Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (42)
Ahlan Wasahlani wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu.
Kipindi chetu kilichopita kilikamilisha sehemu tatu zilizozungumzia historia na maisha ya Muhammad Baqir Majlisi mashuhuri kwa jina la Allama Majlisi. Tulisema kuwa, Alllama Majlisi alikuwa mmoja wa Maulamaa wa Kishia waliokuwa na taathira chanya na muhimu mno katika harakati za kisiasa na kijamii katika kipindi cha utawala wa Ukoo wa Safavi nchini Iran. Bihar al-Anwar ndicho kitabu mashuhuri zaidi cha msomi huyu. Kitabu hiki kina zaidi ya hadithi 85,000 zilizonukuliwa kutoka kwa Bwana Mtume (saw) na Ahlul-Baiti wake watoharifu (as) na ilimchukua Allama Majlisi miaka zaidi ya 30 kuandika kitabu hiki. Kipindi chetu cha wiki hii ambacho ni sehemu ya 42 ya mfululizo huu kitamtambulisha alimu, msomi na mwanazuoni mwingine wa Kishia ambaye ni Allama Wahid Bahbahani. Ni matumaini yangu kuwa, mtakuwa nami hadi mwisho wa kipindi. Karibuni.
Allama Muhammad Baqir Wahid Bahbahani ni mmoja ya wajukuu wa Majlisi wa Kwanza. Alizaliwa mwaka 1117 katika mji wa Isfahan Iran. Katika kipindi hicho kidogo kidogo mji wa Isfahan ulianza kupoteza ile hali yake ya kuwa ni kitovu cha elimu. Muhammad Baqir alihajiri pamoja na familia yake na kuelekea katika mji wa Bahbahan Iran. Baadhi wanaamini kuwa, Muhammad Akmal Isfahan baba wa Allama Bahbahani alielekea katika mji huo kwa ajili ya kwenda kukabiliana na kundi la Akhbariyun ambalo lilikuwa limeenea katika mji huo. Akhbariyun ni kundi la mafakihi na wanazuoni wa fikihi wa Kishia ambao mtindo na mbinu yao ya kielimu ya kufikia hukumu za Kisheria na taklifu za Mwenyezi Mungu ni kufuata hadithi na sio mtindo wa ijitihadi na Usul. Aidha wengine wanataja sababu ya kuhajiri kwake kuwa ni mparaganyiko wa kijamii na kisiasa uliotokea katika mji wa Isfahan katika zama hizo. Hii ni kutokana na kuwa, katika zama hizo, mji wa Bahbahan ulikuwa na utulivu wa kiwango fulani kwa ajili ya watu wanaojihusisha na masuala ya kielimu.
Muhammad Baqir alikulia chini ya malezi na uangalizi wa baba yake. Alikuwa na kusoma katika mji huo wa Bahbahan na kuondokea kuwa mmoja wa wanazuoni na Maulamaa mashuhuri. Alibakia katika mji huo kwa muda wa miaka 30 na kufanya hima ya kuzipatia ufumbuzi hitilafu za kiitikadi zilizojitokeza baina ya wakazi wa mji huo.

Allama Bahbahani ambaye alikuwa ametabahari katika akthari ya elimu za Kiislamu aliweza kufanya ubunifu na kuweka jiwe la msingi katika nyuga mbalimbali za kielimu kama Fikihi, Usulul Fikih. Mambo mapya yaliyoletwa na Allama Bahbahani hayaiishi katika elimu ya Usul tu, kwani alikuwa na mchango mkubwa pia katika elimu nyingine za Kiislamu kama teolojia, elmur rijaa na hadithi na aliweza kufikia daraja za juu kabisa za kielimu katika taaluma hizo. Kwa kuzingatia kwamba, masuala ya fikihi na Usul yanatumiwa mno na Maulamaa, masuala mengine ya kielimu ambayo yalikuwa ni ubunifu mkubwa na usio na mithili wa msomi huyu yamesahaulika au hayatambuliwi sana.
Marhumu Wahid ana ubunifu mkubwa na wa kuzingatiwa katika Elmur Rijaal na Dirayah. Katika zama za Allama Wahid Bahbahani, elimu ya Usulul Fikih ambayo ina nafasi ya kimsingi katika Ijtihad ilikumbwa na hali ya mdodoro na kuzorota na wasomi hawakuwa wakiizingatia na kuipa umuhimu elimu hii kama inavyotakiwa. Allama Wahid Bahbahani alijitokeza kwa ajili ya kuitetea na kuilinda elimu hii muhimu na akaweka jiwe na msingi na kuihuisha upya.
