Nov 04, 2019 08:04 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Nov 4

Hujambo mpenzi msikilizaji natumai huna neno, karibu tututupie jicho baadhi ya matukio muhimu ya spoti yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita, kitaifa na kimataifa…….

Iran yashinda taji la Mieleka ya Greco Roman

Timu ya taifa ya mabarobaro ya mieleka mtindo wa Greco Roman ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetwaa ubingwa wa mashindano ya dunia ya mchezo huo yaliyofanyika katika mji mkuu wa Hungary, Budapest. Iran ambayo imeibuka kidedea kwa alama 122, imetia kibindoni medali 3 za dhahabu na 3 za shaba katika mashindano hayo yaliyofikia tamati Jumapili. Vijana shupavu wa Kiirani waliyotwaa medali za dhahabu ni Meysam Dalkhani katika safu ya kilo 63, Mohammadreza Geraei kilo 72 na Aliakbar Yousefi katika kategoria ya kilo 130. Medali za shaba za Iran zilitwaliwa na Mehdi Mohsennejhad katika safu ya kilo 60, Sajad Imentalab kilo 67, na Mohammadhadi Saravi kwa upande wa wanamieleka wenye kilo 97.

Timu ya taifa ya mabarobaro ya mieleka mtindo wa Greco Roman ya Iran

 

Georgia imetwaa nafasi ya pili kwa kuzoa jumla ya alama 121 huku Russia ikifunga orodha ya tatu bora kwa kuchota pointi 118. Hata hivyo, timu hiyo ya taifa ya mabarobaro ya mieleka ya kujiachia almaarufu freestyle ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeibuka ya pili katika mashindano hayo ya kimataifa. Iran imetwaa medali tatu za dhahabu, moja ya fedha na nyingine ye shaba katika mashindano hayo yanayofahamika kama 2019 U23 World Championships. Russia imetwaa ubingwa mashindano kwa kuzoa jumla ya pointi 145, huku Iran ikiibuka mshindi wa pili kwa alama 139. Uturuki ipo katika nafasi ya 8 ikiwa na alama 60, huku Marekani ikishika nafasi ya 10 kwa alama 5 tu. Dhahabu ya kwanza ya Iran ilitwaliwa na Kamran Ghasempour katika kategoria ya kilo wanamieleka kilo 86, baada ya kumbiruarua raia wa Azerbaijan, Gadzhimurad Magomedsaaidov kwa alama 9-3. Medali nyingine za dhahabu ya Iran zilitwaliwa na Mojtaba Goleij, kilo 97 baada ya kumzidi maarifa Mrusi Shamil Zubairov, huku Amir Hossein akimlemea Mrusi mwingine Vitali Goloev katika safu ya kilo 125.

Raga: Afrika Kusini yatwaa Kombe la Dunia

Timu ya taifa ya raga ya Afrika Kusini imetwaa Kombe la Dunia la Raga huko Yokohama Japan, baada ya kuifanyia mauaji ya kimbari Uingereza katika mchuano wa fainali uliopigwa Jumamosi. Afrika Kusini iliinyoa bila maji Uingereza kwa kuizaba alama 32 kwa 12. Hii ni mara ya tatu kwa Afrika Kusini kutwaa taji hilo la dunia. Mchezo wa Jumamosi ulikuwa marudiano ya mechi ya fainali ya mwaka 2007. Wachezaji wa ubavuni Makazole Mapimpi and Cheslin Kolbe walikuwa wa kwanza kuidhalilisha Uingereza kwa kufunga pointi za kiana.

Wachezaji wa Afrika Kusini wakishangilia ushindi

 

Aidha mchezo huo ulikuwa na msisimuko wa ina yake, kutokana na timu hiyo ya Afrika Kusini kuongozwa na nahodha wa kwanza mweusi. Miji ya Afrika Kusini iiripuka kwa shangwe, vifijo na hi baada ya ushindi huo wa kishindo.

Kabla ya hapo, Afrika Kusini iliisasambua Wales katika ngoma ya nusu fainali. Kiungo Handre Pollard ndiye aliyekuwa nyota wa mechi kwa kufunga pointi 14 kwenye mpambano mkali ulioshia kwa Afrika Kusini kushinda 19-16 dhidi ya Wales. Mpambano huo uliokuwa wa kukata na shoka umeshuhudia mabingwa hao wa kombe la Dunia mwaka 1995 na 2007 kuwabwaga Wales katika shindano lao la tatu la nusu fainali baada ya huko nyuma kupoteza katika mwaka 2011 na 1987. Wanaweka rekodi ya kutwaa Ubingwa huo wakiwa na nahodha wa kwanza mweusi Siya Kolisi katika historia ya timu yao ya Rugby. Sasa Afrika Kusini na New Zeland wametwaa Ubingwa huo mara tatu tatu, Afrika Kusini wakitwaa (1995, 2007, 2019), sasa Afrika Kusini unaweza kusema wanashinda Kombe hilo kila baada ya miaka 12.

