Spoti, Agosti 9
Hujambo mpenzi mwanaspoti wa Radio Tehran. Karibu tuangazie baadhi ya matukio muhimu yaliyojiri viwanjani ndani ya siku zilizopita, ndani na nje ya Iran.
Kombe la Muondoano (Hazfi)
Klabu ya Foolad ya Iran kwa mara ya kwanza kabisa katika historia imeshinda japo kwa mbinde Kombe la Mtoano (Hazfi) baada ya kuizaba Esteqlal mabao 4-2 kupitia mikwaju ya penati katika mchuano wa fainali uliopigwa Jumapili. Katika mchezo huo wa aina yake uliopigwa katika Uwanja wa Naghsh-e Jahan mjini Isfahan, katikati mwa nchi, timu hizo zilikabana koo na kuambulia sare tasa katika dakika 90 za ada na 30 za nyongeza.
Hata hivyo Foolad ya Khuzestan ilijipapatua na kuonesha umbuji wake katika upigaji penati. Esteqlal ndiyo klabu iliyotwaa Kombe la Hazfi mara nyingi katika historia ya taji hilo la muondoana lililoasisiwa mwaka 1975 na Shirikisho la Soka Iran. The Blues ya Tehran imetwaa taji hilo mara saba.
Iran yavuna medali zaidi Michezo ya Olimpiki
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewapongeza wanamichezo wa Iran waliong'ara na kuvuna medali mbali mbali katika Mashindano ya Kimataifa ya Olimpiki ya Tokyo 2020 nchini Japan. Katika salamu zake za tahania, Ayatullah Ali Khamenei amewashukuru wanamichezo wa Jamhuri ya Kiislamu kwa kulipaisha taifa hili na kuliweka katika ramani ya dunia kwa kuibuka kidedea na kutuzwa medali ainati katika mashindano hayo ya kimataifa yaliyofunga pazia lake siku ya Jumapili. Amewapongeza wanamichezo hao kwa jitihada zao na kwa kuliletea furaha katika michezo hiyo ya dunia iliyopaswa kufanyika mwaka jana lakini ikaakhirishwa hadi mwaka huu kutokana na janga la Corona. Wakati huo huo, Rais mpya wa Iran, Sayyid Ibrahim Rasi ameipongeza timu hiyo ya Iran kwa kuvuna medali zenye kung'aa kwenye mashindano hayo, huku akiwatakia wanamichezo wa Jamhuri ya Kiislamu kheri na fanaka wanapoendelea kuliwakilisha taifa hili katika mashindano ya ndani nan je ya nchi. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilianza kwa dhahabu na kumalizia kwa medali hiyo hiyo, ndivyo unavyoweza kusema kwa ufupi kuhusu timu ya wanamichezo wa Iran walioshiriki Michezo ya Olimpiki ya Tokyo 2020 iliyofungua pazia lake Ijumaa ya Julai 23 nchini Japan. Katika siku za mwanzo za mashindano hayo, mlengaji shabaha stadi wa Iran kutwaa medali ya dhahabu katika mchezo wa kupiga shabaha kwa bastola umbali wa mita 10 kwa upande wa wanaume. Javad Foroughi mbali na kutwaa dhahabu, lakini ameweka rekodi mpya ya Olimpiki baada ya kuzoa pointi 244.8, alama 6.9 mbele ya Msabia Damir Mikec aliyeibuka wa pili na kuzawadiwa medali ya fedha. Mbali na Foroughi, wanamichezo wengine wa Jamhuri ya Kiislamu waliotunukiwa medali ya dhahabu ni Mohammad Reza Geraei, aliyeibuka kidedea katika mchezo wa mieleka mtindowa Greco-Roman na Sajjad Ganjzadeh aliyeng'ara katika mchezo wa karate. Ali Davoudi na Hassan Yazdani walijishindia medali ya fedha kila mmoja katika michezo ya unyanyuaji uzani na mieleka kategoria ya Freestyle (kujiachia) kwa usanjari huo. Wanamieleka Mohammad Hadi Saravi wa safu ya Greco-Roman na Amirhossein Zare wa mtindo wa freestyle waliiongeza idadi ya medali ilizoshinda Iran kwa kutwaa medali ya shaba kila mmoja. Kwa matokeo hayo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imemaliza katika nafasi ya 27 ya mashindano hayo ya dunia ambayo mwaka huu yamefanyika bila ya uwepo wa mashabiki viwanjani kutoka na msambao wa virusi vya Corona. Wanariadha 66 wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni miongoni mwa anamichezo kutoka nchi 200 duniani walioshiriki mashindano hayo. Iran ilimaliza katika nafasi ya 25 katika Michezo ya Olimpiki ya Rio de Janeiro mwaka 2016, baada ya kuzoa medali 3 za dhahabu, moja ya fedha na 4 za shaba.
