Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (46)
Assalaam alaykum wapenzi wasikilizaji popote pale yanapokufikieni matangazo haya ya Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu ili tuweze kufungua ukurasa mwingine katika kurasa za historia ya Maulamaa na wanazuoni wa Kishia pamoja na mchango wao katika Uislamu. Kipindi chetu kilichopita kilitupia jicho kwa mukhtasari historia na maisha ya Sheikh Jafar Kashif al-Ghitaa. Tulisema kuwa, Sheikh Jafar Kashif al-Ghitaa alizaliwa mwaka 1154 Hijria katika mji mtakatifu wa Najaf. Nasaba yake inarejea na kufika kwa Malik al-Ashtar swahaba na kamanda shujaa na mwenye nguvu wa jeshi la Imam Ali bin Abi Twalib (as). Sheikh Jafar Kashif al-Ghitaa ameandika na kualifu vitabu vingi katika nyuga mbalimbali za kidini kama Fikihi na Usul. Sehemu ya 46 ya kipindi hiki juma hili itaendelea kumzungumzia alimu na mwanazuuoni huyu. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi.
Moja ya hatua muhimu zilizochukuliwa na Sheikh Jaafar Kashif al-Ghitaa na zilizokuwa athirifu katika kuutetea maktaba ya kifikra ya Uishia ni pale kundi potovu la Mawahabi liliposhambuulia NajaF mwaka 1215 Hijria. Mawahabi wakimfuata kiongozi wao Muhammad bin Abdul-Wahhab walikuwa wakiamini kwamba, akthari ya amali na matendo ya Waislamu iwe ni Masuni au Mashia ni shirki. Wakitumia wenzo na fikra yao hiyo, walikuwa wakiwakufurisha na kuwatambua kuwa ni makafiri akthari ya Waislamu hususan Mashia. Wakiwa na uelewa mbaya na potofu kuhusiana na dini na Qur'ani walichukua hatua za kuua na kupora mali za Waislamu.
Mwaka 1215 Mawahabi walifanya hujuma na mashambuulio dhidi ya miji ya Karbala na Najaf Iraq ambapo sambamba na kubomoa haramu tukufu ya Imam Hussein waliwaua mamia ya wanaume na wanawake wasio na hatia waliokuwa katika haram hiyo. Kisha wakaanza kufanya uporaji huko Karbala. Habari ya jinai hiyo ikafika katika mji wa Najaf na wakazi wa mji huo wakawa wamekumbwa na hali ya wahka na wasiwasi.
Sheikh Kashif al-Ghitaa katika zama hizo alikuwa akiishi katika mji wa Najaf. Aliwashajiisha watu wajitokeze na kuutetea mji wao. Yeye mwenyewe Sheikh Kashif al-Ghitaa alijizatiti kwa silaha na Maulamaa wengine, matalaba (wanafunzi wa masomo ya dini) na wananchi nao wakajizatiti kwa silaha. Katika zama hizo, nyumba ya Sheikh Kashif al-Ghitaa ilikuwa ghala la silaha na mahali pa kukusanyikia wanamapambano na wapiganaji. Kwa mwongozo na usimamizi wa alimu na msomi huyu, Mashia waliweza kusimama kidete dhidi ya uvamizi wa Mawahabi kwa muda wa miezi minne. Hatimaye wavamizi walishindwa kupenya na kuingia katika mji wa Najaf. Baada ya mkasa na tukio hilo, Sheikh Kashif al-Ghitaa alitoa agizo la kujengwa kuta ndefu na imara kuzunguka mji wa Najaf, ili Mawahabi watakapovamia washindwe kupenya kirahisi katika mji huo na hivyo wakazi wake kusalimika na shari yao.
Unyeti na uzingatiaji maalum aliokuwa nao Marjaa huyu mkubwa wa Kishia wa kulinda roho na mali za Waislamu mbele ya hujuma na uvamizi ni jambo lililowafanya wakazi wa mji wa Najaf na viunga vyake kuifanya nyumba ya alimu na msomi huyu kuwa kimbilio kila panapojitokeza tukio fulani. Katika uga wa kupambana na kukabiliana na Mawahabi kwa njia ya kielimu na kiitikadi, Sheikh Kashif al-Ghitaa ameandika kitabu kinachojulikana kwa jina la Manhah al-Rashad Liman Arada al-Sadad (مَنهَجُ الرَّشاد لِمَن ارادَ السَّداد) ambapo ndani ya kitabu hicho amekosoa itikadi na mitazamo ya Mawahabi ambapo inaonekana kuwa, kilikuwa kitabu cha kwanza katika uwanja huo.
