Jumanne tarehe 17 Agosti 2021
Leo ni Jumanne tarehe 8 Muharram 1443 Hijria sawa na Agosti 17 mwaka 2021.
Tarehe 8 Muharram mwaka 61 Hijria maji yalimalizika kabisa katika mahema ya mjukuu wa Mtume (saw), Imam Hussein (as) na watu wengine wa familia yake katika jangwa lenye joto kali la Karbala. Kharazmi katika kitabu cha Maqtalul Hussein na Khiyabani katika Waqaiul Ayyam wameandika kwamba: Katika siku ya nane ya Mfunguo Nne Muharram mwaka 61 Imam Hussein na masahaba zake walikuwa wakisumbuliwa na kiu kali, kwa msingi huo Imam Hussein alichukua sururu na akapiga hatua kama 19 nyuma ya mahema kisha akaelekea kibla na kuanza kuchimba ardhi. Maji matamu ya kunywa yalianza kutoka na watu wote waliokuwa pamoja naye walikunywa na kujaza vyombo vyao kisha maji yakatoweka na hayakuonekana tena. Habari hiyo ilipofika kwa Ubaidullah bin Ziad alimtumia ujumbe kamanda wa jeshi la Yazid mal'uuni, Umar bin Sa'd akimwambia: Nimepata habari kwamba Hussein anachimba kisima na kupata maji ya kutumia, hivyo baada ya kupata risala hii kuwa macho zaidi ili maji yasiwafikie na zidisha mbinyo na mashaka dhidi ya Hussein na masahaba zake."
Miaka 76 iliyopita katika siku kama ya leo, wananchi wa Indonesia walianzisha mapambano ya kujikomboa kutoka katika makucha ya mkoloni Mholanzi. Mapambano hayo yaliyoongozwa na Ahmad Sukarno yaliendelea kwa miaka minne huko Indonesia. Baada ya kushadidi mapambano hayo ya ukombozi ya wananchi Waislamu wa Indonesia, Umoja wa Mataifa uliiamuru serikali ya Uholanzi kuuasisi utawala kwa jina la " Umoja wa Indonesia na Uholanzi". Jamhuri ya Indonesia ilivunja umoja huo mwaka 1956 na kutangaza uhuru wa nchi hiyo na Sukarno akawa Rais wa kwanza wa taifa hilo.
Siku kama ya leo miaka 61 iliyopita, nchi ya Kiafrika ya Gabon iliyoko magharibi mwa Afrika na katika pwani ya bahari ya Atlantic, ilipata uhuru. Wareno walifika huko Gabon kwa mara ya kwanza mwishoni mwa karne ya 15 Miladia. Hata hivyo nafasi ya kijiografia ya Gabon ilizuia kugunduliwa nchi hiyo hadi karne ya 19. Wafaransa waliwasili Gabon katikati ya karne ya 19 na kuidhinishwa kuitawala nchi hiyo katika mkutano uliofanyika huko Berlin Ujerumani. Hatimaye mwaka 1960 Gabon ilipata uhuru. Kijiografia nchi ya Gabon inapakana na Jamhuri ya Afrika ya Kati, Congo, Cameroon na Guinea Bissau.
Siku kama ya leo miaka 34 iliyopita, Rudolf Hess makamu wa dikteta wa zamani wa Ujerumani Adolf Hitler alijiua akiwa jela nchini Uingereza. Hess ambaye alizaliwa mwaka 1894, alikuwa mmoja wa waasisi wa chama cha Kinazi na miongoni mwa viongozi wakuu wa serikali ya Hitler. Rudolf Hess alihukumiwa kifungo cha maisha jela na mahakama ya jinai za kivita ya Nuremberg nchini Ujerumani baada ya nchi hiyo kushindwa katika Vita vya Pili vya Dunia. Hess alijiua akiwa jela mwaka 1987.
Katika siku kama ya leo miaka 31 iliyopita, kundi la kwanza mateka wa Kiirani waliokuwa wakishikiliwa katika magereza za kutisha za Saddam Hussein liliwasili katika ardhi ya Iran. Kuachiwa huru mateka hao ilikuwa hatua muhimu ya kutekelezwa azimio nambari 598 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kati ya Iran na Iraq. Saddam Hussein ambaye wakati huo alikuwa chini ya mashinikizo kutokana na kuivamia Kuwait alikubali kuwaachia huru mateka hao wa Iran na kurejea katika mipaka inayokubalika kimataifa ya nchi mbili baada ya kukubali mkataba wa mpaka wa Algeria.
Na miaka 16 iliyopita katika siku kama ya leo wanajeshi wa utawala haramu wa Israel waliondoka kikamilifu kutoka katika eneo la Ukanda wa Gaza huko Palestina baada ya miaka 38 ya kukalia mabavu eneo hilo na kutenda jinai. Katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, eneo la Ukanda wa Gaza limegeuka na kuwa nembo ya muqawama na kusimama kidete katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu. Wazayuni wakiwa na lengo la kushinda muqawama wa Kiislamu, wamelishambulia eneo la Gaza mara kadhaa ambapo shambulio la mwisho lilikuwa la mwaka 2014 vilivyodumu kwa muda wa siku 51.