Sep 09, 2021 02:34 UTC
  • Alkhamisi, Septemba 9, 2021

Leo ni tarehe Alkhamisi mwezi pili Mfunguo Tano Safar 1443 Hijria sawa na Septemba 9 mwaka 2021 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 1322 iliyopita, aliuawa shahidi Zaid bin Ali bin Hussein mwana wa Imam Sajjad (as) na mjukuu wa Mtume Muhammad (saw). Zaid bin Ali alisimama kupambana na dhulma za Banii Umayyah na kulinda matunda ya mapambano ya babu yake, Imam Hussein bin Ali (as). Baada ya mapambano ya kishujaa, Zaid bin Ali aliuawa shahidi katika mji wa Kufa nchini Iraq. Harakati ya mapambano ya Zaid ni miongoni mwa matunda ya mapambano ya Imam Hussein (as) katika medani ya Karbala hapo mwaka 61 Hijria kwani baada ya mapambano ya siku ya Ashuraa kulijitokeza harakati nyingi baina ya Waislamu zilizopigana jihadi kwa lengo la kuuondoa madarakani utawala dhalimu wa Banii Umayyah. 

Siku kama yale leo miaka 1173 iliyopita, sawa na tarehe pili Safar mwaka 270 Hijiria, harakati ya mapambano za Wazanji ilifeli baada ya kuuawa kiongozi wa harakati hiyo Sahib al-Zanj. Ali Bin Muhammad maarufu kwa jina la Sahib al-Zanj ambaye alikuwa akijitambua kuwa mmoja wa wajukuu wa Bwana Mtume Muhammad (saw) na Imam Ali bin Abi Twalib (as) alianzisha harakati ya mapambano mwaka 255 Hijiria akisaidiwa na wafuasi wake pamoja na watumwa weusi ambao walikuwa wakiitwa Wazanji, dhidi ya utawala wa kidhalimu wa Bani Abbas huko kusini mwa Iraq. Sahib al-Zanj aliwaahidi watumwa hao weusi kuwaachilia huru kutoka katika minyororo ya utumwa na kuwapa haki zao za kijamii kama watu wengine suala ambalo liliwafanya watu wa jamii hiyo kuvutiwa na harakati yake. Mwaka 257 Sahib al-Zanj aliudhibiti mji muhimu wa Basra, Iraq na taratibu akaanza kutwaa maeneo mengine ya karibu na mji huo. Katika kipindi hicho majeshi ya utawala wa Bani Abbasi yalifanya hujuma kadhaa dhidi ya Wazanji lakini hata hivyo hujuma hizo zilifeli kutokana na msimamo imara wa jamii ya watu hao weusi. Hata hivyo kutokana na matatizo ya ndani Wazanji walidhoofika sana na harakati yao iliyoendelea kwa kipindi cha miaka 15 ikasambaratika baada ya kuuawa kiongozi wao Sahib al-Zanj.

Siku kama ya leo miaka 698 iliyopita, alifariki dunia nchini Misri, Abu Hayyan Gharnatwi, malenga na mtaalamu wa fasihi wa Kiislamu. Alizaliwa mwaka 654 Hijiria huko Andalusia 'Uhispania ya leo' na baadaye alifanya safari katika miji mbalimbali kwa ajili ya kutafuta elimu. Mwaka 679 Abu Hayyan Gharnatwi, alielekea nchini Misri ambako aliishi hadi mwisho wa maisha yake. Akiwa nchini humo alijishughulisha na ufundisha na kuandika vitabu. Gharnatwi alikuwa mtaalamu wa elimu ya Qur'ani, Hadithi na sharia za Kiislamu, lakini alipata umashuhuri mkubwa katika utaalamu fasihi ya lugha ya Kiarabu. Abu Hayyan Gharnatwi ambaye mwishoni mwa uhai wake alikuwa kipofu, ameacha turathi nyingi kama kitabu cha 'Al-Idraaku Lilisaanil-Atraak' 'Tadhkiratun-Nuhaat' 'Tafsirul-Bahril-Muhit' na diwani ya mashairi.

Siku kama hii ya leo miaka 193 iliyopita alizaliwa Leo Tolstoy, mwandishi na mwanafasihi raia wa Russia. Awali Tolstoy alijiunga na jeshi la Qaukasia na katika kipindi hicho ndipo alipoandika kitabu chake cha kwanza alichokipa jina la "Childhood". Mwandishi huyo wa Russia baadae alijiengua jeshini na kutumia muda wake wote kwa ajili ya kusoma na kuandika. Miongoni mwa vitabu mashuhuri vya mwandishi Leo Tolstoy ni "Vita na Amani", "Waqazaki" na "Hadji Murad." Tolstoy alifariki dunia mwaka 1910.

Leo Tolstoy

Siku kama ya leo miaka 76 iliyopita yaani tarehe 9 Septemba 1945, ulitiwa saini mkataba wa kusalimu amri vikosi vya Japan vilivyokuwa vimeidhibiti na kuikalia kwa mabavu China. Kwa mujibu wa mkataba huo askari milioni moja wa Japan waliweka chini silaha zao kwa amri ya Hirohito mfalme wa wakati huo wa Japan. Kwa utaratibu huo vita vya kihistoria kati ya China na Japan vikafikia tamati.

Miaka 52 iliyopita katika siku sawa na hii ya leo alifariki dunia Jalal Aal Ahmad, mwandishi na mkosoaji wa Kiirani. Aal Ahmad alizaliwa mwaka 1302 Hijria Shamsiya jijini Tehran. Mwaka 1325, Jalal al Ahmad alitunukiwa shahada ya fasihi ya Chuo Kikuu cha Tehran. Aliingia katika uwanja wa siasa wakati wa Vita vya Pili vya Dunia na akaanza kuandika magazeti. Alijishughulisha na kuandika makala na ukosoaji na hadithi fupifupi. Jalal Aal Ahmad alikuwa hodari katika kuandika visa na hekaya fupifupi.

Jalal Aal Ahmad

Miaka 45 iliyopia katika siku kama ya leo, aliaga dunia Mao Zedong kiongozi wa Uchina. Zedong alizaliwa mwaka 1893 na mwaka 1921 aliunda chama cha Kikomonisti cha Uchina baada ya kuungwa mkono na wafuasi wa fikra zake. Mao alikuwa akisisitiza juu ya kuwatetea na kuwalinda wanavijiji na kwa sababu hiyo alipata uungaji mkono mkubwa wa wanavijiji wa Uchina.

Mao Zedong

Siku kama ya leo miaka 1449 iliyopita vilianza vita maarufu kwa jina la Vita vya Miaka Saba kati ya madola mawili yaliyokuwa na nguvu kubwa wakati huo ya Iran na Roma, baada ya mfalme Justinian wa Roma kuanzisha mashambulizi yaliyokuwa na lengo la kulikalia kwa mabavu eneo la magharibi mwa Iran. Baada ya miaka saba ya vita mfalme wa Iran Anushirvan alimshinda mfalme Justinian wa Roma na hivyo mfalme huyo akalazimika kujiuzulu. Baada ya kujiuzulu mfalme Justinian mfalme Tiberius alishika mamlaka ya utawala wa Roma. Vita hivyo vilimalizika mwaka 579 baada ya Waroma kukubali kuilipa Iran gharama inayofikia sarafu za dhahabu elfu 45.

 

Tags