Jumatatu tarehe 5 Aprili mwaka 2021
leo ni Jumatatu tarehe 22 Shaabani 1442 Hijria sawa na Aprili 5 mwaka 2021.
Siku kama ya leo miaka 854 iliyopita alifariki dunia Ibn Shahr Ashub, alimu na mtaalamu mkubwa wa elimu ya hadithi. Muhammad Bin Ali Ibn Shahr Ashub alizaliwa katika mji wa Mazandaran nchini Iran na kupewa jina la Ibn Shahr Ashub kama ambavyo pia alipewa lakabu ya 'Zainud-Din na Rashidud-Din,' ambapo alitambuliwa kuwa na upeo wa juu wa elimu ya theolojia, hatibu, mtaalamu wa elimu ya fasihi na kadhi mashuhuri wa Waislamu wa Kishia. Kutokana na masuala ya kimadh'hab, Ibn Shahr Ashub alilazimika kuondoka Iran katika kipindi cha utawala wa Maseljuq na kukimbilia mjini Aleppo, Syria ya leo. Aliheshimiwa sana na hata wasomi wakubwa wa Kisuni wa zama zake. Ibn Shahr Ashub alipewa idhini ya kupokeza hadithi na maulama wakubwa wa zama zake kama vile Zamakhshari, Imam Muhammad Ghazali na Khatwib Khawarazmi. Miongoni mwa athari za msomi huyo ni pamoja na kitabu cha 'Maalimul-Ulamaa' 'Manaaqib Aali Abi Twalib' 'Mutashaabihul-Qur'an' na 'Al-Arbaiin.'
Siku kama ya leo miaka 669 iliyopita Ibn Hajar Asqalani, faqih, mwanahadithi, mwanahistoria na mshairi Mwislamu wa Misri alizaliwa mjini Cairo Misri. Alimpoteza baba yake mzazi alipokuwa na umri wa miaka mitano tu na katika umri huo akaanza kujifunza Qur'ani Tukufu pamoja na masomo mengine ya kidini. Kufikia miaka 10 alikuwa amehifadhi Qur'ani nzima na alisafiri katika nchi tofauti kwa lego la kupata masomo ya juu. Alionyesha kipawa na ujuzi mkubwa katika taaluma ya hadithi kiasi kwamba alifahamika kwa jina la Muhifadhi Mkubwa wa Hadithi. Ibn Hajar Asqalani anahesabiwa kuwa mmoja wa waandishi mashuhuri katika ulimwengu wa Kiislamu, kwa kadiri kwamba ameandika vitabu vinavyopata 150. Miongoni mwa vitabu hivyo ni Lisaan al-Mizaan, Fat'h al-Bari fii Sharh Hadith al-Bukhari na al-Ishara fii Tamyiz as-Swahaba. Ibn Hajar al-Asqalani aliaga dunia mwaka 852 Hijiria.
Siku kama ya leo miaka 436 iliyoyopita yaani 5 Aprili 1585, yalifanyika mauaji ya halaiki katika mji wa Harlem nchini Uholanzi, ambacho kilikuwa kitovu cha wapigania uhuru nchini humo. Mauaji hayo yalifanyika kwa amri ya Mfalme wa Uhispania. Jumla ya watu elfu sita wanaaminika kuwa waliuawa kwenye shambulio hilo. Hatimaye Uholanzi ilijipatia uhuru kutoka kwa mkoloni Uhispania hapo mwaka 1609.
Tarehe 5 Aprili 227 iliyopita, aliuawa Georges Danton mmoja kati ya viongozi wa mapinduzi ya Ufaransa. Danton licha ya kusomea taaluma ya sheria, alikuwa mhamasishaji mzuri katika kipindi cha mapinduzi ya Ufaransa. Danton alikuwa akiamini kuwa, sanjari na kuzuia machafuko na maafa ya kibinadamu, utawala wa kifalme nchini Ufaransa ulipaswa kutokomezwa. Amma Robes Pierre mmoja kati ya vinara wakubwa wa mapinduzi ya Ufaransa ambaye pia alikuwa mshindani wa Danton alichukua uamuzi wa kimtia mbaroni Danton na hatimaye kumuuwa.
Siku kama ya leo miaka 88 iliyopita alifariki dunia Allamah Sheikh Muhammad Jawad Balaghi, mmoja wa maulama wakubwa wa Kiislamu. Katika zama zake alikuwa mtaalamu wa elimu ya fiqhi, mwalimu na mwandishi mkubwa. Allamah Balaghi alipata kusoma kwa maulama wakubwa wa zama zake kama vile Mirza Shirazi na kutokea kuwa mmoja wa walimu na waandishi wakubwa wa ulimwengu wa Kiislamu. Miongoni mwa athari za msomi huyo ni pamoja na kitabu kinachoitwa 'Al Balaghul-Mubin' kinachothibitisha uwepo wa Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Na siku kama ya leo miaka 65 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 5 Aprili 1956, yalimalizika mashambulizi ya kinyama ya majeshi ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya wananchi wa Palestina katika eneo la Ukanda wa Gaza. Majeshi hayo, tarehe 4 Aprili, yalianza kufanya mashambulio makubwa na kuwauwa watu 56 na kuwajeruhi wengine 30 wengi wao wakiwa wanawake, watoto na wazee katika kipindi cha siku mbili. Nchi za Magharibi na jamii ya kimataifa hazikutoa radiamali yoyote kuhusiana na jinai hizo za Wazayuni.