Usul Fikih ni elimu ambayo ndani yake zinachambuliwa kanuni na misingi ambayo inatumiwa na Mamujitahidi kwa ajili ya kunyambua hukumu na sheria. Kwa muktadha huo, elimu ya Usulul Fikih ni wenzo ambao fakihi kupitia kwayo anaweza kunyambua na kutoa hukumu kutoka katika nyanzo vikuu na asili yaani Qur'ani, hadithi, akili na Ijmaa (makubaliano ya wanazuoni).
Allama Wahid Bahbahani alianzisha harakati ambayo matunda yake yakawa ni kuzalisha makumi ya mafakihi na wanazuoni wa Usul wa daraja la kwanza katika vyuo mbalimbali vya kidini. Ustadh wa Marhumu Wahid Bahbahani yaani Marhumu Sayyid Sadruddin Radhawi Qumi alikuwa akisema: Katika zama zetu, hakukuweko na msomi hata mmoja wa elimu ya Usul. Lakini katika kipindi kifupi baada yake, kutokana na hima na juhudi za Allama Wahid Bahabahani, kulitokea mageuzi ya kushangaza katika elimu ya Usulul Fikih ambapo wanafunzi wake walifanikiwa mno kulisukuma mbele gurudumu la mjalada na maudhui zinazohusiana na Usul Fikih ya Kishia. Wahid Bahbahani alikuwa mashuhuri kwa harakati zake za mapambano dhidi ya Akhbariyun ambao kama tulivyosema ni kundi la Maulamaa linaloamini kwamba, dhahiri ya hadithi inatosha kabisa kwa ajili ya kufahamu maamrisho na maagizo ya dini. Wao wanaamini kwamba, riwaya na hadithi zote za Kutubul Ar'baa (vitabu vinne vya hadithi vya Mashia) ni sahihi na wanaamini kwamba, kila mtu anaweza mwenyewe kurejea hadithi zilizoko katika vitabu hivyo na kufahamu taklifu za kidini na hivyo hakuna haja ya kumkalidi na kumfuata Marjaa Taqlidi.
Kimsingi ni kuwa, mrengo wa Akhbariyun unaamini kwamba, haijuzu kumkalidi Mujtahidi. Mkabala na mrengo huo kuna mrengo wa Usuliyun ambao unaamini kwamba, ili kuainisha kwa njia sahihi hukumu za dini, ni lazima mtu awe na utaalamu na ubobezi wa kielimu na kuna haja ya kuweko watu ambao kutokana na umahiri na kutabahari kwao kwa vyanzo vya dini na kwa kutumia mbinu makini ya kielimu na kiakili wanyambue hukumu za dini kuhusiana na masuala mbalimbali. Watu wengine ambao hawana ujuzi na ubobezi huu wanapaswa kuwarejea wasomi na wanazuoni hawa yaani kuwakalidi. Suala la asiye na ujuzi kumrejea mwenye ujuzi ni kanuni inayokubalika kiakili na mrengo wa Usuliyun unaamini kwamba, kanuni hii inahusiana pia na suala la kuainisha hukumu ya kidini.
Kinyume na itikadi ya Akhbariyun, mrengo wa Usuliyun unaamini kwamba, siyo kila hadithi iliyonukuliwa na kutufikia ni sahihi, kama ambavyo kutosheka tu na dhahiri ya hadithi kutapelekea kufahamu kimakosa dini. Ili kufahamu usahihi wa hadithi kuna haja ya kuweko mtu mwenye ujuzi na utalaamu katika elimu hiyo ili aweze kuchambua pande zote za hadithi husika, mapokezi yake, wapokezi na kadhalika.
Allama Wahid Bahbahani aliiishi kwa takribani miaka 90 na mwishoni mwa umri wake alikumbwa na udhaifu wa mwili kutokana na umri hivyo akaacha kufundisha na kufanya midahalo na badala yake akatosheka na kufundisha Sherh ya Lum'a. Alimuita mwanafunzi wake mahiri yaani Allama Bahrul Ulum huko Najaf na kumtaka aanzishe darsa na kushughulikia masuala ya Mashia. Allama Wahid Bahbahani aliaga dunia tarehe 29 Mfunguo Mosi Shawwal 205 Hijria huko Karbala Iraq na kuzikwa jirani na Haram ya Imam Hussein (as). Licha kuaga dunia, lakini jina lake lingali linang'ara hadi leo na taa aliyoiwasha msomi huyu ingali hadi leo inamulikia njia ya uongofu wanazuoni na watafuta haki ulimwenguni. Mwenyezi Mungu amrehemu na amfufue pamoja na mawalii wake.
Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh