Oct 16, 2021 07:42 UTC

Assalaam alaykum wapenzi wasikilizaji popote pale yanapokufikieni matangazo haya ya Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Kwa uwezo na tawfiki ya Allah  tumekutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu ili tuweze kupekua ukurasa mwingine katika kurasa za historia ya Maulamaa na wanazuoni wa Kishia pamoja na mchango wao katika Uislamu. Kipindi chetu kilichopita kilimaliza kumzungumzia Ahmad bin Muhammad Ardabili mashuhuri zaidi kwa jina la Muqaddas Ardabili au Muhaqqiq Ardabili. Tulisema kuwa, wanazuoni na wasomi wengi wakubwa wa dini wanashuhudia kwamba, Muqaddas Ardabili alikuwa amefikia daraja ya juu mno ya uchaji Mungu, ibada na kuipa mgongo dunia na hakuwa na mithili katika zama zake. Sehemu ya 30 ya kipindi hiki juma hili itamzungumzi Qadhi Nurullah Shushtari, msomi na mwanazuoni mwingine mahiri na mashuhuri wa Kishia aliyekuwa na mchango mkubwa katika Uislamu. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi.

Qadhi Nurullah Shushtari alizaliwa mwaka 956 Hijria katika mji wa Shushtar nchini Iran. Alizaliwa katika familia ya elimu na iliyokuwa mashuhuri mno kwa elimu na kushikamana na imani na mafundisho ya Uislamu. Baba yake alikuwa ni Sayyid Sharif na alikuwa alimu na msomi mtajika mno.

Babu yake na kaka zake pia wote walikuwa wametabahari katika elimu mbalimbali za kiakili na nakili. Aidha watoto watano wa Qadhi Nurullah Shushtari walikuwa wasomi na wanazuoni watajika katika zama zao. Baada ya Qadhi Nurullah kukamilisha masomo ya awali na msingi katika mji wa Shushtar, alifunga safari na kuelekea mjini Mash’had. Akiwa huko alisoma na kuhudhuria darsa za walimu na maustadhi wakubwa na mahiri wa zama hizo kama Mulla Abdul-Wahid Shushtari na Mulla Abdul-Rashid Shushtari.

 

Mwaka 993 Hijria Qadhi Shushtari alihajiri na kuelekea India na kuuchagua mji wa Agra kuwa makazi yake. Katika zama hizo, Akbar Shah ndiye aliyekuwa akitawala huko India. Akbar Shah alizikomboa ardhi zilizokuwa jirani na utawala wake na hivyo kufanikiwa kupanua mamlaka ya utawala wake.

Licha ya kuwa alikuwa na mapenzi na wasomi na wanazuoni, lakini hakuwa na itikadi imara na dini fulani. Ni kutokana na sababu hiyo, ndio maana ulahidi na upagani nchini India ulikuwa ukienea na kuongezeka kwa kasi katika zama zake, huku dini za mbinguni zikikumbwa na hali ya kudhoofika na kuzimika nchini India.

Wakati Qadhi Nurullah Shushtari alipowasili nchini India, kutokana na elimu na maarifa makubwa aliyokuwa nayo alizingatiwa na kuthaminiwa mno na mtawala Akbar Shah ambapo akiwa na umri wa miaka 35 alikateuliwa na kukabidhiwa jukumu na wadhifa wa Ukadhi Mkuu. Hata hivyo kabla ya kukubali jukumuu hilo, Qadhi Nurullah alimuwekea sharti Akbar Shah ya kwamba, atakubali kuchukua jukumu hilo kwa sharti kwamba, atahukumu kwa mtazamo wake ingawa hatatoka katika mduara wa Madhehebu Manne ya Hanafi, Hanbali, Shafii na Maliki. Akbar Shah kwa upande wake alikubali sharti hilo.

Umahiri wa Kadhi Nurullah kuhusu masuala ya kifikihi ya madhehebu mengine ya Kiislamu ulikuwa mkubwa kiasi kwamba, fatuwa zake na hukumu alizokuwa akizitoa zilikuwa zikikubaliwa na Maulamaa wa Ahlu-Sunna na fatuwa hizo kusifiwa. Aidha msomi na mwanazuoni huyo alikuwa akifundisha watu elimu ya fikihi kulingana na madhehebu yao ya Kishia, Kihanafi, Kihanbali, Kishafii na Kimaliki. Ni mashuhuri katika historia ya Maulama na wanazuoni na hata baina ya watu katika zama hizo kwamba, Kadhi Nurullah alikuwa muadilifu na alisimama kukabiliana vilivyo na watoa rushwa na alikuwa akihukumu kwa mujibu wa haki na bila kupindisha sheria. Mwenendo na msimamo wake huu uliwakera na kuwaudhi watu waliokuwa na satwa na nguvu katika jamii. Hata hivyo watu wa kawaida na Maulamaa wa Kishia na Kisuni walikuwa wakifurahishwa na kuridhishhwa mno na utendaji wake.

