Feb 08, 2020 11:08 UTC
  • Mapinduzi ya Kiislamu, mlinganiaji wa uadilifu na maendeleo

Assalaamu Alaykum wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Tunakutana tena katika mfululizo wa vipindi hivi maalumu vya Alfajiri Kumi ambacho ni kipindi cha tangu siku aliporejea Imam Khomeini kutoka uhamishoni hadi kupata ushindi Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini Iran

 

Kipindi chetu cha leo kina anuani isemayo: Mapinduzi ya Kiislamu, mlinganiaji wa uadilifu na maendeleo. Kuweni nami hadi mwisho wa dakika hizi chache ili mtegee sikio kile nilichokuandalieni kwa leo. Karibuni.

Kwa ushahidi wa Qur'ani Tukufu, dini zote za mbinguni zililiweka suala la uadilifu kuwa ndilo lengo lao. Ni kwa msingi huo ndio maana Mwenyezi Mungu anasema katika Aya ya 25 ya Surat al-Hadid kwamba:

لَقَدْ أَرْسَلْنا رُسُلَنا بِالْبَیِّناتِ وَ أَنْزَلْنا مَعَهُمُ الْکِتابَ وَ الْمیزانَ لِیَقُومَ النَّاسُ بِالْقِسْطِ

Kwa hakika tuliwatuma Mitume wetu kwa dalili waziwazi, na tukateremsha Kitabu pamoja nao na Mizani, ili watu wasimamie uadilifu.

Aya hii inabainisha lengo la kutumwa Mitume, kuteremshwa vitabu na kuja Manabii kwamba, ni kutekeleza uadilifu na kuueneza katika jamii ya mwanadamu. Neno Bayyinaat yaani hoja na dalili za wazi lililokuja katika Aya iliyotangulia lina maana ya hoja na dalili za wazi kabisa, madhubuti na ambazo haiwezekani kuzitilia shaka ambazo Mitume walikuwa wakizitoa. Ama neno Kitabu lililokuja katika Aya tuliotangulia kuisoma nalo lina maana ya mwongozo na dira ya dini kuhusiana na maarifa, hukumu na maadili. Aidha neno Mizani ambalo nalo limekuja katika Aya hiyo lina maana ya kipimo, kigezo na chombo cha kupimia na kuleta uadilifu katika maeneo mbalimbali ya jamii ya mwanadamu huyu. Kadhalika katika kipindi chote cha historia yao, Manabii wa Mwenyezi Mungu walikuwa kando na watu waliodhulumiwa na wasio na uwezo na daima daghadagha na hangaiko lao kubwa lilikuwa ni kutekeleza uadilifu na usawa katika jamii.

 

Tukirejea katika Kitabu Kitakatifu cha Qur'ani tunapata imeelezwa bayana na wadhiha kabisa kwamba, Manabii wa Allah daima walikabiliwa na changamoto kubwa za mataghuti, mabwanyenye na makabaila waliokuwa wakidhulumu na kukandamiza watu wengine. Hii ilitokana na kusimama kwao kidete na kutokubaliana na dhulma na ukandamizaji wao. Aya ya 34 katika Surat Sabaa inasema:

وَمَا أَرْسَلْنَا فِی قَرْیَةٍ مِّن نَّذِیرٍ إِلاَّ قَالَ مُتْرَفُوهَا إِنَّا بِمَا أُرْسِلْتُم بِهِ کَافِرُونَ

Na hatukumtuma mwonyaji yeyote kwenye mji, ila walisema waliojidekeza kwa starehe zao wa mji huo: Hakika sisi tunayakataa hayo mliyotumwa nayo.

 

Dini zote zinakubaliana kwa kauli moja kwamba, mwisho wa harakati hii adhimu na kubwa ya kihistoria ni mwisho wenye matumaini ya kupatikana uadilifu na kipindi cha dini kutawala kikamilifu duniani. Tunasoma katika dua baada ya ziara ya Aal Yassin:

یَمْلَأُ اَلْأَرْضَ قِسْطاً وَ عَدْلاً کَمَا مُلِئَتْ ظُلْماً وَ جَوْراً

"Ili aje kuijaza dunia kwa uadilifu na usawa kama ambavyo itakuwa imejaa dhulma na uonevu."

Manabii wote, dini zote na Mitume wote waliashiria mwisho huu wenye matumaini na wote waliegemea na kutegemea suala la uadilifu katika njia na harakati zao. Uislamu umetangazwa na Qur'ani Tukufu kwamba, ndiyo dini pekee inayoridhiwa na Mwenyezi Mungu na ni maktaba ya uadilifu na kufanya mambo kwa wastani kama ambavyo Umma wa Kiislamu nao unaelezwa kuwa ni Umma wa wastani ili uwe mashahidi wa watu.

