Jan 22, 2020 01:02 UTC
  • Jumatano tarehe 22 Januari 2020

Leo ni Jumatano tarehe 26 Jamadil Awwal 1441 Hijria sawa na Januari 22 mwaka 2020.

Siku kama ya leo miaka 1161 iliyopita, sawa na tarehe 26 Jamadil Awwal 1437 Hijria, alifariki dunia Ibn Tayfur, mwandishi na malenga wa Kiarabu. Ibn Tayfur alizaliwa mwaka 204 Hijiria. Baada ya kuhitimu masomo yake ya awali, alijishughulisha na uandishi wa vitabu mjini Baghdad. Katika kipindi hicho Ibn Tayfur alifahamiana na maulama na wasomi mashuhuri wa mji wa Baghdad. Ni baada ya hapo ndipo Ibn Tayfur akawa mashuhuri katika uwanja wa mashairi. Mbali na uwanja huo, msomi huyo alijulikana sana kwa uandishi wa vitabu mbalimbali ambavyo hii leo vinapatikana katika maktaba za mji wa Baghdad, Iraq. 

Siku kama ya leo miaka 459 iliyopita inayosadifiana na tarehe 22 Januari 1561, alizaliwa mwanafalsafa na mtaalamu wa hesabati wa Uingereza Francis Bacon. Awali, Bacon alijishughulisha na masuala ya kisiasa na baadaye alikamatwa na kufungwa jela baada ya kupatikana na hatia ya kula rushwa. Kipindi cha kufungwa jela kilikuwa fursa mwafaka kwa Francis Bacon kudhihirisha kipawa chake. Mwanafalsafa huyo alitoa mchango mkubwa katika kueneza sayansi asili nchini Uingereza na kuhuisha sayansi na falsafa barani Ulaya. Bacon ameandika vitabu kadhaa kikiwemo kile cha New Atlantis. Msomi huyo wa Uingereza alifariki dunia mwaka 1626.

Francis Bacon

Siku kama ya leo miaka 245 iliyopita, alizaliwa Andre Marie Ampere, mtaalamu wa hisabati na fizikia wa Ufaransa. Akiwa kijana mdogo alipendelea sana fani ya hesabati. Akiwa Chuo Kikuu cha Polytechnique cha mjini Paris, aligundua mambo kadhaa katika uga wa fizikia. Moja ya mambo aliyoyagundua Andre Marie Ampere ni pamoja na simu ya upepo "Telegrafu." Mtaalamu huyo alifariki dunia mwaka 1836.

Andre Marie Ampere

Siku kama ya leo miaka 119 iliyopita, alifariki dunia Alexandrina Victoria, malikia maarufu wa Uingereza akiwa na umri wa miaka 82. Victoria alizaliwa mjini London mwaka 1819 Miladia, huku akichukua nafasi ya William IV kiutawala ambapo alisalia katika madaraka kwa kipindi cha miaka 64. Katika utawala wa Alexandrina Victoria, kulishtadi ukandamizaji dhidi ya raia wa nchi hiyo. Kufariki dunia malikia huyo ilikuwa mwanzo wa kudhoofika utawala wa kifalme ambapo baada yake aliingia madarakani Edward VII.

Alexandrina Victoria

Siku kama ya leo miaka 86 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Allamah Mirza Muhammad Hussein Naini, marjaa na faqihi mkubwa na mmoja wa wahakiki wa elimu ya usulu fiq’h. Allamah Naini alizaliwa mwaka 1276 Hijiria Qamaria mkoani Nain, ambao ni moja ya mikoa ya katikati mwa Iran katika familia ya kidini. Allamah Naini alisoma na kuhitimu masomo yake ya awali nyumbani kwao na kuendelea na masomo ya juu huko mjini Najaf, Iraq. Akiwa mjini hapo, alipata kusoma kwa wasomi wakubwa wa zama hizo kama vile Allamah Mirza Shirazi na kufikia daraja ya juu ya elimu za hesabu, falsafa ya sayansi, falsafa, irfan na fiq’hi. Miongoni mwa athari za Allamah Naini ni pamoja na vitabu vya “Wasiilatun-Najjat” na “Tanbiihul-Ummah wa Tanziihul-Millah” kitabu ambacho kilitoa mchango mkubwa katika kuathiri mapambano dhidi ya viongozi dhalimu wa zama hizo.

Ayatullah Allamah Mirza Muhammad Hussein Naini

Siku kama ya leo miaka 41 iliyopita, inayosadifiana na tarehe Pili Bahman 1357 Hijria Shamsia, watu kadhaa waliuawa na wengine kujeruhiwa, baada ya kujitokeza mapigano ya barabarani kati ya wananchi wa Iran na vikosi vya utawala wa Kifalme hapa nchini. Wananchi Waislamu wa Iran walikuwa kwenye maandalizi ya kumpokea Imam Khomeini. Wananchi wa matabaka mbalimbali kutoka mijini na vijijini walikuja mjini Tehran kwa shabaha ya kumlaki Imam Khomeini akitokea uhamishoni nchini Ufaransa. Wakati harakati hiyo ya wananchi ikiendelea, maafisa wasiopungua elfu nne wa Jeshi la Anga, walionyesha uungaji mkono wao kwa wananchi, na kutangaza mgomo wa kula chakula, sanjari na kutaka washauri wa Kimarekani waliokuwepo hapa nchini waondoke haraka iwezekanavyo.

 

Tags