Baadhi walikuwa wakiamini kwamba, awali Kadhi Nurullah alikuwa akificha itikadi yake ya kimadhehhebu kwa kufanya taqiya, huku kundi jingine la wataalamu wa historia likiamini kwamba, kwa kuzingatia baadhi ya ushahidi na nyaraka za kihistoria kama midahalo, vitabu na matamshi ya Maulamaa mbalimbali wa zama zile, kuwa kwake Mshia na mapenzi yake kwa Ahlul-Baiti ni jambo lililokuwa likijulikana wazi na bayana. Aidha yeye ni mmoja wa wahubiri na waenezaji wakubwa na wa mwanzo wa Ushia nchini India. Yumkini kipindi fulani alijificha imani na itikadi yake ya kimadhehebu, lakini ilipolazimu alijitokeza na kutetea Ushia na kuueneza na hivyo kudhihirisha wazi itikadi yake.

Katika upande wa uandishi na kualifu vitabu, Kadhi Nurullah Shushtari alikuwa mwandishi mahiri na stadi kama ambavyo alikuwa na hima kubwa katika uwanja huo akifahamika pia kama malenga na mshairi hodari.

 

Historia inaonyesha kuwa, Kadhi Nurullah Shushtari alitumia nguvu na kila alichonacho kwa ajili ya kueneza madhehebu ya Ahlul-Baiti (a.s). Miongoni mwa vitabu muhimu vya msomi huyu shahidi ni kile kiitwacho: Ih'qaq al-Ahaq Waizhaq al—Batil. Aidha kitabu cha: Majalisul Muuminina ni moja ya vitabu vyake muhimu pia. Kitabu cha Ih'qaq al-Ahaq Waizhaq al-Batil alikitunga kwa ajili ya kutetea na kujengea hoja Uongozi na Uimamu wa Amirul-Muuminina Ali bin Abi Twalib (a.s) na kubainisha fikra ya kiitikadi ya Kishia.

Katika zama hizo, alimu na mwanazuoni mmoja wa  Kishafii ambaye alikuwa Muirani alikuwa ameandika kitabu kiitwacho: Ibtal Nahaj al-Batil akikosoa itikadi ya Kishia ambapo yaliyoandikwa ndani ya kitabu hicho yaliwaudhi mno Mashia. Hivyo Sayyid Nurullah akawa ameandika kitabu cha Ih'qaq al-Ahaq Waizhaq al-Batil kama majibu ya kitabu cha alimu huyo wa Kisuni, kitabu ambacho kimebakia kuwa kumbukumbu muhimu katika historia. Baadhi wanaamini kuwa, kitabu hicho ndicho kilichopelekea kuuawa shahidi Kadhi Nurullah Shushtari.

Kadhi Shushtari aliendelea na kazi ya kufundisha, kutoa hukumu akiwa kama Kadhi na kueneza mafundisho ya Kiislamu huko nchini India. Baada ya kuaga dunia mtawala Akbar Shah na kisha mwanawe Jahangir kushika hatamu za uongozi, ndipo kuliposhuhudiwa kuongezeka uadui dhidi ya msomi huyo. Maadui walifanya kila wawezalo kumkinaisha mtawala mpya yaani Jahangir Shah ili abadilishe mtazamo wake kuhusiana na Kadhi Shushtari. Baada ya msomi huyo kuandika na kutoa kitabu cha Majalisul Muuminina, maadui zake wakaazimia kumuua. Hatimaye walifanikiwa kumridhisha mtawala baada ya kuandaa tuhuma chungu nzima, hivyo alimu huyo akahumukiwa kuchapwa mijeledi. Hata hivyo Kadhi Nurullah ambaye wakati huo alikuwa na umri wa zaidi ya miaka 70, hakuweza kuvumilia mijeledi hiyo, hivyo akaaga dunia wakati wa kutekelezwa adhabu hiyo dhidi yake. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana anatambulika kama Shahidi wa Tatu.

Mahala alipozikwa Kadhi Nurullah Shushtari katika mjini Agra India

 

Mwili uliokuwa umetapakaa damu wa Kadhi Nurullah Shushtari ukazikwa  katika eneo la Akbarabad huko India. Hii leo, kaburi lake linatembelewa na wapenzi na maashiki wa Ahlul-Baiti (a.s).

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu kwa leo umefikia tamati, tukutane wiki ijayo katika sehemu nyingine ya mfululizo huu. Basi hadi tutakapokutana tena juma lijalo ninakuageni nikikutakieni usikilizaji mzuri wa vipindi vyetu vingine.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh

Tags