Dondoo za Olimpiki
Mwanariadha wa Kenya, Eliud Kipchoge Jumapili hii ameibuka mshindi wa mbio za marathon kwa wanaume katika michuano ya Olimpiki huko Japan. Kipchoge amekuwa mwanariadha wa kwanza wa Kenya tangu mwaka 1980 kuuchukua ubingwa wa marathon kwenye olimpiki. Ametumia masaa 2, dakika 8 na sekunde 38 kumaliza mbio hizo na kuwa mkimbiaji wa tatu pekee kuwahi kushinda olimpiki mara mbili. Kipchoge alifuatiwa na Abdi Nageeye wa Uholanzi aliyekuwa nyuma kwa sekunde 20. Mshindi wa tatu ni Bashir Abdi wa Ubelgiji aliyemshinda Lawrence Cherono wa Kenya. Tanzania imewakilishwa na Alphonce Simbu aliyeshika nafasi ya 7 kwa kutumia masaa mawili, dakika 11 na sekunde 25. Mbali na Kipchoge, wanariadha wengine wa Kenya waliotwaa medali za dhahabu ni Emmanuel Korir (800m), Faith Chepng’etich Kipyegon (1,500m) na bingwa wa marathon Peres Jepchirchir; huku medali za fedha zikitiwa kibindoni na Hellen Obiri (5,000m), Ferguson Rotich (800m), Timothy Cheruiyot (1,500m) na Brigid Kosgei. Wanariadha wa Kenya walioshinda medali za shaba ni pamoja na Hyvin Kiyeng na Benjamin Kigen, katika mbio za mita 3,000 kuruva viunzi na maji. Kenya ndiyo nchi ya Afrika iliyofanya vizuri zaidi katika mashindano hayo, lakini kimataifa imemaliza katika nafasi ya 19 kiujumla.
Kwengineko, timu ya taifa ya soka ya Brazil imefanikiwa kutwaa Medali ya Dhahabu kwa mara ya pili mfululizo kwenye Michezo ya Olimpiki upande wa soka baada ya ushindi wa 2-1 dhidi ya Hispania ndani ya dakika 120 Uwanja wa Nissan Jijini Yokohama. Dakika 90 zilimalizika timu hizo zikiwa zimefungana 1-1 Matheus Cunha akiitanguliza Brazil dakika ya 45 na ushei akimalizia kazi nzuri ya Dani Alves, kabla ya Mikel Oyarzabal kuisawazishia Hispania dakika ya 61 kwa usaidizi wa Carlos Soler – na Malcom akafunga la ushindi dakika ya 108 kwa pasi ya Antony.
