Apr 28, 2022 06:14 UTC
  • Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (45)

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami tena katika sehemu nyingine ya kipindi cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu, ili kwa tawfiki ya Allah tufungue ukurasa mwingine katika kurasa za historia ya Maulamaa wa Kishia, mchango wao pamoja na athari na vitabu vyao.

 

Kipindi chetu kilichopita kilimzungumzia Bahr al-Ulum, msomi na mwanazuoni mwingine wa Kishia ambapo tulisema kuwa, Allama Bahrul Ulum siyo tu kwamba, alikuwa ameibuka na kuondokea kuwa msomi na mwanazuoni aliyebobea kielimu na usimamiaji mambo kwa njia sahihi, bali kwa hakika alikuwa mfano wa kuigwa wa mtu aliyekamilika kwa mujibu wa maadili ya Kiislamu na mtindo wa maisha ya kidini. Alimu huyu mtajika kutokana na kuwa na daraja ya juu kimaanawi, taqwa, uchajimungu na kumtambua Mwenyezi Mungu aliondokea kuheshimiwa mno na Maulamaa wa Kishia. Sehemu ya 45 ya mfululizo huu juma hili, itamzungumzia Sheikh Jafar Kashif al-Ghitaa. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi. Karibuni.

 

Jafar bin Khidhr bin Jahya Janaji Hilli Najafi, mashuhuri kwa jina la Sheikh Jafar Najafi mwenye lakabu ya Kashif al-Ghitaa, Sheikh Jafar al-Kabir na Sheikh al-Mashayikh mmoja wa Maulamaa na Mamarjaa wakubwa na mahiri wa Kishia katika karne ya 13 Hijria. Mwanazuoni huyu ndiye mwanafunzi mtajika zaidi wa Allama Wahid Bahbahani na Allama Bahr al-Ulum. Sheikh Jafar Kashif al-Ghitaa baada ya kuaga dunia Allama Bahr al-Ulum, alichukua jukumu la uongozi na Umarjaa wa Shia.

Sheikh Jafar Kashif al-Ghitaa

 

Sheikh Jafar Kashif al-Ghitaa alizaliwa mwaka 1154 Hijria katika mji mtakatifu wa Najaf. Nasaba yake inarejea na kufika kwa Malik al-Ashtar swahaba na kamanda shujaa na mwenye nguvu wa jeshi la Imam Ali bin Abi Twalib (as). Baba yake ni Khidhr na alikuwa akihesabiwa kuwa mmoja wa wanazuoni na Maulamaa wachaji Mungu na walioipa mgongo dunia katika zama zake.

Khidhr bin Yahya kwao ilikuwa ni mji wa Hillah huko Iraq na alielekea Najaf kwa ajili ya masomo na kubakia katika mji huo. Sheikh Jafar alizaliwa katika mji wa Najaf na kuanza kusoma masomo ya dini katika Chuo Kikuu cha Karbala. Baadaye msomi na mwanazuoni huyo alielekea katika mji wa Najaf na kuchota elimu katika bahari ya elimu ya wanazuoni na walimu waliokuwa mahiri na stadi katika zama hizo.

Kidogo kidogo elimu yake ilianza kuchanua, kukua na kuenea kiasi cha kupelekea  Maulamaa wa madhehebu mbalimbali na wasomi wakubwa katika dini kumtambua kuwa ni Allama na msomi wa Kishia asiye na mithili katika zama hizo.

Kashif al-Ghitaa alifanya safari katika maeneo mbalimbali ya nchi za Kiislamu ikiwemo Hijaz, Iran na Palestina. Waislamu wa madhehebu ya Shia katika maeneo mbalimbali ya nchi za Kiislamu wakafahamu na kutambua bahari ya elimu ya mwanazuoni huyu pamoja na shakhsia ya uchajimungu na yenye taathira ya alimu na msomi huyu mahiri. Ni kwa msingi huo, kivitendo Kashif al-Ghitaa akawa ni Marjaa Taqlidi wa Mashia ulimwenguni.

Sheikh Jafar Kashif al-Ghitaa akiwa Palestina

 

Kiwango cha satwa na ushawishi pamoja na kukubalika Kashif al-Ghitaa baina ya watu ni mambo ambayo yaliwafanya watawala wa nchi za Kiislamu nao waithamini nafasi na daraja yake maalumu aliyokuwa nayo.

