Jumatatu, tarehe 15 Juni, 2020
Leo ni Jumatatu tarehe 23 Shawwal 1441 Hijria sawa na Juni 15 mwaka 2020.
Katika siku kama ya leo miaka 329 iliyopita alifariki dunia Sayyid Neematulllah Jazairi aliyekuwa faqihi na mpokezi mkubwa wa hadithi wa Kiislamu akiwa na umri wa miaka 62. Alikuwa hodari katika elimu za fiqhi, hadithi, tafsiri ya Qur'ani na fasihi ya lugha ya Kiarabu na alistahamili mashaka mengi katika njia ya kulingania sheria za dini ya Kiislamu. Sayyid Neematullah Jazairi ameandika vitabu kadhaa vya thamani kama Madinatul Hadith, Qiswasul Anbiyaa na Hidayatul Muuminin.
Siku kama ya leo miaka 172 iliyopita sawa na tarehe 15 Juni 1848, Otto von Bismarck Kansela wa Ujerumani aliuchagua mji wa kihistoria na maarufu wa Berlin, kuwa mji mkuu wa nchi hiyo. Kuteuliwa mji wa Berlin kuwa mji mkuu wa Ujerumani, kulitokana na utekelezaji wa mpango wa kuziunganisha Ujerumani mbili, uliobuniwa na Kansela Bismarck. Baada ya Vita vya Pili vya Dunia, Ujerumani iligawanyika katika sehemu mbili za Mashariki na Magharibi. Mwezi Septemba 1990 baada ya kuvunjwa ukuta wa Berlin, kuliandaliwa mazingira ya kuunganishwa pande hizo mbili, na hatimaye Berlin kurejea tena na kuwa mji mkuu wa Ujerumani.
Siku kama ya leo miaka 20 iliyopita, mwafaka na tarehe 15 Juni 2000, idadi kubwa ya askari wa kikosi maalumu cha jeshi la Uingereza iliondoka kwenye ardhi ya Sierra Leone, magharibi mwa Afrika. Amri ya kuondoka vikosi hivyo vya Uingereza ilitangazwa na John Prescott, Naibu Waziri Mkuu wa Uingereza. Wanajeshi wengine 300 wa nchi hiyo waliendelea kubaki nchini Sierra Leone kwa wiki kadhaa kwa shabaha ya kutoa mafunzo kwa jeshi la nchi hiyo.
Siku kama ya leo miaka 13 iliyopita, alifariki dunia Ayatullahil-udhma Sheikh Muhammad Fadhil Lankarani aalimu na marjaa mkubwa wa Kiislamu baada ya kuugua. Allamah Fadhil Lankarani alizaliwa mnamo mwaka 1310 Hijria Shamsia katika mji wa kidini wa Qum huko kusini mwa Tehran na kuanza kujifunza masomo ya dini akiwa kijana mdogo. Aidha alipata kustafidi na mafunzo ya walimu wakubwa wa zama zake kama vile Ayatullahil udhma Burujerdi na Imam Khomeini Mwenyezi Mungu awarehemu. Ayatullahil Udhma Sheikh Muhammad Fadhil Lankarani katika kipindi kifupi aliweza kufikia daraja ya ijtihad.