ا

 

Aya ya 143 ya Surat al-Baqara inasema:

کَذَلِکَ جَعَلْنَاکُمْ أُمَّةً وَسَطًا لِّتَکُونُواْ شُهَدَاء عَلَى النَّاسِ

Na vivyo hivyo tumekufanyeni muwe Umma wa wastani, ili muwe mashahidi juu ya watu.

Moja ya malengo ya muda mrefu ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ni kutekeleza fikra za Manabii na kupatikana matumaini ya wanaompwekesha Mwenyezi Mungu. Yaani kuunda mjumuiko wa watu ambao wataishi maisha yao kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu. Imam Ruhullah Khomeini (MA) mwasisi wa Mapinduzi ya Kiislamu alikuwa akiyatambua mapinduzi haya kwamba, yana tofauti na mapinduzi mengine yaliyotokea katika maeneo mbalimbali ya dunia. Mtazamo huo wa Imam Khomeini ulitokana na kuwa, Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalijengeka juu ya msingi wa malengo matukufu ambapo uadilifu na umaanawi kwa maana yake pana vilikuwa vikitembea katika mishipa ya damu ya mapinduzi haya.

Kwa hakika uadilifu ni mafuhumu ambayo uhakika wake upo katika fitra na maumbile ya mwanadamu aliyopatiwa na Mwenyezi Mungu. Kila mtu mwenye dhamira safi basi katika moyo wake kuna kiu cha uadilifu. Hata kafiri anapohisi uadilifu unakanyagwa na dhulma inafanyika, hupaza sauti ya kutaka uadilifu. Hapana shaka kuwa, kutekelezwa uadilifu huandaa uwanja na mazingira mwafaka kabisa ya kupatikana utukufu, hadhi na heshima ya mwanadamu. Ni kwa muktadha huo, ndio maana kutekeleza uadilifu kunaunda msingi na kujenga harakati za Mitume wa Mwenyezi Mungu.

 

Kwa hakika uadilifu ni matumaini makongwe na ya kale ya wanadamu waliodhulumiwa katika historia yote ya kiumbe mwanadamu. Hii leo fikra za mwanadamu zimechoshwa na mamlaka ya kimabavu na ukandamizaji katika mifumo ya jamii, na mwanadamu wa leo ana kiu kikali cha uadilifu na analitafuta hilo kama kito cha thamani ambacho upatikanaje wake ni mgumu; na anakimbia ukosefu wa uadilifu, miamala ya kidhulma na ukiukaji wa haki mambo ambayo yameyafanya maisha yake yawe mabaya na yasiyo na amani na utulivu.

Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndio maana Ayatullahh Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran anasema: Kama uadilifu utadhaminiwa, basi haki na utukufu wa mwanadamu pia vitadhaminiwa na hali hiyo itawafanya watu kufikia na kupata haki na uhuru wao.

 

Uadilifu maana yake ni kuweka kila kitu mahala pake na kutoa haki kwa kila kitu na kwa kila mtu. Hatua ngumu zaidi ya kila mapinduzi au utawala ni kutekeleza uadilifu. Kutekeleza uadilifu kunahitajia sera na mipango madhubuti na kuvumilia mambo magumu katika njia hiyo na hata gharama zake; kwani katika baadhi ya jamii huenda kiongozi muadilifu akakumbwa na misukosuko.

Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yamejengeka juu ya msingi wa wito wa dini na kupigania uadilifu. Msimamo huu katu hauyafurahishi madola ya kibeberu ambayo ada na mazoea yao ni kukandamiza madola mengine.

Na Ndio maana tangu kutokea Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran mwaka 1979, madola ya kitwaghuti hayajasitisa uadui wao hata siku moja dhidi ya taifa hili ambalo haliko tayari kuburuzwa au kutwishwa siasa za mabeberu ambao daima wanachokijali wao ni maslahi yao tu. Mbali na uadilifu, Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yamekuwa yakifanya kila yawezalo kuwaletea maendeleo wananchi wa taifa hili. Na ndio maana tunashuhudia kwamba, licha ya njama za kila leo za maadui dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu, lakini taifa hili limesimama kidete na kufanikiwa kupiga hatua kubwa za kimaendeleo katika nyanja mbalimbali tena kwa kutegemea wataalamu na vijana shupavu na waumini wa hapa nchini.

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu hiki maalumu cha Alfajiri Kumi umefikia tamati. Ninakuageni nikikutakieni usikilizaji mzuri wa vipindi vyetu vingine. Ahsanteni na kwaherini.