Feb 04, 2020 02:42 UTC
  • Jumanne tarehe 4 Februari 2020

Leo ni Jumanne tarehe 9 Jamadithani 1441 Hijria sawa na Februari 4 mwaka 2020

Na siku kama ya leo miaka 742 iliyopita yaani tarehe 9 Mfunguo Tisa Jamadithani mwaka 699 Hijria, Ibn Farah Eshbily malenga, mshairi na mtaalamu wa elimu ya hadithi katika karne ya saba Hijria alifariki dunia. Alizaliwa katika Andalusia ya zamani ambayo leo ni eneo la kusini mwa Uhispania. Alitiwa mbaroni baada ya majeshi ya Uhispania kuushambulia mji huo. Hata hivyo baada ya kushikiliwa kwa muda, alitoroka na kukimbilia nchini Misri. Akiwa nchini Misri Ibn Farah Eshbily alifanikiwa kuchota elimu na maarifa kwa maulama mashuhuri wa zama hizo mjini Cairo. Baada ya muda alielekea Damascus Syria na kujiendeleza zaidi kielimu. Alimu na msomi huyu wa Kiislamu ameacha athari nyingi za kielimu hususan katika uga wa mashairi.

Siku kama hii ya leo miaka 332 iliyopita Pierre Marivaux mwandishi wa riwaya na michezo ya kuigiza wa Kifaransa alizaliwa huko Paris nchini Ufaransa. Pierre alianza kujishughulisha na kazi ya sanaa tangu akiwa kijana na kwa muda fulani alishiriki pia katika michezo ya kuigiza hadi pale alipoanza kuandika michezo hiyo. Marivaux alipata umashuhuri mkubwa kutokana na ukosoaji wake katika uandishi wa riwaya. Marivaux ameacha athari nyingi za kimaandishi zikiwemo riwaya na michezo ya kuigiza ambapo miongoni mwake tunaweza kuashiria zile alizozipa majina kama ya The Prudent na Equitable Father, The Triumph of Love na The Life of Marianne. 

Pierre Marivaux

Siku kama ya leo miaka 75 iliyopita kulifanyika mkutano uliojulikana kwa jina la Yalta katika peninsula ya Crimea huko kusini mwa Urusi ya zamani. Mkutano huo uliwakutanisha pamoja  viongozi wa nchi za Uingereza, Marekani na Shirikisho la Urusi ya zamani (Churchill, Roosevelt and Stalin). Mkutano huo ulifanyika baada ya kudhihiri dalili za kushindwa Ujerumani katika Vita vya Pili vya Dunia. Lengo hasa la mkutano wa Yalta lilikuwa kujadili hali ya kisiasa na kijeshi ya nchi zilizokuwa zikipigana vita hivyo, ikiwa ni pamoja na kuainisha hatima ya ardhi zilizokuwa chini ya madola waitifaki.

Churchill, Roosevelt and Stalin

Siku kama ya leo miaka 72 iliyopita nchi ya Sri Lanka ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Muingereza. Nchi hiyo iliyoko kusini mashariki mwa India ilivamiwa na wakoloni wa Kireno katikati mwa karne ya 16 na baadaye wakoloni wa Kiholanzi na tangu mwaka 1798 iliunganishwa rasmi na makoloni ya Uingereza. Mapambano ya kupigania uhuru wa Sri Lanka yalianza mwanzoni mwa Vita vya Kwanza vya Dunia. Mwaka 1931 Uingereza ililazimika kutoa haki ya kutoa maoni kwa wananchi wa Sri Lanka na kuasisi baraza la kutunga sheria na baraza la utekelezaji. Hata hivyo nchi hiyo ilikuwa bado haijapata uhuru kamili katika masuala ya kigeni. Kwa msingi huo mapambano ya wananchi yaliendelezwa hadi kisiwa hicho kilipopata uhuru kamili mwaka 1948.

Bendera ya Sri Lanka

Katika siku kama ya leo miaka 41 iliyopita wakati mapambano ya wananchi dhidi ya utawala wa Shah yalipokuwa yamefika kileleni, Waziri Mkuu wa utawala wa kifalme hapa nchini Shapour Bakhtiar alifanya jitihada za kuzima vuguvugu la wananchi bila ya mafanikio yoyote. Bakhtiar alisema katika mahojiano na vyombo vya habari kwamba, hatamruhusu Imam Khomeini kuunda serikali ya mpito. Wakati huo uasi wa kiraia, kukimbia wanajeshi na kujiunga na safu za wananchi katika miji mbalimbali ya Iran ikiwa ni pamoja na kujiuzulu wabunge, viongozi wa ngazi za juu serikali na kadhalika viliifanya serikali ipoteze udhibiti wa mambo ndani ya nchi.

ورود امام خمینی (ره ) به ایران

Na siku kama ya leo miaka 4 iliyopita aliaga dunia Raghib Mustafa Ghalwash qarii na msomaji Qur'ani mahiri wa Kimisri. Ghalwash alizaliwa Julai 5 mwaka 1938 nchini Misri na kukulia katika familia iliyokuwa na mapenzi makubwa na Qur'ani. Raghib Mustafa Ghalwash alikuwa tayari amehifadhi Qur'ani nzima katika rika la ubalobaro na kuanza kusoma kitabu hicho katika hafali na majlisi mbalimbali akiwa na umri wa miaka 16. Sheikh Raghib Mustafa Ghalwash alikuwa miongoni mwa wasomaji wa Qur'ani waliofanya safari nchini Iran baada ya kumalizika vita vya kulazimishwa vilivyoanzisha na Iraq dhidi ya Iran. Qiraa na kisomo cha gwiji huyo wa Misri kilipendwa sana nchini Iran. Hatimaye Qarii huyo mashuhuri aliaga dunia alfajiri ya Alkhamisi tarehe 4 Februari mwaka 2016 akiwa na umri wa miaka 77 baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Raghib Mustafa Ghalwash

 

 

Tags