Dec 10, 2021 04:41 UTC
  • Ijumaa tarehe 10 Disemba 2021

Leo ni Ijumaa tarehe 5 Jamadil Awwal 1443 Hijria sawa na Disemba 10 mwaka 2021.

Siku kama ya leo miaka 1438 iliyopita alizaliwa Bibi Zainab (s.a) binti mtukufu wa Imam Ali bin Abi Twalib na Bibi Fatimatu Zahraa (as). Bibi Zainab alikuwa mashuhuri miongoni mwa watu kutokana na maarifa na elimu kubwa aliyokuwa nayo. Katika tukio la Karbala, Bibi Zainab (s.a) alisimama kidete na kukabiliana na dhulma za watawala dhalimu na ujahili watu wa zama hizo ili kutimiza malengo matukufu ya kaka yake, Imam Hussein (a.s). Bibi Zainab alipelekwa Sham pamoja na mateka wengine wa Nyumba Tukufu ya Mtume (saw) baada ya mapambano ya Imam Hussein (a.s) huko Karbala. Hotuba za Bibi Zainab mbele ya majlisi ya Ibn Ziyad mtawala wa Kufa na katika ikulu ya Yazid bin Muawiya huko Sham zilikuwa na taathira kubwa katika kufichua dhulma na ukandamizaji wa Bani Umayya na kuonesha jinsi Watu wa Nyumba Tukufu ya Mtume walivyodhulumiwa.

Siku kama ya leo, miaka 1435 iliyopita kulijiri vita vya Mu'utah, baina ya jeshi la Waislamu na jeshi la Roma na waitifaki wake. Vita hivyo vilitokea baada ya mjumbe aliyekuwa ametumwa na Mtume (saw) huko Sham kwa ajili ya kulingania dini ya Kiislamu, kuuawa shahidi na askari wa kulinda mpaka wa eneo hilo. Baadhi ya wanahistoria wanasema kuwa, miongoni mwa sababu zilizomfanya Mtume (saw) kutuma jeshi la wapiganaji 3,000 kukabiliana na utawala wa Roma katika eneo hilo ni kuuawa shahidi walimu 14 wa Qur'ani Tukufu waliokuwa wametumwa na Mtukufu Mtume katika maeneo ya mpakani ya Sham. Katika vita hivyo Mtume alimteua Jaafar bin Abi Twalib, mtoto wa ami yake, kwa ajili ya kuongoza jeshi la Kiislamu, na akawateua Zaid bin Haritha na Abdullah bin Rawaaha kwa ajili ya kukaimu nafasi hiyo. Jeshi la Kiislamu ambalo lilikuwa limechoka kutokana na kwamba ilikuwa mara ya kwanza kwenda safari ndefu kama hiyo, lilipambana na jeshi la Roma na wapiganaji wa kikabila katika eneo la Mu'utah, magharibi mwa Jordan ya leo ambapo liliwapoteza viongozi wote watatu wa jeshi hilo la Kiislamu. Hatimaye Waislamu walimpa jukumu la kuongoza jeshi hilo Khalid Bin Walid ambaye ndiye kwanza alikuwa amesilimu, ambapo naye alitoa amri ya kuwataka Waislamu kurudi nyuma. Hata kama jeshi la Kiislamu halikushinda vita hivyo, lakini liliweza kusoma mbinu za jeshi la adui hatua ambayo ilikuwa utangulizi wa ushindi dhidi ya jeshi hilo la adui katika vita vya baadaye.

Siku kama ya leo miaka 461 iliyopita, alifariki dunia, Muhammad Mustafa Imadi, maarufu kwa jina la 'Abus-Suud', faqihi na mfasiri wa Qur'an Tukufu. Abus-Suud alizaliwa karibu na mji wa Istanbul, magharibi mwa Uturuki na kuanza kujifunza masomo ya dini ya Kiislamu ambapo alipanda daraja na kuanza kufundisha. Mbali na msomi huyo wa Kiislamu kufahamu lugha ya Kituruki, alikuwa hodari pia katika lugha ya Kifarsi na Kiarabu ambapo aliweza hata kusoma mashairi kwa lugha hizo. Miongoni mwa athari za Abus-Suud ni pamoja na 'Tafsir Abis-Suud' 'Dua Nameh' 'Qanun Nameh' na 'Mafruudhaat.'

