Jumapili, Disemba 6, 2020
Leo ni Jumapili, tarehe 20 Mfunguo Saba Rabiuthani 1442 Hijria inayosadifiana na Disemba 6, 2020 Milaadia
Miaka 67 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani ya Hijria Shamsia, wanachuo wa Chuo Kikuu cha Tehran walifanya maandamano ya kupinga kuja nchini Iran Makamu wa Rais wa Marekani wakati huo, Richard Nixon. Askari wa Shah waliua wanachuo watatu katika maandamano hayo. Safari hiyo ilifanywa na Nixon miezi mitatu na nusu baada ya Marekani kufanya mapinduzi ya kijeshi yaliyoipindua serikali ya Dk Mosaddiq. Nixon aliamua kuja Iran ili kufaidika na mapinduzi hayo ya kijeshi, lakini alikumbwa na upinzani mkubwa wa wanafunzi wa vyuo vikuu. Askari wa kikosi maalumu cha Shah walitumwa katika Chuo Kikuu cha Tehran wakawashambulia wanafunzi na kuua wanachuo watatu. Siku moja tu baada ya mauaji hayo, Nixon alipewa cheti cha ufakhari cha uzamivu katika chuo kikuu hicho. Siku hii imetangazwa kuwa ni Siku ya Wanafunzi wa Vyuo Vikuu nchini Iran kutokana na umuhimu wake mkubwa.
Tarehe 6 Disemba miaka 28 iliyopita, Wahindu wenye misimamo mikali waliubomoa Msikiti wa Babri katika mji wa Faizabad kwenye jimbo la Uttar Pradesh nchini India. Msikiti huo ulijengwa mwaka 1528 na Zahiruddin Muhammad Babur juu ya kilima na tangu wakati huo ulijulikana kwa jina la Msikiti wa Babri. Baada ya kupita karne tatu tangu ujengwe yaani mwaka 1855, mtawala mmoja Muingereza alipotosha ukweli kwa makusudi na kuandika kuwa msikiti huo umejengwa kwenye magofu ya jumba la ibada ya masanamu la Wahindu. Suala hilo lilikuwa chanzo cha fitina na ugomvi mkubwa kati ya Waislamu na Wahindu. Mwaka 1992 Wahindu wenye misimamo ya kufurutu mipaka walivamia Msikiti wa Babri na kuubomoa kikamilifu, suala ambalo lilizusha vita baina ya Waislamu na Wahindu au kwa jina jingine Mabaniani.
Miaka 242 iliyopita katika siku kama ya leo, sawa na tarehe 6 Disemba mwaka 1778, alizaliwa Joseph Louis Gay-Lussac mwanafizikia na mwanakemia wa Ufaransa. Gay-Lussac amefanya tafiti nyingi na kugundua vitu tofauti katika kipindi cha maisha yake. Miongoni mwa aliyoyagundua mwanakemia huyo ni gesi ya sumu ya halogen, kipimio cha ulevi, hydromita au chombo cha kupimia uzito wa maji na viowevu na kuitambua Chloride na Iodine kama elementi mpya. Miongoni mwa kazi muhimu za kisayansi alizofanya mwanakemia huyo ni kuweka kanuni ya kupanuka kwa gesi. Kanuni hiyo iliyopewa jina lake pamoja na la mshirika wake ilijulikana kama Law of Charles and Lussac. Gay-Lussac alifariki dunia mwaka 1850.
Siku kama ya leo miaka 103 iliyopita inayosadifiana na 6 Disemba 1917, nchi ya Finland iliyokuwa chini ya utawala wa Russia ilijipatia uhuru wake. Kuwa jirani Finland na Russia kuliwatia wasi wasi mno viongozi wa Finland, kiasi kwamba, katika karne ya 12 Miladia, waliiomba Sweden iwahami dhidi ya Moscow. Hata hivyo, Wasweden waliikalia kwa mabavu Finland. Mwaka 1721 Russia iliivamia Finland na kudhibiti sehemu ya ardhi ya nchi hiyo. Hatimaye mwaka 1917 vikosi vamizi vya Russia vililazimika kuondoka nchini Finland na nchi hiyo ikajitangazia uhuru.