Jan 05, 2022 02:35 UTC
  • Jumatano tarehe 5 Januari mwaka 2022

Leo ni Jumatano tarehe Pili Jamadithani 1443 Hijria sawa na na Januari 5 mwaka 2022.

Siku kama ya leo miaka 1419 iliyopita vilianza vita vya miaka 24 kati ya falme za Iran na Roma. Vita hivyo viliibuka kufuatia kuuawa Maurice, aliyekuwa mfalme wa Roma na ambaye pia alikuwa muungaji mkono na rafiki wa karibu wa Mfalme Khosrow Parviz wa Iran. Kufuatia mauaji hayo ya Maurice, mtoto wake alikuja Iran na kumuomba msaada Mfalme Khosrow. Mfalme huyo wa Iran na kwa lengo la kulipiza kisasi cha damu ya Maurince, alituma jeshi lililojizatiti kwa silaha kwenda kuishambulia Roma ambapo kwa kipindi kifupi liliweza kuteka miji mingi ya nchi hiyo. Baada ya ushindi huo, mfalme mpya wa Roma alimtuma mjumbe wake kuja Iran kwa ajili ya kufanya mazungumzo ya amani na mfalme wa Iran, hata hivyo Mfalme Khosrow Parviz ambaye alikuwa tayari ameingiwa na kiburi cha kupata ushindi mkubwa katika vita hivyo, alikataa mpango wa amani na hivyo akawa ameendeleza vita hivyo. Vita hivyo ambapo pande mbili zilipata ushindi katika vipindi tofauti, viliendelea kwa muda wa miaka 24.

Tawala za Iran na Warumi

Siku kama ya leo miaka 331 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 5 Januari 1691, ilichapishwa na kusambazwa noti ya kwanza huko Ulaya. Noti hiyo ilichapishwa na Benki ya Stockholm na kutumiwa kama fedha. Kabla ya kuchapishwa noti hiyo nchini Sweden, miamala ya kibiashara ilikuwa ikifanyika kwa kutumia sarafu za dhahabu zenye pembe nne. Moja kati ya noti za awali kabisa kuchapishwa nchini Sweden, inahifadhiwa kwenye makumbusho ya Benki ya Stockholm.

Siku kama ya leo miaka 213 iliyopita, ulitiwa saini mkataba wa Dardanelles (Treaty of the Dardanelles) baina ya utawala wa Othmania na Uingereza. Kwa mujibu wa mkataba huo, Uingereza iliahidi kuondoka katika ardhi zote zilizokuwa chini ya utawala wa Othmania ikiwemo Misri na kuhitimisha ukaliaji mabavu wa ardhi hizo. Mkabala wake, utawala wa Othmania uliahidi kutambua rasmi haki za kibalozi za Uingereza katika ardhi za utawala wa Othmania.

Tarehe 15 Dei miaka 43 iliyopita wanafunzi wa vyuo vikuu nchini Iran waligoma kwenda madarasani na kufunga masomo wakionesha upinzani wao dhidi ya safari ya rais wa wakati huo wa Marekani, Jimmy Carter hapa nchini na uungaji mkono wake kwa utawala wa Shah. Wakati huo Carter alikuwa akidai kuwa ni mtetezi wa haki za binadamu na mpinzani wa suala la kuziuzia silaha tawala za kidikteta. Hata hivyo serikali ya Washington ilichukua uamuzi wa kufunga mikataba ya kuuzia silaha nzito utawala wa kidikteta wa Shah na kupuuza ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu uliokuwa ukifanywa nchini Iran. Jimmy Cater alifikia kiwango cha kumwita Shah kuwa ni kiongozi anayependwa na wananchi na kwamba Iran ni kisiwa cha amani. Hata hivyo muda mfupi baadaye wananchi walianza harakati za kudai uhuru na kujitawala na miezi 13 baada ya safari ya Carter mjini Tehran Shah aliondolewa madarakani na ikaanzishwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Jimmy Carter na Shah

Miaka 37 iliyopita katika siku kama ya leo, inayosadifiana na tarehe 5 Januari 1985, utawala wa Kizayuni wa Israel uliwachukua maelfu ya Mayahudi wa Ethiopia "Mafalasha' kupitia ardhi ya Sudan. Mafalasha hao ambao idadi yao ilikuwa watu 8,000 walipelekwa huko katika ardi inayokaliwa kwa mabavu ya Palestina. Nchi za Kiarabu ziliikasirikia Sudan kwa kushirikiana na Israel katika kuwahamisha Mayahudi wa Kiethiopia na kuwapeleka Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Na siku kama hii leo miaka 7 iliyopita aliaga dunia mkongwe wa soka nchini Ureno Eusebio da Silva Ferreira. Eusebio alifariki dunia kutokana na mshituko wa moyo akiwa na umri wa miaka 71. . Eusebio ambaye ni mzaliwa wa Msumbiji, aliichezea timu ya taifa ya Ureno mechi 64 na kupachika mabao 41, huku akiipachikia mabao klabu yake ya Benfica mabao 585 katika mechi 571 alichoichezea.

Anatambuliwa kuwa mmoja kati ya wafungaji bora zaidi katika historia ya mpira wa miguu duniani. Nyota huyo, alisifa kwa kuwa na tabia na maadili bora wakati wa alipokuwa akisakata kandanda na hata baada ya kustaafu mchezo huo, na kwa sababu hiyo ametambuliwa kuwa gwiji mkubwa wa nyakati zote nchini Ureno.

Inafaa kuashiria hapa kuwa katika michuano ya kombe la dunia iliyofanyika 1966, Eusebio aliibuka mfungaji bora kwenye michuano hiyo kwa kupachika mabao 9 na Ureno kushika nafasi ya tatu. Mwaka 1965, Eusebio alifanikiwa kuchaguliwa kuwa mchezaji bora duniani na kupewa tuzo ya mpira wa dhahabu, na mara mbili alichaguliwa kuwa mfungaji bora wa Ulaya.

Eusebio da Silva Ferreira