Jan 17, 2022 02:38 UTC
  • Jumatatu tarehe 17 Januari 2022

Leo ni Jumatatu tarehe 14 Jamauthani 1443 Hijria sawa na Januari 17 mwaka 2022.

Miaka 938 aliyopita katika siku kama hii ya leo, alifariki dunia msomi na mtaalamu wa fiq'hi wa Kiiran Abu Hamid Muhammad Ghazali Tusi, maarufu kwa jina la Imam Muhammad Ghazali. Baada ya kuaga dunia baba yake, yeye na kaka yake, Ahmad walilelewa na Ahmad bin Radkani. Ghazali alisoma elimu ya fiq'hi kutoka kwa Abu Nasri Ismail na baada ya kufikia umri wa miaka 28 alikuwa mmoja wa wasomi wakubwa wa Kiislamu katika elimu hiyo. Umaarufu wa Imam Muhammad Ghazali ulipelekea kiongozi wa Iraq wakati huo Khoja Nidham al-Mulk kumwalika msomi huyo kwenda mjini Baghdad kwa ajili ya kufundisha. Hatimaye alirejea Iran na kujishughulisha na masuala ya ualimu. Kabla ya kurejea Iran, Imam Muhammad Ghazali alipata kuandika vitabu vya thamani kama "Ihyau Ulumud Din," "Kemia ya Saada" na "Nasaha za Wafalme."

Imam Muhammad Ghazali

Katika siku kama ya leo miaka 162 iliyopita, alizaliwa Anton Chekhov, mwandishi mashuhuri wa Urusi. Chekhov alizaliwa katika familia ya kipato cha chini na kupitia matatizo mbalimbali. Pamoja na hayo Anton Chekhov alifanya bidii kubwa ya masomo hususan katika fani ya udaktari katika Chuo Kikuu cha Moscow na kuhitimu masomo yake chuoni hapo. Akiwa kijana alipendelea sana masuala ya uandishi na kuanza kujishughulisha na kazi za uandishi katika magazeti na wa makala tofauti za wakati huo. Alikuwa mahiri katika tenzi fupifupi na hivyo kutokea kuwa mashuhuri katika uga huo. Miongoni mwa athari za mwandishi huyo ni pamoja na kitabu cha "Jogoo wa Bahari" na vitabu vingine kadhaa. Anton Chekhov alifariki dunia nchini Ujerumani mwaka 1902 Miladia.

Anton Chekhov

Siku inayosadifiana na hii ya leo, miakka 131 iliyyopita alifariki dunia Ayatullah Mirza Habibullahi Rashti mmoja kati ya wanazuoni na maraaji' wakubwa wa Kiislamu. Katika uhai wake alielekea mjini Najaf Iraq kwa ajili ya masomo ya dini na kuhudhuria masomo ya Sheikh Murtadha Ansari. Ayatullah Mirza Habibullahi Rashti taratibu akawa mmoja wa maraaji' wakubwa katika mji mtakatifu wa Najaf. Miongoni mwa athari za msomi huyo ni pamoja na kitabu cha "Badaiul Afkar.

Ayatullah Mirza Habibullahi Rashti

Tarehe 27 Dei miaka 66 iliyopita Navvab Safavi, mwanachuoni na mwanaharakati wa Iran aliuawa shahidi akiwa pamoja na wenzake watatu, baada ya kuhukumiwa adhabu ya kifo kwenye mahakama ya kimaonyesho tu ya kijeshi katika utawala wa Shah hapa nchini. Akiwa kijana, Navvab Safavi alipata taaluma ya masomo ya kidini nchini Iran na kisha akaelekea Najaf nchini Iraq kwa shabaha ya kujipatia elimu zaidi. Alirejea nchini baada ya miaka kadhaa na kuanzisha mapambano dhidi ya utawala tegemezi na kibaraka wa Shah. Hatimaye katika siku kama hii ya leo Safavi alikamatwa na utawala wa Shah na kuuawa shahidi akiwa na wenzake watatu.

Navvab Safavi

Miaka 61 iliyopita katika siku kama hii ya leo aliuawa Patrice Lumumba mhandisi wa uhuru wa Kongo. Lumumba alitoa mchango mkubwa katika juhudi za kukombolewa Kongo wakati wa harakati za ukombozi wa nchi za Kiafrika. Lumumba aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu na Waziri wa Ulinzi baada ya kuundwa Jamhuri ya Kongo mwaka 1960. Patrice Lumumba aliuawa mwaka 1961 na vibaraka wa Marekani na Ubelgiji baada ya kuvumilia mateso na unyama mkubwa. Mwanamapinduzi huyo shujaa aliandika vitabu kadhaa wakati wa uhai wake na mashuhuri zaidi ni kile alichokita "Kongo, Nchi Yangu."

Patrice Lumumba

Tarehe 17 Januari mwaka 1991 vikosi vya majeshi ya nchi kadhaa chini ya uongozi wa Marekani vilizishambulia ngome za wanajeshi wa Iraq huko Kuwait na Iraq ili kukomesha kukaliwa kwa mabavu Kuwait na jeshi la utawala wa Saddam. Mgogoro huo ulianza tarehe Pili mwezi Agosti mwaka 1990 baada ya utawala wa zamani wa Iraq kuikalila kwa mabavu ardhi ya Kuwait. 

Kikosi cha kwanza cha wanajeshi wa Marekani waliowasili Kuwait

Na miaka 13 iliyopita katika siku kama ya leo, Wazayuni maghasibu walilazimika kutangaza usitishaji vita baada ya jeshi la utawala wa Israel kufanya mashambulizi ya kinyama ya siku 22 dhidi ya raia wa Ukanda wa Gaza. Katika mashambulizi hayo, utawala wa Kizayuni ulikusudia kuiangamiza Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas au kwa uchache kuilazimisha harakati hiyo ikubali mazungumzo eti ya mapatano. Hata hivyo uungaji mkono wa Wapalestina kwa harakati ya Hamas na vilevile malalamiko makali ya walimwengu dhidi ya jinai za wanajeshi wa Israel katika Ukanda wa Gaza, yaliulazimisha utawala haramu wa Israel usitishe mashambulio yake.

Ukanda wa Gaza

 

Tags