Jumamosi, 24 Agosti, 2019
Leo ni Jumamosi tarehe 22 Mfunguo Tatu Dhul-Hija 1440 Hijria mwafaka na tarehe 24 Agosti 2019 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1380 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, Maytham al-Tammar mmoja wa Masahaba na wafuasi wa Mtume Muhammad (saw) aliuawa shahidi. Awali Maytham al-Tammar alikuwa mtumwa na alinunuliwa na kuachiwa huru na Imam Ali bin Abi Talib (as). Imam Ali alikuwa akimpenda na kumthamini sana Maytham al-Tammar kama ambavyo Maytham pia alikuwa na mapenzi makubwa kwa Imam Ali. Hatimaye katika siku kama ya leo, sahaba huyo mwema wa Mtume (saw) aliuawa kinyama na watawala wa Bani Umayyah kwa kosa la kuwapenda na kuwaunga mkono Ahlul Bait (as). ***
Katika siku kama ya leo miaka 959 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, alifariki dunia malenga na arif mkubwa wa Kiislamu na wa Iran wa karne ya tano Hijria Khaja Abdullah Ansari. Alizaliwa katika mji wa Herat ulioko Afghanistan ya leo ambao wakati huo ulikuwa sehemu ya ardhi ya Iran. Alipewa lakabu ya Mzee wa Herat. Khaja Abdullah Ansari ameandika vitabu vingi vya elimu ya irfani kwa lugha za Kiarabu na Kifarsi kwa sura ya mashairi, mashuhuri zaidi vikiwa ni "Munajat Nameh", "Mohabbat Nameh" na "Zadul Arifin". Vilevile ameandika tafsiri ya Qur'ani Tukufu aliyoipa jina la "Kashful Asrar." ***
Siku kama ya leo miaka 199 iliyopita, duru ya vita vya pili kati ya Iran na Russia ilianza. Sababu ya kutokea vita hivyo ilikuwa ni uvamizi wa jeshi la Russia kwa mipaka ya Iran. Licha ya jeshi la Iran kujitolea katika vita hivyo, lakini wanajeshi hao walishindwa kutokana na udhaifu wa serikali kuu ya wakati huo ya Iran pamoja na kutosaidiwa na kupatiwa himaya askari hao kwa wakati. Vita hivyo vilimalizika kwa kushindwa majeshi ya Iran na kutiwa saini mkataba wa Turkmenchay. Kwa mujibu wa mkataba huo, sehemu kubwa ya ardhi ya Azerbaijan Iran kaskazini mwa Mto Aras ikakaliwa kwa mabavu na Russia na kwa utaratibu huo Iran ikapata hasara isiyofidika. ***
Miaka 90 iliyopita katika siku kama ya leo, mapambano ya Ukuta wa Nudba huko Baitul Muqaddas yalianza. Ukuta wa Nudba huko magharibi mwa Masjidul Aqswa ni eneo alilotumia Mtume Muhammad SAW wakati wa kupaa mbinguni katika safari ya Miiraj na kwa sababu hiyo eneo hilo lina umuhimu wa kidini na kihistoria kwa Waislamu. Tangu wiki moja kabla ya kuanza mapambano ya Ukuta wa Nudba, Wazayuni ambao kidogo kidogo walikuwa wameanza kuikalia kwa mabavu Palestina wakiungwa mkono na Uingereza walianzisha harakati dhidi ya Waislamu. Siku hiyo Wapalestina waliokuwa na hasira walianzisha mapambano makali dhidi ya Wazayuni. Mapambano hayo yalienea kwa kasi kwenye miji mingine ya Palestina na Waingereza wakaamua kutangaza utawala wa kijeshi huko Palestina kwa kuhofia hasira za Wapalestina. ***
Siku kama ya leo miaka 41 iliyopita, Hujjatul Islam Walmuslimin Sayyid Ali Andarzgu aliuawa shahidi na vibaraka wa utawala wa Shah. Shahidi Andarzgu alianza harakati za mapambano akiwa na umri wa miaka 19 na kufahamiana kwa karibu shahidi Nawab Safawi, kiongozi wa kundi la Waislamu wanamapinduzi. Baada ya hapo Shahid Andarzgu alijiunga na harakati ya Muutalifeye Eslami na alikuwa miongoni mwa waliotekeleza mauaji ya kimapinduzi dhidi ya Waziri Mkuu wa wakati huo wa Shah, Hassan Ali Mansour. Shahid Andarzgu aliendesha mapambano ya siri dhidi ya utawala wa Shah kwa kipindi cha miaka 13 na hatimaye aliawa shahidi shahidi na vibaraka wa Shah katika siku kama hii ya leo katika mapambano ya silaha. ***
Na katika siku kama ya leo miaka 28 iliyopita, nchi ya Ukraine ilipata uhuru wake toka kwa Umoja wa Kisovieti. Ilikuwa katikati mwa karne ya 17 wakati Russia ilipoanza kuikalia kwa mabavu nchi hiyo ambayo katika zama hizo ilikuwa chini ya udhibiti na utawala wa Poland. Hata hivyo mwaka 1922, nchi hiyo ikaunganishwa na mataifa yaliyokuwa yakiunda Umoja wa Sovieti. Hadi mwaka 1980, harakati za wapigania uhuru nchini humo hazikuwa na nguvu. Hatimaye katika tarehe kama ya leo, Ukraine ikajipatia uhuru. ***