Ijumaa, 01 Januari, 2021
Leo ni Ijumaa tarehe 17 Mfunguo Nane Jamadil-Awwal 1442 Hijria sawa na tarehe Mosi Januari mwaka 2021 Miladia
Leo ni tarehe Mosi Januari inayosadifiana na kuanza mwaka mpya wa 2021 Miladia. Mpangilio wa miezi ya mwaka wa Kirumi unaoanza Januari hadi Disemba ulianza kutumiwa katika kipindi cha Mfalme Numa Pompilius yapata miaka 700 kabla ya kuzaliwa Nabii Issa Masih (as). Kwa msingi huo tarehe 31 Disemba huwa siku ya mwisho ya mwaka wa Miladia na usiku wa kuamkia tarehe Mosi Januari huanza sherehe za kupokea mwaka mpya katika jamii za Wakristo na nchi nyingi za Afrika, America, Ulaya, Australia na hata Asia.
Miaka 992 iliyopita alizaliwa mmoja wa wasomi na wanafalsafa wakubwa wa Kiislamu na Kiirani kwa jina la Abu Hamid Muhammad Ghazali, maarufu kwa jina la Imam Muhammad Ghazali. Ghazali alisoma elimu ya fiq'hi kutoka kwa Abu Nasri Ismail na baada ya kufikia umri wa miaka 28 alikuwa mmoja wa wasomi wakubwa wa Kiislamu katika elimu hiyo. Umaarufu wa Imam Muhammad Ghazali ulipelekea kiongozi wa Iraq wakati huo Khoja Nidham al-Mulk kumwalika msomi huyo kwenda mjini Baghdad kwa ajili ya kufundisha. Hatimaye alirejea Iran na kujishughulisha na masuala ya ualimu. Kabla ya kurejea Iran, Imam Muhammad Ghazali alipata kuandika vitabu vya thamani kama "Ihyau Ulumud Din," "Kemia ya Saada" na "Nasaha za Wafalme.
Siku kama ya leo miaka 127 iliyopita Heinrich Rudolf Hertz mwanafizikia na mwanahisabati wa Ujerumani aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 37. Alizaliwa mjini Hamburg Ujerumani mwaka 1857. Alikuwa na mapenzi makubwa na fizikia na umakenika tangu akiwa kijana mdogo. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana akajiendeleza kimasomo katika uwanja huo.
Miaka 65 iliyopita katika siku kama ya leo nchi ya Sudan ilipata uhuru kutoka kwa Misri na Uingereza. Mwaka 1899 Uingereza na Misri zilitiliana saini mkataba wa kuitawala kwa pamoja Sudan. Katikati mwa karne ya 20 lilianza vuguvugu la kutaka kujipatia uhuru nchini Sudan na mwaka 1956 Misri na Uingereza zikalazimika kuutambua uhuru wa nchi hiyo.
Miaka 217 iliyopita sawa na tarehe Mosi Januari mwaka 1804 Miladia nchi ya Haiti ilijitangazia uhuru ikiwa nchi ya kwanza kufanya hivyo katika eneo la Amerika ya Latini. Uhuru wa Haiti ulipatikana kufuatia mapambano na harakati kubwa ya watumwa weusi wa nchi hiyo dhidi ya vitendo vya utumwa vya Ufaransa na kisha baadaye kuanzisha mapambano dhidi ya jeshi la Ufaransa. Ufaransa ilianza kuikoloni Haiti mwaka 1677. Baada ya kujipatia uhuru, Haiti ilikumbwa na machafuko ya ndani.