Jumatano tarehe 18 Septemba 2019
Leo ni Jumatano tarehe 18 Mfunguo Nne Muharram 1441 Hijria inayosadifiana na tarehe 18 Septemba 2019
Miaka 31 iliyopita katika siku kama ya leo ya tarehe 27 Shahrivar mwaka 1367 Hijria Shamsia, aliaga dunia, Ustadh Muhammad Hussein Shahriyar mshairi mashuhuri wa Kiirani. Alizaliwa mjini Tabriz kaskazini magharibi mwa Iran na baada ya kumaliza masomo yake ya sekondari katika Chuo cha Dar al-Funun mjini Tehran alijiunga na chuo cha tiba. Hata hivyo baada ya miaka michache aliacha masomo na kurejea katika kijiji alichozaliwa. Ustadh Shahariyar alitoa mashairi yake ya kwanza akiwa na umri wa miaka 23. Sambamba na kushadidi harakati za Mapinduzi ya Kiislamu nchini, Shahriyar aliungana na wimbi hilo kwa kutumia mashairi yake. Vilevile alikuwa mashuhuri sana kwa kumpenda Mtume wa Ahlubaiti zake na mapenzi hayo yalidhihiri katika tungo na mashairi yake.
Siku kama ya leo miaka 58 iliyopita yaani tarehe 18 Septemba mwaka 1961 aliaga dunia Dag Hammarskjold mwanasiasa na Katibu Mkuu wa Pili wa Umoja wa Mataifa. Mwanasiasa huyo wa nchini Sweden alifariki dunia baada ya ndege iliyokuwa imembeba wakati wa safari yake katika ardhi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuanguka. Hammarskjold alikuwa Congo kwa lengo la kufanya mazungumzo na pande husika ili kumaliza vita vya ndani nchini humo. Mwanasiasa huyo alizaliwa mwaka 1905 na alihesabiwa katika zama zake kuwa mmoja kati ya waandishi stadi nchini Sweden. Mwaka 1952, Dag Hammarskjold alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Alitunukiwa tuzo ya amani ya Nobeli kutokana na harakati zake za kuimarisha amani duniani.
Siku kama ya leo miaka 132 iliyopita, alizaliwa Ayatullah Sayyid Ahmad Khansari, faqihi na marjaa mkubwa wa Kishia. Akiwa na miaka 20, Ayatullah Ahmad Khansari alielekea mjini Najaf, Iraq na kupata elimu kutoka kwa wasomi wakubwa kama Muhaqqiq Khorasani, Sayyid Muhammad Kadhim Yazdi, Shariat Isfahani na Muhaqqiq Naaini. Ayatullah Sayyid Ahmad Khansari alielekea mjini Arak, Iran katika kipindi cha kuasisiwa chuo kikuu cha kidini cha mji huo na kujishughulisha na ukufunzi. Baadaye msomi huyo alishirikiana na Ayatullah Sheikh Abdul-Karim Hairi katika shughuli za tablighi na baada ya kuasisiwa hauza ya Qum, chini ya usimamizi wa Ayatullah Hairi Yazdi, Ayatullah Ahmad Khansari alikuwa imamu wa Swala ya jamaa katika chuo cha Faiziya mjini humo. Mwaka 1370 Hijiria, Ayatullah Ahmad Khansari alielekea Tehran na kuwa imamu wa Swala ya jamaa katika msikiti maarufu wa ‘Sayyid Azizullah’. Msomi huyo alibakia mjini Tehran hadi mwishoni mwa uhai wake na baada ya kufariki dunia akazikwa mjini Qum.
Siku kama ya leo, miaka 148 iliyopita alizaliwa Allamah Haidar Qali Sardar Kabuli, alimu mkubwa na mtaalamu wa fiqhi mjini Kabul, Afghanistan. Akiwa kijana mdogo Allamah Sardar Kabuli alipata elimu kwa wasomi wakubwa wa enzi hizo kama, Mirza Hussein Nuri na Sayyid Safiyyud-Din Hassan bin Hadi Kadhimi, sanjari na kustafidi na daqrsa za maulama watajika kama vile, Sayyid Hassan Sadr na Haji Sheikh Abbas Qumi, ambapo pia alipata ijaza na (idhini) ya kunakili na kuandika hadithi. Mwaka 1310 Hijiria, Allamah Haidar Qali Sardar Kabuli alielekea Kermanshah, Iran na kujishughulisha na kazi ya kufundisha wakazi wa mji huo sambamba na kuandika vitabu kadhaa. Msomi huyo pia alibobea katika lugha kadhaa za dunia, kama vile Kiarabu, Kingereza, Kiebrania na Kiurdu. Kitabu cha ‘Tarjama ya Injili ya Barnaba’ na ‘Hadithi 40 kuhusu matukufu ya Amirul-Muuminin’ ni miongoni mwa athari za msomi huyo. Allamah Haidar Qali Sardar Kabuli alifariki dunia mwaka 1372 Hijiria akiwa na umri wa miaka 79 na kuzikwa mjini Najaf, Iraq.
Siku kama ya leo miaka 201 iliyopita, nchi ya Chile ilipata uhuru. Mwaka 1536 Chile ilidhibitiwa na Hispania. Sehemu kubwa ya kukoloniwa Chile, nchi hiyo ilikuwa sehemu ya utawala wa Naibu Mfalme wa Uhispania nchini Peru.
Katika siku kama ya leo miaka 310 iliyopita, alizaliwa Samuel Johnson mwandishi wa drama, malenga na mwandishi wa visa wa Kiingereza. Alianza shughuli zake za fasihi sambamba na ukosoaji wake katika taaluma hiyo. Baada ya muda mwanatamthilia huyo aliingia katika uga wa utunzi wa mashairi. Samuel Johnson aliaga dunia mwaka 1784.