Wakati Brazil ikibeba Medali ya Dhahabu, Hispania wamechukua Fedha na Mexico iliyomaliza nafasi ya tatu baada ya kuwafunga wenyeji, Japan 3-1 jana wameondoka na Shaba. Rais wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki amesema mashindano ya Tokyo yamekwenda vizuri, licha ya changamoto za hapa na pale zilizosababishwa na janga la Corona. Thomas Back amesema kinachosuburiwa sasa ni Michezo ya Olimpiki ya Walemavu (Paralimpiki) itakayong'oa nanga Agosti 24 na kufunga shughuli zake Septemba 5. Marekani imemaliza katika nafasi ya kwanza kwenye mashindano hayo kwa kuzoa jumla ya medali 113 zikiwemo 39 za dhahabu, ikifuatiwa na China medali 88 zikiwemo dhahabu 38, huku mwenyeji Japan ikifunga orodha ya tatu bora kwa kutia kibindoni medali 58 zikiwemo dhahabu 27. Gavana wa jiji la Tokyo, Yuriko Koike amemkabidhi bendera ya Olimpiki kwa Meya wa jiji la Paris Anne Hidalgo, huku Ufaransa ijiandaa kuwa mwenye wa Michezo ya Olimpiki mwaka 2024.
Kombe la Kagame
Klabu Yanga ya Tanzania imebanduliwa kwenye mashindano ya Kombe la Kagame baada ya kuchabangwa mabao 3-1 na Express ya Uganda. Katika mchezo huo uliopigwa wikendi, Young Africans licha ya kuupigia nyumbani katika Uwanja wa Mkapa, walifanya uzembe na kutandikwa mabao 3-1 na vijana wa Uganda. Kipa wa Yanga Ramadhan Kabwili ambaye katika mechi ya kwanza alipigwa kadi nyekundu walipovaana na Malawi, aliandamwa na mkosi kwenye mechi hiyo ya Waganda na akthari ya mashabiki wanambebesha mzigo wa kushindwa huko. Kipindi cha pili Yanga ilikosa mipango kabisa ya kusawazisha mabao 2-0 waliofungwa kipindi cha kwanza, badala yake wakaongezwa bao lingine. Bao la tatu la Express lilifungwa na Erick Kenzo, liliwaongezea nguvu ya kuishambulia zaidi ya Yanga na kuwafanya mabeki. Tanzania sasa imebaki na wawakilishi wawili katika mashindano hayo ambao ni Azam FC na KMKM ya Zanzibar. Yanga iliyokuwa kundi A pamoja na timu za Nyasa Big Bullet ya Malawi, Express (Uganda) na Atlabara (Sudan Kusini) imetolewa katika hatua ya makundi baada ya kumaliza nafasi ya tatu sambamba na Atlabara iliyokuwa ya nne huku Express na Nyasa zikitinga fainali. Licha ya kutolewa kwa Yanga ambao ni mabingwa mara tano wa michuano hiyo, Azam na KMKM zimetinga nusu fainali ambapo Azam ilimaliza juu ya msimamo wa kundi B ikifuatiwa na KMKM wakati Le Messager (Burundi) na KCCA ya (Uganda) zikitolewa. Mechi za nusu fainali zimepangwa kupigwa Jumanne hii ya Agosti 10, ambapo Express itacheza na KMKM na mechi nyingine itakuwa kati ya Azam na Nyasa Big Buletts. Timu zitakazoshinda mechi hizo mbili zitaingia fainali, na zitakazoshindwa zitacheza mechi ya kugombea nafasi ya tatu.
