Sep 09, 2019 00:27 UTC
  • Jumatatu, 09 Septemba, 2019

Leo ni Jumatatu tarehe 9 Muharram 1441 Hijria sawa na Septemba 9 mwaka 2019.

Leo kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, ni siku ya Tasua yaani tarehe tisa Mfunguo Nne Muharram. Katika siku kama hii mwaka 61 Hijria wakati majeshi ya Yazid yalikuwa yamejiandaa kikamilifu kumshambulia Imam Hussein AS na masahaba zake katika ardhi ya Karbala, Imam alimtuma ndugu yake aliyesifika kwa ushujaa mkubwa yaani Abul Fadhl Abbas akawaombe maadui hao wampe fursa aupitishe usiku huo, kwa Swala na kunong'ona na Mola wake. Usiku huo Imam Hussein aliwakusanya wafuasi wake na baada ya kumhimidi Mwenyezi Mungu na kumsalia Mtume, aliwaambia: ''Kila anayetaka, aitumie fursa iliyobakia ya giza la usiku kwa ajili ya kuyanusuru maisha yake, kwani hakuna atakayebaki hai hapo kesho tutakapokabiliana na jeshi la Yazid.'' Hata hivyo masahaba na wafuasi waaminifu na waumini wa kweli wa mtukufu huyo walikuwa wameshakata shauri la kujitolea mhanga kwa ajili ya Mwenyezi Mungu hadi tone la mwisho la damu zao. Usiku huo wa kuamkia Ashuraa yaani tarehe 10 Muharram, uwanja wa Karbala ulikuwa medani ya ibada kwa mashujaa ambao licha ya kuwa wachache kwa idadi lakini walisimama imara kama mlima na hawakumuacha Imam na kiongozi wao hata dakika moja.

Siku kama hii ya leo miaka 191 iliyopita alizaliwa Leo Tolstoy, mwandishi na mwanafasihi raia wa Russia. Awali Tolstoy alijiunga na jeshi la Qaukasia na katika kipindi hiki ndipo alipoandika kitabu chake cha kwanza alichokupa jina la "Childhood". Mwandishi huyo wa Russia baadae alijiengua jeshini na kutumia muda wake wote kwa ajili ya kusoma na kuandika. Miongoni mwa vitabu muhimu vya mwandishi Leo Tolstoy ni "Vita na Amani", "Waqazaki" na "Hadji Murad." Tolstoy alifariki dunia mwaka 1910.

Leo Tolstoy

Katika siku kama hii ya leo miaka 50 iliyopita alifariki dunia Jalal Aal Ahmad, mwandishi na mkosoaji wa Kiirani. Aal Ahmad alizaliwa mwaka 1302 Hijria Shamsiya jijini Tehran. Mwaka 1325, Jalal Aal Ahmad alitunukiwa shahada ya fasihi kutoka Chuo Kikuu cha Tehran. Aliingia katika uwanja wa siasa wakati wa Vita vya Pili vya Dunia na akaanza kuandika magazeti. Alijishughulisha na kuandika makala zenye kukosoa na hadithi fupifupi. Jalal Aal Ahmad alikuwa hodari katika kuandika visa na hekaya fupifupi.

Jalal Aal Ahmad

Miaka 43 iliyopia katika siku kama ya leo, aliaga dunia Mao Tse Tung kiongozi wa Uchina. Tse Tung alizaliwa mwaka 1893 na mwaka 1921 aliunda chama cha Kikomonisti cha Uchina baada ya kuungwa mkono na wafuasi wa fikra zake. Mao alikuwa akisisitiza juu ya kuwatetea na kuwalinda wanavijiji na kwa sababu hiyo ilipata uungaji mkono mkubwa wa wanavijiji wa Uchina. 

Mao Tse Tung

Na siku kama ya leo miaka 18 iliyopita Ahmad Shah Massoud mmoja wa makamanda wakubwa wa Mujahidina wa Afghanistan ambaye pia aliyekuwa Waziri wa Ulinzi katika serikali ya mpito ya Rais Burhanuddin Rabani wa Afghanistan, aliuawa. Ahmad Shah Massoud alizaliwa mwaka 1952 na alianza kupigana vita na nchi za kigeni katika milima ya kaskazini mwa Afghanistan sambamba na kuingia madarakani wakomunisti huko Afghanistan na mara baada ya kukaliwa kwa mabavu nchi hiyo na jeshi la Urusi ya zamani mwaka 1979.

Ahmad Shah Massoud