Jumamosi, 23 Mei, 2020
Leo ni Jumamosi tarehe 29 ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani 1441Hijria sawa na tarehe 23 Mei 2020 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 793 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, alizaliwa mwanazuoni mahiri wa Kiislamu katika mji wa Hillah Iraq, Ayatullah Jamaluddin Hassan bin Yusuf mwenye lakabu ya Allamah Hilli. Awali alisoma kwa baba yake na mjomba wake na akiwa katika rika la ujana alikuwa tayari amefanikiwa kufikia daraja za juu za elimu katika taaluma kama fikihi, usul Fikih, hadithi na kadhalika. Mwanazuoni huyo alikuwa hodari pia katika uga wa uandishi. Miongoni mwa vitabu vya Allamah Hilli ni Tadhkiratul al-Fuqahaaa, Irshadul Adh'han, na Kashful Murad. Alimu huyo aliaga dunia mwaka 726 Hijria. ***
Miaka 634 iliyopita, alifariki dunia Nassirddin Muhammad maarufu kwa Ibn Furat, faqih, mwanahistoria na khatibui wa nchini Misri. Ibn Furat alizaliwa mjini Cairo mwaka 735 Hijiria na kuanza masomo yake akiwa kijana mdogo. Msomi huyo alijikita sana katika masuala ya historia, kiasi cha kumfanya aandike vitabu mbalimbali katika uwanja huo. Miongoni mwa athari muhimu za Ibn Furat ni pamoja na kitabu kiitwacho ‘Taarikhud-Duwal wal-Muluuk’, kitabu ambacho kimeshamili historia na matukio ya karne ya sita Hijria. ***
Katika siku kama ya leo miaka 402 iliyopita, vilianza vita vya miaka 30 vya kidini barani Ulaya. Madhehebu ya Kikristo ya Kiprotestanti yaliundwa mwanzoni mwa karne ya 16 Milaadia na hivyo kuzusha mpasuko mkubwa katika safu za Wakristo. Baada ya hapo, Wakristo wa madhehebu mawili ya Kikatoliki na Kiprotestanti waliingia vitani kwa karne nyingi. Moja ya vita maarufu baina ya Wakristo wa madhehebu hayo mawili, ni vile vilivyotokea kwenye muongo wa pili wa karne ya 17 Milaadia. Vita hivyo viliendelea kwa muda wa miaka 30 mfululizo. Sehemu kubwa ya vita hivyo ilitokea nchini Ujerumani. Vita hivyo vilikuwa na pandashuka nyingi. Katika kipindi chote cha vita hivyo, nchi za Ufaransa, Sweden na Denmark ziliwaunga mkono Wakristo wa Kiprotestanti na serikali ya Uhispatia na Ufalme wa Roma waliwaunga mkono Wakatoliki. Vita vya miaka 30 baina ya madhehebu mawili ya Wakristo huko barani Ulaya, vilimalizika kwa kutiwa saini makubaliano ya Westphalia mwaka 1648 Milaadia. Ijapokuwa uhasama mkubwa baina ya Wakristo wa Kiprotestanti na Kikatoliki ulitokana na ugomvi wa muda mrefu baina ya madhehebu hayo mawili, lakini sababu kubwa za vita hivyo ilikuwa ni kugombania ardhi na masuala ya kisiasa ya tawala za wakati huo barani Ulaya. Moja ya matokeo muhimu ya vita hivyo ni kumalizika kwa namna vita vya kimadhehebu baina ya madhehebu hayo mawili ya Kikristo na kuanza kupata nguvu mirengo ya utaifa na ya ubaguzi wa rangi na kizazi barani Ulaya. ***
Siku kama ya leo miaka 114 iliyopita, aliaga dunia Henrik Ibsen mwandishi wa tamthiliya wa nchini Norway. Alizaliwa mwaka 1828 kusini mwa Norway. Shauku na mapenzi ya Ibsen ya kuwa mwandishi wa tamthiliya ndiyo yaliyomsukuma kwenye taaluma hiyo. Mwandishi huyo wa Kinorway ameandika drama na tamthiliya nyingi. Moja kati ya tamthmliya zake mashuhuri ni ile iitwayo, An Enemy of the People yaani Adui wa Watu. ***
Miaka 105 iliyopita katika siku kama ya leo, Italia ilijiingiza katika Vita vya Kwanza vya Dunia. Kuingia Italia katika Vita vya Kwanza vya Dunia kulianza wakati nchi hiyo ilipoivamia Austria bila ya sababu yoyote isipokuwa tu kwa tamaa ya kujinufaisha kisiasa na kupanua utawala wake. Muda mchache baadaye, serikali ya Italia ilitangaza vita dhidi ya ufalme wa Uthmania na hivyo kuufanya moto wa vita uwake kwa ukali zaidi. Hata hivyo, licha ya kupata ushindi kundi la nchi Waitifaki, Italia ikiwa moja yao, lakini nchi hiyo haikufaidika kivyovyote na vita hivyo. Matunda pekee iliyopata ni kuwaulisha raia wa Italia baada ya kuwaingia Waitaliano milioni tano na nusu katika vita hivyo. Kwa maneno mengine ni kuwa maamuzi na siasa za Italia katika Vita vya Kwanza vya Dunia zilifeli, kwani haikupata matunda yoyote ya maana kwa kujiingiza kwake kwenye vita hivyo. ***
Siku kama ya leo miaka 75 iliyopita, alijiua Heinrich Himmler Mkuu wa zamani wa Shirika la Kijasusi na Usalama la Ujerumani ya Kinazi. Himmler alizaliwa mwaka 1900 na alipofikisha umri wa miaka 34 aliweza kupanda cheo na kuwa mkuu wa shirika hilo la kijasusi na usalama la Ujerumani (Gestapo). Heinrich Himmler anahesabiwa kuwa mmoja kati ya viongozi wauaji na wamwagaji damu ambaye aliongoza operesheni kadhaa za mateso na kuuwa watu nchini humo. Himmler alitiwa mbaroni baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia na kuhukumiwa adhabu ya kifo kwenye mahakama ya Nurenberg nchini Ujerumani, lakini kabla ya kutekelezwa hukumu hiyo aliamua kujiua mwenyewe baada ya kunywa sumu. ***
Na katika siku kama ya leo miaka 38 iliyopita, mji wa Khorramshahr wa Iran ulikombolewa na wapiganaji wa Kiislamu na ukaondoka katika uvamizi wa majeshi vamizi ya Iraq. Mji wa Khorramshahr uko katika mkoa wa Khozestan kusini magharibi mwa Iran. Mji huo ulikuwa chini ya uvamizi wa majeshi ya Iraq kwa muda wa karibu mwaka mmoja na miezi minane. Uvamizi dhidi ya mji huo ulijiri mwanzoni mwa vita vya miaka minane vya kulazimishwa vya utawala wa Saddam wa Iraq dhidi ya Iran. Ama wapiganaji shupavu wa Iran waliokuwa wamejihami kwa silaha ya imani ya kumtegemea Mwenyezi Mungu walipambana kishujaa na kufanikiwa kuwapa pigo kubwa wanajeshi vamizi wa Iraq na hatimaye kuukomboa mji wa Khorramshahr na hivyo kuibua hamasa ya aina yake jambo ambalo liliwashangaza weledi wa mambo ya kijeshi duniani. Siku hii ya kukumbuka kukombolewa mji wa Khorramshahr inajulikana katika utamaduni wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kuwa, "Siku ya Muqawama na Ushindi". ***