Dondoo za Hapa na Pale
Wapiga kura 80 wamempitisha Wallace Karia kuongoza kwa mara nyingine Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwenye uchaguzi mkuu unaoendelea jijini Tanga. Karia ameidhinishwa na wapiga kura baada ya kukosa mpinzani. Wakati akiwahoji wapiga kura, Mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi Kiomoni Kibamba aliwauliza wapigakura wanaoafiki Karia aendelee kuongoza Shirikisho hilo kwa miaka minne ijayo waseme ndio. Wapiga kura walisema ndio huku wakipiga makofi na mwenyekiti kuwambia wana haki ya kusimama kumshangilia Rais huyo wa TFF na wajumbe kusimama. Mwenyekiti alisema kwa kuwa uchaguzi ni wa demokrasia, wapiga kura wasioafiki Karia kuidhinishwa wasimame, hakuna aliyesimama huku vicheko vikisikika. Klabu ya Barcelona imetangaza kuwa staa wao raia wa Argentina Lionel Messi hatoendelea tena kuitumikia FC Barcelona licha ya club na mchezaji kufikia makubaliano ya kubaki. Barcelona wametangaza kuwa wanalazimika kumuachia Messi aondoke kwa sababu sheria za matumizi ya kifedha kwa vilabu vya LaLiga ndio imeleta kikwazo. Messi (34) ameitumikia FC Barcelona karibia kipindi chote cha maisha yake, Messi alianza kuichezea timu za vijana za Barcelona toka 2003 alipojiunga nayo akitokea Newell’s Old Boys ya kwao Argentina na mwaka 2004 ndio akaanza kucheza timu ya wakubwa ya Barcelona. Siku ya Jumapili, Messi alibubujikwa na machozi alipokuwa katika mkutano na wanahabari Uwanjani Nou Camp kwa ajili ya kuwaaga rasmi viongozi, wachezaji wenzake pamoja na mashabiki.
Huku hayo yakiarifiwa, timu ya taifa ya wanaume ya tenisi ya Kenya ya Kombe la Davis imewasili nchini Misri tayari kwa mashindano ya Afrika ya Kundi la tatu yatakayoandaliwa Agosti 11-14 jijini Cairo. Wachezaji Ismael Changawa, Kevin Cheruiyot, Albert Njogu, Ibrahim Kibet na Derrick Ominde pamoja na Rais wa Shirikisho la Tenisi Kenya James Kenani (Kiongozi wa Msafara), Rose Wanjala (meneja wa timu) na Philomena Minoo (mnyooshaji misuli na daktari) walisafiri mapema Jumapili Agosti 8 kwenda Misri. Mataifa saba yatashiriki mashindano hayo ya kuamua timu mbili zitakazoingia mchujo wa dunia wa kuingia Kundi la Pili la Dunia. Droo ya Afrika itafanywa Agosti 10 jijini Cairo ambapo Kenya itafahamu wapinzani wake wa mechi za makundi kutoka orodha Algeria, Benin, Misri, Ghana, Msumbiji na Rwanda. Madagascar ilijiondoa. Timu hizi zitagawanywa katika makundi mawili. Kundi moja litakuwa na mataifa manne la lingine matatu. Timu zitakazokamilisha makundi yao katika nafasi mbili za kwanza zitaingia nusu-fainali. Zile zitakazomaliza makundi yao katika nafasi ya tatu zitapigania kusalia Kundi la Tatu ambapo timu itakayopoteza itaungana na mvuta-mkia kutoka kundi la timu nne kushushwa daraja hadi Afrika Kundi la Nne.
Na klabu Leicester City waliendeleza ubabe wao katika soka ya Uingereza kwa kutwaa taji la Ngao ya Jamii (Community Shield) baada ya kuisasambua Manchester City bao1-0 katika Uwanja wa Wembley. Bao la pekee na la ushindi katika mchuano huo uliokutanisha mabingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na wafalme wa Kombe la FA, lilipachikwa wavuni na Kelechi Iheanacho – fowadi wa zamani wa Man-City aliyeangushwa na beki Nathan Ake ndani ya kijisanduku. Gozi hilo liliwapa Man-City ambao ni washikilizi wa taji la EPL, fursa ya kumwajibisha kiungo Jack Grealish kwa mara ya kwanza tangu aagane na Aston Villa kwa Sh15.6 bilioni wiki iliyopita. Tangu watawazwe mabingwa wa EPL mnamo 2016, Leicester wameshuhudia ufufuo mkubwa uliowazolea Kombe la FA msimu uliopita chini ya kocha Brendan Rodgers.
…………………..TAMATI……………..