Jumatatu tarehe 11 Julai 2022
Leo ni Jumatatu tarehe 11 Mfunguo Tatu Dhulhija 1443 Hijria ambayo inasadifiana na tarehe 11 Julai 2022.
Tarhe 11 Julai imepewa jina la Siku ya Kimataifa ya Jamii. Siku ya leo inakumbusha tukio la tarehe 11 Julai 1978 wakati idadi ya watu duniani ilipopindukia bilioni 5. Takribani miaka 40 iliyopita, Umoja wa Mataifa kwa mara ya kwanza ulitoa mpango wa kupanga na kudhibiti idadi ya watu duniani. Hatua hiyo ilitokana na kuwa, ongezeko la watu linahitajia ustawi wa kudumu, upanuzi wa miji na kupatikana huduma muhimu kama za tiba. Kutokana na uhakika huo, kuna haja kwa mataifa yote ya dunia kuandaa mipango mizuri ili kuhakikisha watu wanaishi maisha salama, umasikini unapungua, kunakuweko na uwiano wa ukuaji na uongezekaji wa idadi ya watu, kuweko familia na jamii salama na ambazo zitaishi katika maisha mazuri na salama zaidi. Siku hii huadhimishwa kila mwaka kama Siku ya Idadi ya Watu Duniani.
Katika siku kama ya leo miaka 778 iliyopita, mji wa Baitul Muqaddas ulikombolewa na Waislamu wakati wa Vita vya Msalaba. Vita vya Msalaba vilianza mwishoni mwa karne ya 11 Miladia na watu wa Ulaya waliwatwisha Waislamu vita hivyo. Watu wa msalaba walianzisha vita hivyo kidhahiri wakiwa na lengo la kuteka Baitul Muqaddas, ingawa shabaha halisi ya wapiganaji hao ilikuwa ni kudhibiti ardhi kubwa za Waislamu na kuwanyonya na kuwakoloni wafuasi wa dini hiyo. Katika vita hivyo wafuasi wa kanisa walichora alama za msalaba kwenye mabega na mavazi yao, na kwa sababu hiyo vita hivyo vimekuwa maarufu kwa jina la Vita vya Msalaba.
Miaka 465 iliyopita katika siku kama ya leo, Sebastian Cabot mvumbuzi na mwanabaharia wa Kiitalia aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 81. Tangu awali alikuwa akifanya safari na baba yake aliyekuwa mwanabaharia na kwa msingi huo akafanikiwa kujifunza mambo mengi yanayohusiana na ubaharia.
Siku kama ya leo miaka 101 iliyopita, nchi ya Mongolia ilijitangazia uhuru. Mongolia ina historia kongwe mno. Changiz Khan Moghol alianza kuziteka ardhi za nchi hiyo mwanzoni mwa karne ya 13 na kusonga mbele hadi Ulaya ya mashariki. Mongolia iligawanyika katika sehemu mbili yaani Mongolia ya nje na ya ndani baada kusambaratika utawala wa kifalme wa Wamogholi. Mongolia ya ndani iliijumuisha China, na Mongolia ya Nje ikawekwa chini ya udhibiti wa China mwishoni mwa karne ya 17.
Miaka 99 iliyopita katika siku kama ya leo yaani tarehe 11 Mfunguo Tatu Dhulhija alifariki dunia Ayatullah Mirza Jawad Malaki Tabrizi ustadhi mkubwa wa akhlaqi, msomi na arif wa Kiislamu. Alizaliwa katika mji wa Tabriz moja ya miji ya Iran na baada ya kukamilisha masomo yake ya msingi na ya kati alielekea katika Chuo Kikuu cha Kidini cha Najaf nchini Iraq. Akiwa huko alihudhuria darsa za maustadhi mahiri katika zama hizo kama Haji Agha Reza Hamadani, Akhund Khorasani, Muhaddith Nuri na Akhund Hamedani. Mwanazuoni huyo mbali na kufundisha na kulea wanafunzi wengi hakuwa nyuma pia katika taaluma ya uandishi wa vitabu. Asraru Salat, al-Muraqabaat na A'amalu al Sunna ni baadhi tu ya vitabu vya Ayatullah Mirza Jawad Maliki Tabrizi.*
Na miaka 27 iliyopita katiak siku kama ya leo, Waislamu zaidi ya elfu nane wa mji wa Srebrenica mashariki mwa Bosnia Herzegovina waliuawa kwa umati. Mauaji hayo yalifanywa na Waserbia wenye misimamo mikali. Maafa hayo yalikuwa mauaji makubwa zaidi ya halaiki kuwahi kutokea barani Ulaya baada ya Vita vya Pili vya Dunia. Wanamgambo wa Kiserbia wakiungwa mkono na serikali ya Belgrade, waliuvamia mji wa Srebrenica licha ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kulitangaza eneo hilo kuwa la amani mwaka 1993 na kutumwa askari wa umoja huo katika mji huo. Waislamu wa mji wa Srebrenica walijaribu kuondoka katika mji huo, lakini watenda jinai wa Kiserbia waliwauwa wanaume na watoto wao wa kiume na kuwaruhusu wanawake kuondoka katika mji huo. Wakati wa mauaji hayo ya kimbari, wanajeshi wa kulinda amani wa Uholanzi waliokuweko katika eneo hilo hawakuchukua hatua yoyote ya kuwahami Waislamu hao wa Srebrenica.