini tofauti kati ya Adam na Ibilisi ni kwamba, Adam hakutetea kosa alilofanya, bali alitubia toba ya kweli na akajuta kwa alilolifanya. Na kwa kufanya hivyo, Allah SW aliikubali toba yake na kumfanya apate rehma zake mahususi. Lakini kwa upande wa shetani, yeye badala ya kutubia na kuomba maghufira, aliamua kutoa hoja ya kutetea na kuhalalisha dhambi yake na kwa sababu hiyo akapatwa na laana ya Mwenyezi Mungu. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kiburi, ghururi na majivuno hayana matokeo mengine ghairi ya kumkosesha mtu rehma za Mwenyezi Mungu na neema zake na kumfanya ahasirike. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kuna ulazima wa kuhakikisha watu wasiofaa na wenye kuasi na kupiga vita sheria za Mwenyezi Mungu wanawekwa kando katika jamii. Jukumu na masuulia ya uongozaji na uendeshaji wa jamii inapasa yawe mikononi mwa watu wema na waumini. Vile vile tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, watu wenye sifa za kishetani ambao huwa na husuda na kinyongo na kiburi na ghururi, inapasa wadunishwe na kudhalilishwa katika jamii. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 834 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atughufirie madhambi yetu, atutakabalie toba zetu na aufanye mwema mwisho wetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.