Jumanne, Mei 24, 2016
Leo ni Jumanne 17 Shaaban mwaka 1437 Hijria mwafaka na tarehe 24 Mei mwaka 2016 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 16 iliyopita, yaani mwaka 2000, vikosi vya utawala dhalimu wa Israel vililazimika kuondoka kwa madhila katika eneo la kusini mwa Lebanon baada ya kulikalia kwa mabavu eneo hilo kwa muda wa miaka 22. Majeshi hayo yaliondoka baada ya kushindwa kukabiliana na mapambano ya wananchi wa kusini mwa Lebanon. Mwaka 1982, majeshi ya utawala wa Kizayuni wa Israel yalishambulia Lebanon na kusonga mbele hadi katika mji mkuu wa nchi hiyo Beirut. Hata hivyo kutokana na wananchi hao kuathirika na mafunzo ya kutokubali dhulma hasa baada ya ushindi wa mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, nchini Lebanon kulianzishwa harakati za mapambano ya Kiislamu dhidi ya majeshi vamizi ya utawala haramu wa Israel. Harakati ya Hizbullah ilikuwa na nafasi muhimu na ya kuzingatiwa mno katika kukombolewa eneo la kusini mwa Lebanon toka katika makucha ya utawala dhalimu wa Israel.
***
Miaka 23 iliyopita katika siku kama ya leo, nchi ya Eritrea iliyoko kaskazini mashariki mwa bara la Afrika ilipata uhuru kutoka kwa Ethiopia. Mwaka 1936 Italia iliikalia kwa mabavu Eritrea iliyokuwa ikihesabiwa katika zama hizo kuwa sehemu ya ardhi ya Ethiopia. Mwaka 1953, Italia iliirejeshea Ethiopia ardhi hiyo. Hata hivyo wananchi wengi wa nchi hiyo waliokuwa wakitaka uhuru walianzisha harakati za ukombozi dhidi ya serikali ya Ethiopia. Mwaka 1991, Harakati ya Ukombozi wa Eritrea ikisaidiana na wanamapinduzi wa Ethiopia walihitimisha utawala wa kidikteta wa Mengistu Haile Mariam, na wakakubaliana kuanishwa mustakbali wa Eritrea mwaka 1993 kupitia kura ya maoni. Washiriki wengi wa kura hiyo ya maoni walipiga kura ya kutaka kujitawala Eritrea.
***
Na katika siku kama ya leo miaka 194 iliyopita, nchi ya Ecuador ilipata uhuru wake kutoka kwa mkoloni Muhispania. Ecuador ni moja ya nchi za Amerika ya Kusini ambayo kupitia uongozi wa Simón Bolívar mwanamapinduzi maarufu wa Venezuela, ilifanikiwa kuwa huru na kujiunga na umoja wa Colombia Kubwa. Hata hivyo umoja huo ulisambaratika haraka na kufanya nchi wanachama wa umoja huo ikiwemo Ecuador kuasisi mfumo wa jamhuri.