Sheikh Jafar Kashif al-Ghitaa ameandika na kualifu vitabu vingi katika nyuga mbalimbali za kidini kama Fikihi na Usul. Kitabu muhimu zaidi cha mwanazuoni huyu ni Kashful Ghitaa an Mub’hamat al-Shariati al-Gharra. Kutokana na kuandika kitabu hiki aliondokea kuwa mashuhuri kwa jina la Kashif al-Ghitaa. Kashful Ghitaa ni kitabu bora zaidi miongoni mwa vitabu vya Kishia vilivyoandikwa katika uga wa teolojia, fikihi na Usul. Kitabu hiki kinachambua na kuthibitisha kwamba, Ushia ni madhehebu ya haki.

Umuhimu wa kitabu hiki ni mkubwa mno kwa Maulamaa na mafakihi wa Kishia kiasi kwamba, inanukuliwa kuwa, Sheikh Murtadha Ansari alimu na mwanafakihi mtajika, mashuhuri na asiye na mithili wa karne ya 13 Hijria alisema kuwa: Endapo mtu atafahamu kanuni na misingi ya kitabu hiki, kwangu mimi mtu huyo ni Mujtahidi.

Miongoni mwa harakati muhimu za Sheikh Jafar Kashif al-Ghitaa ilikuwa ni kuimarisha na kupanua mbinu ya mrengo wa Usuliyuun na kupambana na harakati za Akhbariyuun katika fikihi. Tulibainisha katika vipindi vyetu vilivyotangulia kwamba, Akhbariyuun ni kundi la Maulamaa wa Kishia linaloamini kwamba, dhahiri ya hadithi inatosha kabisa kwa ajili ya kufahamu maamrisho na maagizo ya dini. Kundi hilo linaamini kwamba, riwaya na hadithi zote za Kutubul Ar'baa (vitabu vinne vya hadithi vya Mashia) ni sahihi na wanaamini kwamba, kila mtu anaweza mwenyewe kurejea hadithi zilizoko katika vitabu hivyo na kufahamu taklifu za kidini na hivyo hakuna haja ya kumkalidi na kumfuata Marjaa Taqlidi. Kimsingi ni kuwa, mrengo wa Akhbariyun unaamini kwamba, haijuzu kumkalidi Mujtahidi.

Sheikh Jafar Kashif al-Ghitaa

 

Mkabala na kundi hilo kuna mrengo wa Usuliyun ambao unaamini kwamba, ili kuainisha kwa njia sahihi hukumu za dini, ni lazima mtu awe na utaalamu na ubobezi wa kielimu na kuna haja ya kuweko watu ambao kutokana na umahiri na kutabahari kwao kwa vyanzo vya dini na kwa kutumia mbinu makini za kielimu na kiakili wanyambue hukumu za dini kuhusiana na masuala mbalimbali. Watu wengine ambao hawana ujuzi na ubobezi huu wanapaswa kuwarejea wasomi na wanazuoni hawa yaani kuwakalidi.

 

Sheikh Jafar Kashif al-Ghitaa binafsi alileleka katika misingi na maktaba ya Usuliyuun alipokuwa akisoma kwa Allama Wahid Bahbahani ambaye alikuwa na nafasi na mchango mkubwa na athirifu katika uwanja huu. Mbali na kitabu cha Kashful Ghitaa an Mub’hamat al-Shariati al-Gharra ambacho kilimpatia umashuhuri na kuondokea kufahamika kwa jina la Kashif al-Ghitaa, mwanazuoni huyu ameandika vitabu vingine katika nyanja mbalimbali.

Mbali na uga wa uandishi wa vitabu Sheikh Jafar Kashif al-Ghitaa alikuwa akijishughulisha pia na harakati za kijamii na kisiasa na kuna athari zake nyingi katika uwanja huo.

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu kwa leo umefikia tamati. Tukutane tena wiki ijayo katika sehemu nyingine ya mfululizo huu ambapo tutaendelea kumzungumzia msomi na mwanazuoni huyu yaani Kashif al-Ghitaa. Basi hadi tutakapokutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki juma lijalo ninakuageni nikikutakieni kila la kheri.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.