Jumatano, Juni 15, 2022
Leo ni Jumatano mwezi 15 Mfunguo Pili Dhulqaad, 1443 Hijiria inayosadifiana na tarehe 15 Juni 2022 Milaadia.
Miaka 943 iliyopita, kwa mujibu wa riwaya za kihistoria, katika siku kama hii, tarehe kumi na tano ya Dhiqaadah katika mwaka wa 500 Hijiria, Ibn Fakhir, msomi wa ngazi za juu wa Kiislamu na mwandishi wa kamusi, aliaga dunia huko Baghdad. Akiwa kijana mdogo, alifunga safari nyingi kwenda Makka na Yemen, kwa lengo la kupata elimu kutoka kwa wanazuoni wa wakati huo, na akawa msomi aliye tabahari katika msamiati na hadithi. Mtindo wa uandishi wa Ibn Fakhir umeegemezwa kwenye nathari adhimu iliyochanganywa na ufundi wa maneno, lakini ni fasaha na wazi. Miongoni mwa kazi za Ibn Fakhir, tunaweza kutaja kitabu "Jibu kwa Matatizo".
Tarehe 15 Juni miaka 314 iliyopita harakati ya wapigania uhuru wa Scotland ilikandamizwa vikali na Uingereza. Uingereza daima imekuwa ikifanya jitihada za kuiunganisha Scotland na ardhi ya kaskazini mwa nchi hiyo. Hata hivyo harakati za mapambano za Wascotland zilipinga vikali suala hilo. Hata hivyo mwaka 1707 mabunge ya nchi hizo mbili yaliunganishwa. Suala hilo liliwakasirisha sana Wascotland walioanzisha harakati nyingine ya mapambano mbayo ilikandamizwa vikali katika siku kama ya leo hapo mwaka 1708.
Siku kama ya leo miaka 174 iliyopita sawa na tarehe 15 Juni 1848, Otto von Bismarck Kansela wa Ujerumani aliuchagua mji wa kihistoria na maarufu wa Berlin, kuwa mji mkuu wa nchi hiyo. Kuteuliwa mji wa Berlin kuwa mji mkuu wa Ujerumani, kulitokana na utekelezaji wa mpango wa kuziunganisha Ujerumani mbili, uliobuniwa na Kansela Bismarck. Baada ya Vita vya Pili vya Dunia, Ujerumani iligawanyika katika sehemu mbili za Mashariki na Magharibi. Mwezi Septemba 1990 baada ya kuvunjwa ukuta wa Berlin, kuliandaliwa mazingira ya kuunganishwa pande hizo mbili, na hatimaye Berlin kurejea tena na kuwa mji mkuu wa Ujerumani.
Siku kama ya leo miaka 27 iliyopita, mwafaka na tarehe 15 Juni 2000, idadi kubwa ya askari wa kikosi maalumu cha jeshi la Uingereza iliondoka kwenye ardhi ya Sierra Leone, magharibi mwa Afrika. Amri ya kuondoka vikosi hivyo vya Uingereza ilitangazwa na John Prescott, Naibu Waziri Mkuu wa Uingereza. Wanajeshi wengine 300 wa nchi hiyo waliendelea kubaki nchini Sierra Leone kwa wiki kadhaa kwa shabaha ya kutoa mafunzo kwa jeshi la nchi hiyo.
Miaka 104 iliyopita, siku ya ishirini na tano ya Khordad mwaka 1297 Hijiria Shamsiya,Ayatullah "Seyyed Mostafa Mojtahed Kashani", mwanachuoni na mujahid mashuhuri, alifariki dunia. Alizaliwa Kashan, mojawapo ya miji ya kati ya Iran, katika familia ya wanazuoni, na alipata elimu yake ya awali kutoka kwa baba yake. Kisha akaenda Isfahan nchini Iran na kisha Najaf huko Iraq kumalizia elimu yake ili kufaidika na elimu ya wanazuoni wengi zaidi, na hatimaye akaifikia cheo cha Ijtihad. Ayatullah Mostafa Kashani pia alikuwa na uwezo wa hali ya juu katika ushairi na aliandika mashairi kwa Kiajemi au Kifarsi na Kiarabu. Lakini sifa zake muhimu zaidi ni kupinga dhumla na kutetea haki. Msomi huyu mkubwa alikuwa ni miongoni mwa wapinzani wa dhulma na waungaji mkono wa Mapinduzi ya Kiktiba ya Iran na alipigana dhidi ya uingiliaji wa wakoloni wa Uingereza na Russia nchini Iran na Iraq. Kwa mfano, wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia na uvamizi wa Waingereza nchini Iraq, Ayatullah Seyyed Mustafa Kashani sio tu alitoa fatwa za jihad na wanachuoni wengine, bali pia alionekana kwenye medani za vita dhidi ya wakoloni. Mwanawe, Ayatullah Seyyed Abolghasem Kashani, pia alikuwa mmoja wa wapiganaji wakubwa dhidi ya ukoloni wa Uingereza, hasa wakati wa kutaifishwa kwa sekta ya mafuta ya Iran.