Riadha: Kenya yatamba tena New York

Kenya imeendelea kuidhihirishia dunia kuwa ni moto wa kuotoea mbali ikija katika mbio za masafa marefu. Wanariadha nyota wa Kenya, Geoffrey Kamworor na Joyciline Jepkosgei wameibuka kidedea katika mbio za New York Marathon nchini Marekani siku ya Jumapili, katika safu ya wanaume na wanawake. Kamworor ambaye ni bingwa wa mbio hizo za New York Marathon mwaka 2017 alikata utepe wa ushindi kwa kutumia saa 2, dakika 8 na sekunde 13. Mwaka 2017 alimaliza mbio hizo kwa kutumia 2:10:53. Mkenya mwingine Albert Korir amemaliza wa pili kwa kutumia 2:08:36 huku Girma Bekele Gebre wa Ethiopia ikitwaa nafasi ya tatu kwa kutumia 2:08:38. Katika safu ya wanawake, Joyciline Jepkosgei aliibuka wa kwanza kwa kutumia saa 2:22:38, na kumpiku Mkenya mwenza Mary Keitany ambaye amewahi kushinda New York Marathon mara tano. Anasisitiza kuwa, hakua chini ya mashinikizo yoyote na alikimbia kwa kasi yake.

Geoffrey Kamworor aliposhinda Copenhagen Marathon miezi michache iliyopita

 

Mhabeshi Lelisa Desisa ambaye alitazamiwa kutoa ushindani mkali kwa akina dada hao wa Kenya, alijiondoa kwenye mbio hizo baada ya kukimbia kilomita 11 tu. Wakati huohuo, wanariadha nyota wa tafa hilo la Afrika Mashariki Eliud Kipchoge na Brigid Kosgei wamekabidhiwa tuzo ya Abbott World Marathon Majors Series XII. Kipchoge aliwapiku washindani wenzake kutoka Ethiopia Lelisa Desisa na Birhanu Legese kutia kikapuni tuzo hiyo maridadi baada ya kujizolea alama 50. Desisa na Legese walipata alama 41 kila mmoja, lakini walichukuwa nafasi za pili kufuatia kura kutoka kwa wakurugenzi wa hafla hiyo. Katika kitengo cha akina dada, Kosgei, ambaye pia alijizolea alama 50, aliwabwaga wanariadha matata wa Ethiopia Ruti Aga na mwenzake Vivian Cheruiyot na kujipatia taji hilo. Aga na Cheruiyot walimaliza katika nafasi ya pili na tatu mtawalia.

Soka: Yanga basi tena!

Wiki moja baada ya klabu ya soka ya Yanga ya Tanzania kupoteza mchezo muhimu katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika ikiwa nyumbani katika Uwanja wa CCM Kirumba, timu hiyo imejikuta tena ikiangukia pua ugenini. Usiku wa kuamkia Jumatatu, klabu hiyo ilichezea tena mkong'oto na kugaragazwa mabao 3 bila jibu katika mchezo wa marudiano na klabu ya Pyramids ya Misri, na hivyo kukamilisha safari ya siku 86 kwenye michuano ya kimataifa. Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera raia wa DR Congo anasisitiza kuwa, timu yake ipo ngangari na kwamba kushindwa kwako sio kutokana na umbuji wa soka wa vijana wa Kiarabu. Kwa kipigo hicho cha msimu, Yanga imebanduliwa rasmi nje ya michuano hiyo ya kimataifa kwa jumla ya magoli 5-1. Kwa kutulia maanani kuwa Klabu za Simba, KMC na Azam zilizotolewa mapema kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho, Tanzania sasa msimu wa 2019/2020 haina muwakilishi yoyote wa kimataifa katika michuano hiyo.

Ligi Kuu ya Soka Uingereza

Na tunatamatisha kipindi kwa kutupia jicho baadhi ya matokeo ya mechi kwenye Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza. Klabu ya Manchester United imechezea kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Bournemouth katika mchezo wa Ligi Kuu ya EPL. Goli la Bournemouth liliwekwa wavuni na Josh King kunako dakika ya 45.

Liverpool nusra itoe sare ya 1-1

 

Kwengineko, klabu ya Liverpool imeweza kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 ilipokabana koo na Aston Villa katika mchezo ulioonekana kuwa mgumu kwa upande wa Liverpool. Wekundu hao wa Uingereza ambao walikuwa wanaitandazia ngozi nyumbani, waliruhusu goli la kizembe kabla ya kusawazisha na kuongeza jingine katika dakika za majeruhi. Mabao ya Liverpool yalifungwa na Andrew Robertson dakika ya 87 na Sadio Mane dakika ya 94.

Mbali na hayo, Crystal Palace ilijikuta ikikubali kudhalilishwa na Leicester City kwa kuzabwa mabao 2-0 katika mechi ya Jumapili, wakati ambapo Tottenham walikuwa wakilazimishwa sare ya 1-1 na Everton. Klabu ya Arsenal licha ya kuupigia nyumbani katika Uwanja wa Emirates, walijikuta na kibarua cha ziada walipovaana na Wanderers na mchuano huo kuishia kwa sare ya bao 1-1. Na kwa kuwa kutangulia sio kufika, bao Pierre-Emerick Aubameyang la dakika ya 21 lilijibiwa na la Raul Jimenez kunako dakika ya 76.

Liverpool inasalia kileleni mwa jedwali la EPL ikiwa na alama 31, mbele ya Manchester City yenye alama 25, huku Leicester ikifunga orodha ya tatu bora kwa alama 23. City ilimaliza 2-1 iliposhuka dimbani kuvaana na Southampton, wakati watani wao wa jadi, Manchester United walipokuwa wanachabangwa na Bournemouth.

………………………TAMATI……………..