Siku kama ya leo miaka 191 iliyopita, alizaliwa Bi Emily Dickinson malenga wa Kimarekani. Bi Emily alijiendeleza na masomo yake katika ngazi ya Chuo Kikuu nchini Marekani. Aidha alivutiwa na fasihi ya lugha na kutunga mashairi baada ya kufahamiana na baadhi ya waandishi mashuhuri wa Kimarekani. Malenga huyo wa Kimarekani aliweza kutunga beti karibu elfu mbili za mashairi, ambapo sehemu tatu tu za mashairi hayo zilichapishwa wakati wa uhai wake na zilizosalia zikachapishwa baada ya kuaga kwake dunia.

Emily Dickinson

Miaka 125 iliyopita katika siku kama hii ya leo alifariki dunia mwanakemia maarufu wa Sweden, Alfred Bernhard Nobel. Nobel alizaliwa mwaka 1833 na kuhamia nchini Russia wakati wa ujana wake. Alfred Nobel alifanikiwa kuvumbua dynamite au baruti baada ya kufanya utafiti mkubwa kwa miaka kadhaa katika uwanja wa sayansi ya kemia. Hata hivyo mada hiyo badala ya kutumiwa kwa matumizi ya amani, ilianza kutumiwa kama kifaa cha kivita. Ni kwa sababu hiyo, ndipo Nobel akatoa pendekezo la kutolewa tuzo kila mwaka kwa shakhsia aliyefanya juhudi kubwa katika uwanja wa kuimarisha amani na usalama duniani. Tuzo hiyo ambayo imepewa jina la mwasisi wake yaani Nobel mwenyewe, hutolewa katika nyanja tano za fizikia, kemia, tiba, fasihi na amani ya kimataifa kwa wasomi waliofanya jitihada kubwa za kuleta amani na mafanikio ya kielimu, uvumbuzi, na mambo mengine makubwa duniani. Hata hivyo uteuzi wa washindi wa tuzo ya Nobel hususan ile ya amani duniani umeathiriwa na ushawishi wa baadhi ya madola makubwa na kuiondoa tuzo hiyo katika mkondo wa asili wa mwanzilishi wake.

Alfred Bernhard Nobel

Katika siku kama hii ya leo miaka 73 iliyopita, yaani tarehe 10 mwezi Disemba mwaka 1948, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipasisha Azimio la Kimataifa la Haki za Binadamu na kuidhinisha haki za kimsingi na kijamii za binadamu. Azimio hilo la haki za binadamu lilitayarishwa kwa maelekezo ya Umoja wa Mataifa kupitia jopo la wawakilishi wa nchi kadhaa duniani. Kipengee nambari moja cha azimio hilo kinasisitiza kuwa binadamu wote ni sawa. Licha ya kupasishwa azimio hilo, leo hii vitendo na siasa za madola ya Magharibi hasa Marekani vinakinzana wazi na azimio hilo. Leo hii pia baadhi ya madola hayo ya Magharibi yamekuwa yakilitumia suala la haki za binaadamu kama wenzo wa kuyashinikiza mataifa mengine.

Miaka 37 iliyopita katika siku kama ya leo, Baraza Kuu la Mapinduzi ya Kiutamaduni liliundwa nchini Iran kwa amri ya Imam Ruhullah Khomeini mwasisi na mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Baada ya ushindi wa mapinduzi ya Kiislamu, makundi mbalimbali yalikuwa yakikwamishwa mwenendo wa masomo katika vyuo vikuu na shule mbalimbali hapa nchini. Kuna waalimu na wahadhiri wengi wapotofu ambao walikuwa wakifanya kazi katika vyuo vikuu na skuli tofauti hapa nchini na hakukuwa kumefanyika mabadiliko yoyote ya ratiba, mbinu za ufundishaji, malezi na masomo. Natija ya hilo ikawa ni kufungwa kwa muda vyuo vikuu. Baada ya vyuo vikuu kufungwa, Imam Khomeini alitoa amri ya kuundwa Baraza la Mapinduzi ya Kiutamaduni kwa shabaha ya kuboresha masuala ya utamaduni wa shule na vyuo vikuu.