Jul 17, 2021 02:38 UTC
  • Jumamosi, 17 Julai, 2021

Leo ni Jumamosi tarehe 6 Mfunguo Tatu Dhul-Hija 1442 Hijria mwafaka na tarehe 17 Julai 2021 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1184 iliyopita, yaani sawa na tarehe 6 Dhul-Hijja mwaka 258 Hijiria, alizaliwa Abu Ali Muhammad ibn Hammam, mmoja wa maulama mashuhuri wa Iran. Ibn Hammam alikuwa akiishi mjini Baghdad, Iraq ambapo alifanikiwa kusoma elimu ya hadithi kutoka kwa maulama wakubwa wa enzi zake. Aidha msomi huyo alikuwa na idadi kubwa ya wanafunzi ambao walijifunza toka kwake elimu ya hadithi na elimu nyingine za Kiislamu. Msomi huyo ameacha vitabu kadhaa katika uga wa hadithi. ***

Abu Ali Muhammad ibn Hammam

 

Miaka 108 iliyopita Profesa Roger Garaudy, mwanafalsafa na mwanafikra wa Ufaransa alizaliwa huko katika mji wa Marseille. Garaudy alipata shahada ya daraja ya udaktari katika taaluma tatu za masomo ya falsafa, fasihi na utamaduni. Roger Garaudy alifungwa jela katika kambi ya mateka wa kivita wa Ujerumani tangu mwaka 1940 hadi 1943 kutokana na mapambano yake dhidi ya ufashisti wa Adolph Hitler wakati Ufaransa ilipokaliwa kwa mabavu na Ujerumani. Profesa Garaudy alikuwa mwanachama wa chama cha Kikomonisti cha Ufaransa kwa miaka 36 na pia mwanachama wa kamati kuu ya chama hicho kwa miaka 25. Hata hivyo mitazamo ya kikomunisti na kiliberali haikuweza kukata kiu ya kutafuta ukweli ya msomi huyo wa Ufaransa na hatimaye alikubali dini ya tukufu ya Uislamu baada ya kufanya utafiti mkubwa. Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran mwaka 1979 ulikuwa na taathira kubwa katika mitazamo ya Profesa Roger Garaudy. ***

Profesa Roger Garaudy

 

Katika siku kama ya leo miaka 53 iliyopita, chama cha Baath cha Iraq kilichukua hatamu za uongozi kupitia mapinduzi yaliyoongozwa na Ahmad Hassan al-Bakr na kumpindua Rais Abdulrahman Aarif. Baada ya kuchukua madaraka chama cha Baath, Saddam Hussein ambaye alikuwa kiongozi nambari mbili wa chama hicho alianza kuwauwa wapinzani wake nchini Iraq na vikosi vya usalama na vya jeshi la nchi hiyo pia vikaanzisha hujuma kali dhidi ya wapinzani wa Kikurdi, wazalendo, wanaharakati wa Kiislamu na hata Wakomonisti. ***

Ahmad Hassan al-Bakr

 

Siku kama ya leo miaka 41 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia, Baraza la kwanza la Kulinda Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran lilianza rasmi kazi zake. Kwa mujibu wa kifungu nambari 91 cha Katibu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kwa lengo la kulinda sheria za Kiislamu na kuhakikisha kwamba sheria zinazopasishwa na Bunge hazipingani na dini ya Uislamu na Katiba, kuliundwa baraza lililopewa jina la Baraza la Kulinda Katiba. Baraza hilo lina wanazuoni sita wa fiqhi na sheria za Kiislamu wanaoteuliwa na Kiongozi Mkuu wa Iran na wataalamu 6 wa sheria ambao huarifishwa bungeni na kupigiwa kura baada ya kuteuliwa na Idara ya Vyombo vya Mahakama. Wadhifa mkubwa zaidi wa baraza hilo ni kuhakikisha kwamba, sheria zinazopasishwa na Bunge hazipingani na sheria za Kiislamu na Katiba, kufasiri Katiba na kusimamia chaguzi mbalimbali hapa nchini. ***

Baraza la Kulinda Katiba

 

Katika siku kama ya leo miaka 35 iliyopita, mamia ya mahujaji wa Iran na wengine kutoka nchi tofauti waliokuwa wameenda kuzuru Nyumba ya Mwenyezi Mungu mjini Makka na wakiwa katika hali ya kutekeleza ibada ya faradhi ya kujitenga na mushrikina, waliuawa shahidi na askari wa utawala wa Saudi Arabia. Ni vyema kukumbusha kuwa, mahujaji wa Iran kwa miaka yote huwa wanatekeleza ibada hiyo kwa mujibu wa mafundisho ya dini ya Kiislamu na Qur'ani Tukufu, ambapo mbali na kuwasisitizia Waislamu kuungana, hutangaza kujitenga na maadui wa Uislamu hususan Marekani na utawala haramu wa Israel. Ibada hiyo ambayo hufanyika kwa kuhudhuriwa na idadi kubwa ya Mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu, huwa na taathira kubwa katika msimu wa Hija. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana Imam Khomeini mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, akasisitiza sana umuhimu wa ibada ya kujitenga na mushrikina na maadui wa dini ya Kiislamu. ***

Jinsi maafisa usalama wa Saudi walivyowauwa Mahujaji

 

Na miaka 34 iliyopita katika siku kama ya leo kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia uhusiano wa kisiasa wa Iran na Ufaransa ulivunjika wakati wa kujiri vita vya kichokozi vya dikteta Saddam dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Serikali ya wakati huo ya Ufaransa ilitoa himaya na uungaji mkono wa pande zote kwa Iraq wakati wa kuanza hujuma na mashambulio ya jeshi la dikteta Saddam dhidi ya Iran. Aidha wakati wote wa vita hivyo, himaya ya Ufaransa ilichukua wigo mpana zaidi.  Hatimaye katika siku kama ya leo Ufaransa ilichukua hatua ya upande mmoja ya kukata uhusiano wake wa kisiasa na Tehran. ***

Bendera za Iran na Ufaransa

 

Tags