Mar 26, 2020 04:16 UTC
  • Alkhamisi, tarehe 26 Machi, 2020

Leo ni Alkhamisi tarehe Mosi Shaaban mwaka 1441 Hijria sawa na tarehe 26 Machi mwaka 2020.

Mwezi wa shaabani unaoanza leo ni mwezi wa ibada, kujipinda na kuomba maghufira. Mtume Muhammad (saw) aliutukuza mno mwezi huu na kuuita kuwa ni mwezi wake. Mtume na maimamu watoharifu katika kizazi chake waliusia mno kufanya ibada hususan kufunga swaumu katika mwezi huu wa Shaabani kwa sababu ndio unaotayarisha uwanja mzuri wa kuingia kwenye mwezi wa ugeni wa Mwenyezi Mungu na wenye baraka tele wa Ramadhan. Katika mwezi huu wa Shaabani kumetukia mambo mengi muhimu kama kuzaliwa Imam Hussein bin Ali (as) mjukuu wa Bwana wetu Muhammad (saw) na pia tukio la kuzaliwa Imam wa Zama, Mahdi (as) Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake.

Tarehe Mosi Shaabani miaka 175 iliyopita alifariki dunia mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu Sheikh Muhammad Hassan Najafi maarufu kwa lakabu ya Sahib al Jawahir. Sahib al Jawahir alifanya uhakiki mkubwa wa masuala ya fiqhi na kusajili fikra zake katika taaluma hiyo kwa njia ya kuvutia na nyepesi. Kitabu kikubwa zaidi cha mwanazuoni huyo ni "Jawahirul Kalam" ambacho kina thamani na umuhimu mkubwa sana kati ya wataalamu wa taaluma hiyo. Katika kitabu hicho Sheikh Muhammad Hassan Najafi ameandika masuala ya kifiqhi na sheria za Kiislamu kwa kutumia hoja madhubuti na uangalifu mkubwa.

Sheikh Muhammad Hassan Najafi

Siku kama hii ya leo miaka 109 iliyopita alizaliwa mwandishi mashuhuri wa michezo ya kuigiza wa Marekani, Tennessee Williams. Alivutiwa sana na fasihi na mvuto huo ulikolea na kuimarika zaidi wakati alipokuwa masomoni katika chuo kikuu na hatimaye alifanikiwa kuwa mwandishi mkubwa. Tennessee Williams alitumia uhodari wake kueleza fikra zake kwa lugha ya michezo ya kuigiza. Kazi zake nyingi zilieleza hali ya watu wa tabaka la chini na wanaosumbuliwa na ukata katika jamii ya Marekani. Miongoni mwa kazi za mwandishi huyo mashuhuri ni Cat on a Hot Tin Roof, Sweet Bird of Youth na The Glass Menagerie. 

Tennessee Williams

Siku kama ya leo miaka 68 iliyopita, yalianza mapambano ya Mau-Mau yakiongozwa na Mzee Jomo Kenyatta, mwasisi wa nchi huru ya Kenya, dhidi ya wakoloni wa Kiingereza. Katika kipindi cha vita viwili vikubwa vya dunia, Kenya ilikumbwa na machafuko na vurugu nyingi. Hata hivyo baada ya Vita vya Pili vya Dunia, wananchi wa nchi hiyo waliamua kupambana kufa na kupona ili kuikomboa nchi yao kutoka mikononi mwa wakoloni wa Ulaya. Wakoloni wa Kiingereza waliweka sheria kali katika maeneo tofauti ya Kenya hasa katika maeneo ya Wakikuyu lakini hilo halikuzuia kuasisiwa harakati ya Mau-Mau. Kaulimbiu kuu ya wapiganaji wa Mau-Mau ilikuwa ni kuweko usawa na uadilifu katika masuala ya kijamii na kisiasa baina ya wenyeji wa Kenya na Wazungu. Hatimaye harakati hiyo ya Mau-Mau kwa uongozi wa Mzee Jomo Kenyatta ilifanikiwa kuikomboa Kenya kutoka mikononi mwa wakoloni wa Kiingereza mwanzoni mwa muongo wa 60. 

Mzee Jomo Kenyatta

Tarehe 26 Machi mwaka 1971 katika siku kama hii ya leo, Pakistan Mashariki ambayo hivi sasa inajulikana kwa jina la Bangladesh iliamua kujitenga na Pakistan baada ya kuzuka mivutano mikubwa ya kisiasa na uasi nchini humo. Pakistan Mashariki na ile ya Magharibi ilikuwa nchi moja, iliyoamua kujitenga na India mwaka 1947. Wabangladeshi waliokuwa wakiishi Pakistan Mashariki na kuunda jumla ya asilimia 98 ya watu wa eneo hilo, hawakuridhishwa na vitendo vya kibaguzi vilivyokuwa vikifanywa na serikali kuu huko Pakistan Magharibi na kwa msingi huo awali walitaka kupewa mamlaka ya kujiendeshea mambo yao wenyewe. Baadaye walianzisha mapambano ya silaha na kufanikiwa kulifukuza jeshi la Pakistan Magharibi wakisaidiwa na jeshi la India. Pakistani Mashariki ilipewa jina la Bangladesh. 

Bendera ya Bangladesh

Miaka 36 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia Ahmad Sekou Toure kiongozi mkubwa wa nchi ya Kiafrika ya Guinea. Sekou Toure alizaliwa Januari 9 mwaka 1922 katika moja ya miji ya katikati mwa Guinea. Aliingia katika harakati za kisiasa akiwa katika rika la ujana na alikuwa akitaka uhuru wa  chi yake kutoka kwa wakoloni wa Kifaransa. Hatimaye mwaka 1958 nchi hiyo ilipata uhuru na mwaka mmoja baadaye Touré akateuliwa kuwa rais na kusalia madarakani hadi mwaka 1984 alipofariki dunia.

Ahmad Sekou Toure

 

Tags