Aug 18, 2021 02:39 UTC
  • Jumatano tarehe 18 Agosti 2021

Leo ni tarehe 9 Muharram 1443 Hijria sawa na Agosti 18 mwaka 2021

Leo kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, ni siku ya Tasua yaani tarehe tisa Mfunguo Nne Muharram. Katika siku kama hii mwaka 61 Hijria wakati majeshi ya Yazid yalikuwa yamejiandaa kikamilifu kumshambulia Imam Hussein AS na masahaba zake katika ardhi ya Karbala, Imam alimtuma ndugu yake aliyesifika kwa ushujaa mkubwa yaani Abul Fadhl Abbas akawaombe maadui hao wampe fursa aupitishe usiku huo, kwa Swala na kunong'ona na Mola wake. Usiku huo Imam Hussein aliwakusanya wafuasi wake na baada ya kumhimidi Mwenyezi Mungu na kumsalia Mtume, aliwaambia: ''Kila anayetaka, aitumie fursa iliyobakia ya giza la usiku kwa ajili ya kuyanusuru maisha yake, kwani hakuna atakayebaki hai hapo kesho tutakapokabiliana na jeshi la Yazid.'' Hata hivyo masahaba na wafuasi waaminifu na waumini wa kweli wa mtukufu huyo walikuwa wameshakata shauri la kujitolea mhanga kwa ajili ya Mwenyezi Mungu hadi tone la mwisho la damu zao. Usiku huo wa kuamkia Ashuraa yaani tarehe 10 Muharram, uwanja wa Karbala ulikuwa medani ya ibada kwa mashujaa ambao licha ya kuwa wachache kwa idadi lakini walisimama imara kama mlima na hawakumuacha Imam na kiongozi wao hata dakika moja.

Siku kama ya leo miaka 1368 iliyopita, vilitokea vita vya Ajnadeen katika eneo la Ajnadeen huko Palestina kati ya Waislamu na Warumi. Katika vita hivyo ambavyo havikuwa na mlingano hasa kwa kuzingatia kuwa, askari wa Kirumi walikuwa wengi mara kadhaa kuliko Waislamu, jeshi la Waislamu liliibuka na ushindi mkubwa kutokana na wapiganaji wake kuwa na irada na imani thabiti. Baada ya Warumi kushindwa vibaya na Waislamu waliamua kurejea nyuma hadi katika mpaka wa Palestina na Syria sambamba na kupoteza maeneo mengi yaliyokuwa chini ya udhibiti wao.

Enel la Ajnadeen karibu na Palestina

Siku kama ya leo miaka 81 iliyopita, alifariki dunia Muhammad Ghaffari aliyekuwa na lakabu ya Kamal al-Mulk mchoraji mahiri wa Kiirani. Alisoma katika skuli ya Darul Funun ya Tehran na kupata mafanikio makubwa katika fani ya uchoraji aliyokuwa akiipenda. Kipindi fulani Muhammad Ghaffar alifanya kazi katika utawala wa Nasser Deen Shah Qajar na kufanikiwa kutoa athari zenye thamani kubwa za uchoraji.

Kamal al-Mulk

Siku kama ya leo miaka 33 iliyopita, baada ya vita vya miaka minane vya kulazimishwa Iran na Iraq, hatimaye Umoja wa Mataifa ulitangaza rasmi kusimamishwa vita hivyo kwa mujibu wa moja ya vipengee vya azimio nambari 598 la Baraza la Usalama la umoja huo. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, madola yanayopenda kujitanua ambayo yaliona maslahi yao yamo hatarini hapa nchini yalianza kutekeleza njama mbali mbali ili kuuangusha mfumo wa Kiislamu wa Iran. Saddam Hussein kibaraka wa madola ya Magharibi na hasa Marekani, wakati huo akiwa Rais wa Iraq alitumiwa na Washington na kuanzisha vita vya miaka minane dhidi ya taifa la Iran akitumia visingizo visivyo na msingi wowote. Mwanzoni mwa vita hivyo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipasisha azimio la kutaka kusimamishwa vita hivyo, ingawa cha kusikitisha katika azimio hilo ni kwamba, baraza hilo halikuashiria hata kidogo uchokozi wa majeshi vamizi ya Iraq dhidi ya taifa la Iran.

Azimio nambari 598

 

Tags