Mwaka 1222 Hijria, Sheikh Kashif al-Ghitaa alifanya safari nchini Iran na kupokewa na Maulamaa na wananchi wa kawaida. Katika safari yake hii, mwanazuoni huyu mahiri aliandaa vikao vya mawaidha na midahalo mikubwa katika maeneo mbalimbali ya Iran na kufanya hima na juhudi kubwa ya kueneza madhehebu ya Ahlul-Baiti ambapo alikuwa akijibu maswali na shubhaa zilizokuwa zikielekezwa dhidi ya madhehebu haya.
Akiwa katika kilele cha umashuhuri na uwezo wa kidini na kisiasa, Sheikh Kashif al-Ghitaa alifunga safari na kwenda Tehran kwa ajili ya kwenda kukutana na mtawala wa wakati huo wa Iran Fat'h Ali Shah Qajar. Alikutana naye na kumpatia zawadi ya kitabu chake mashuhuri cha Kashful-Ghitaa. Kitabu hicho ndio kitabu mashuhuri zaidi cha alimu huyo ambacho baada ya kukiandika ndipo alipoondokea kuwa mashuhuri kwa jina la Kashif al-Ghitaa.
Katika zama hizo Iran ilikuwa imeshughulishwa na vita na Russia na Kashif al-Ghitaa alikuwa akilipa umuhimu mno suala la kuhifadhi nguzo na nguvu za Waislamu. Akiwa Marjaa wa dini alimpa ijaza Fat'hi Ali Shah kwa ajili ya kukusanya askari, kama ambavyo alitoa jibu chanya kwa takwa la mtawala huo kwa ajili ya kutoa fatuwa ya jihadi.
Sheikh Kashif al-Ghitaa alikuwa na itibari kubwa kwa tawala za Iran na Othmania na ni kwa kuzingatia uhakika huo ndio maana maneno yake yalikuwa na nafasi muhimu katika kuondoa mzozo na hitilafu zilizokuwa zikijitokeza baina ya tawala mbili hizo.
Mwaka 1219 Hijria wakati jeshi la Iran lilipojikusanya na kuanza safari ya kuelekea Baghdad kwa ajili ya vita, Ali Pasha mtawala wa wakati huo wa Baghdad alimuomba Sheikh Kashif al-Ghitaa aende Iran na kuonana na kamanda wa jeshi la nchi hiyo ili kuzua vita baina ya pande mbili. Mwanazuoni huyu ambaye alikuwa akitambua vyema kwamba, pendekezo la Ali Pasha ni kwa maslahi ya Waislamu alikubali ombi hilo na kufuatia mazungumzo yake na Kamanda wa jeshi la Iran alifanikiwa kusitisha vita na wafungwa wa Kituruki na Kiarabu wakaachiliwa huru.
Mwaka 1221 Hijria ambapo kuliibuka tena vita baina ya nchi mbili, Sheikh Kashif al-Ghitaa akawa mpatanishi baina ya kamanda wa jeshi la Iran na mtawala wa Baghdad na kufanikiwa kwa mara ya pili kuzua vita na umwagaji damu baina ya Waislamu.
Mwanazuoni huyo mbali na kujihusisha na kazi za kielimu, kusimamia Chuo cha Kidini, kufundisha na kuandika vita, alikuwa akizingatia na kuyapa umuhimu pia masuala ya kijamii na kisiasa kama ambavyo hakuwa nyuma pia katika suala la familia na malezi ya watoto wake. Watoto wake watatu walisoma na kufikia daraja ya Ijtihadi na kuondokea kuwa miongoni mwa wanazuoni na mafakihi watajika.
Hatimaye baada ya umri uliojaa baraka na jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu na katika kuhudumia madhehebu ya Ahlul-Baiti, Sheikh Kashif al-Ghitaa aliaga dunia mwezi Rajab 1228 Hijria. Mwanazuoni huyo amezikwa katika mji wa Najaf katika chuo cha kidini (Hawza) alichokijenga mwenyewe.
Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu juma hili umefikia tamati msisite kujiunga nami katika sehemu nyingine ya mfululizo wa vipindi hivi vya Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu.
Ahsanteni kwa kunitegea sikio na kwaherini.