Alkhamisi tarehe 25 Novemba 2021
Leo ni Alkhamisi tarehe 19 Rabiuthani 1443 Hijria sawa na Novemba 25 mwaka 2021.
Siku kama ya leo miaka 141 iliyopita sawa na Novemba 25 mwaka 1880, kijidudu maradhi kinachosababisha maradhi ya Malaria kiligunduliwa na Charles Luis Alphonse Laveran, tabibu mashuhuri wa Kifaransa. Ugunduzi huo wa kijidudu maradhi cha malaria ulitayarisha uwanja mzuri wa kukabiliana na kuangamiza maradhi hayo. Mnamo mwaka 1907 Dakta Alphonse Laveran alitunukiwa Tuzo ya Nobeli kutokana na utafiti wake katika masuala ya tiba.
Miaka 71 iliyopita na katika siku kama ya leo yaani tarehe 4 Azar mwaka 1329 Hijiria Shamsia, Tume ya Mafuta ya Bunge la Taifa la Iran, ilipinga mkataba ziada wa mafuta kati ya Iran na Uingereza. Mkataba huo ulikuwa na lengo la kuimarisha nafasi ya Uingereza na kuzidisha uwezo wa nchi hiyo kuchimba mafuta huko kusini mwa Iran. Vilevile mkataba huo uliotayarishwa katika kilele cha ushindani wa Marekani na Uingereza wa kupora utajiri wa mafuta wa Iran, ulitambuliwa kuwa ni tishio kwa maslahi ya taifa.

Siku kama ya leo miaka 56 iliyopita alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 81 Muhammad Hadi Farzaneh, maarufu kwa jina la Hakim Farzaneh, mtaalamu mkubwa wa elimu ya theolojia na falsafa. Hakim Farzaneh alizaliwa mwaka 1302 Hijiria katika moja ya maeneo ya mji wa Isfahan. Alisoma elimu ya msingi eneo alikozaliwa na kisha kuelekea mjini Isfahan kwa ajili ya kuendelea na masomo yake ambapo alipata kusomea elimu mbalimbali muhimu hususan theolojia na falsafa. Aliweza kuinukia kielimu na kuwa msomi mkubwa kiasi kwamba mwishoni mwa umri wake alikuwa miongoni mwa wataalamu wa taaluma hizo. Baadaye alirejea katika mji alikozaliwa na kujishughulisha na kazi ya ufundishaji hadi alipofariki dunia.
Siku kama ya leo miaka 56 iliyopita dikteta wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo au Zaire ya zamani, Jenerali Mobutu Sese Seko alitwaa madaraka ya nchi kupitia mapinduzi ya uwagaji damu. Mobutu alizaliwa mwaka 1930 nchini Congo na mwaka 1950 alijiunga na harakati ya ukombozi ya Patrice Lumumba. Baada ya uhuru wa Congo, Jenerali Mobutu alishika uongozi wa jeshi la nchi hiyo na mwaka 1960 alikuwa waziri mkuu akiwa na umri wa miaka 30. Tarehe 25 Novemba mwaka 1965 Mobutu alipindua serikali na kushika hatamu za nchi hiyo aliyeitawala kidikteta. Tarehe 16 Mei 1997 Mobutu alilazimika kukimbia nchi hiyo na kwenda Morocco ambako alifia na kuacha nyuma faili jesi la ukatili na mauaji.
Siku kama ya leo miaka 55 iliyopita Ustadh Jabbar Baghcheban alifariki dunia baada ya miaka mingi ya kutoa huduma kubwa kwa viziwi hapa nchini. Ustadh Baghcheban alizaliwa mwaka 1261 Hijria Shamsia na mwaka 1303 aliasisi shule ya kwanza ya watoto katika mji wa Tabriz magharibi mwa Iran. Shule hiyo ilianza kutoa mafunzo kwa watoto watatu viziwi. Ustadh Jabbar Baghcheban alivumbua mbinu mpya na ya kisasa ya kutoa mafunzo ya kusoma na kuandika kwa watoto viziwi ambayo ingali inatumika hadi hii leo hapa nchini.
Miaka 46 iliyopita katika siku kama ya leo, nchi ya Suriname ambayo kijiografia ipo katika Amerika ya Kusini ilijitangazia rasmi uhuru wake toka kwa Uholanzi. Mwanzoni mwa karne ya 16 nchi hiyo ilikuwa chini ya utawala wa Uingereza. Mwaka 1954 Suriname ilijipatia utawala wa ndani na miaka 21 baadaye ikajipatia uhuru kamili. Nchi hiyo inapakana na Brazil na Guyana na iko katika pwani ya Bahari ya Atlantic.
Na siku kama hii ya leo mwaka mmoja uliopita aliaga dunia gwiji wa soka wa Argentina na dunia, Diego Armando Maradona. Maradona anatambuliwa na baadhi ya wataalamu wa mpira wa miguu kuwa mmoja kati ya wanasoka bora zaidi katika historia ya mchezo huo duniani. Baadhi yao pia wanamtaja Diego Armando Maradona kuwa ndiye mwanasoka bora wa vipindi vyote. Maradona alizaliwa Oktoba mwaka 1960 na aling'aa sana katika mashindano ya Kombe la Dunia mwaka 1986 baada ya kuiwezesha timu ya taifa ya Argentina kutwaa kombe hilo. Alisifika kuwa na kipaji kikubwa katika kusakata gozi, hodari katika kukontroli mpira na kupiga chenga na mtazamo makini anapokuwa uwanjani. Diego Armando Maradona aliaga dunia siku kama hii ya leo tarehe 25 Novemba mwaka jana kutokana na matatizo ya moyo.