Familia Salama (5)
Katika Makala yetu iliyopita tuliangazia umuhimu wa maziwa katika lishe. Makala yetu ya leo itaangazia faida na umuhimu wa samaki katika lishe ya familia. Hakuna shaka kuwa kati ya matakwa muhimu zaidi ya kila mwanadamu ni kuwa na usalama wa kimwili na kuishi maisha mazuri pasina kukabiliwa na hatari ya kuambukizwa magonjwa.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanyika, moja kati ya mambo muhimu katika kupata afya bora ni kuwa na lishe bora yenye kujumuisha makundi yote ya vyakula. Iwapo mwanadamu atazingatia lishe kamili, basi ataweza kujizuia kupata maradhi mbali mbali.
Kati ya vyakula muhimu kwa afya ya mwanadamu ni samaki. Ingawa wengi hutumia samaki kama kitoweo katika jamii za Afrika Mashariki, ni wachache wanaofahamu umuhimu wa chakula hicho katika afya ya mwanadamu. Kwa hakika samaki ni chakula muhimu sana na chenye faida kubwa katika mtazamo wa lishe. Wataalamu wa tiba na lishe wanashauri kuwa, ili kuzuia idadi kubwa ya magonjwa na pia kuponya magonjwa yaliyoibuka, utumizi wa samaki katika lishe ni jambo la dharura.
Iwapo katika familia, samaki atatumika katika lishe mara mbili hadi tatu kwa wiki, basi jambo hilo linaweza kuwa na mchango mkubwa katika kuzuia magonjwa mengi na kuimarisha afya jumla ya wanafamilia.
Leo wataalamu wamebaini kuwa kutumia samaki na wanyama wengine wa baharini hupunguza athari mbaya za mafuta mabaya mwilini maararufu kama bad cholesterol. Hii ni kwa sababu samaki na wanyama wa baharini wana mafuta yajulikanayo kama omega-3 ambayo yana asidi maalumu yenye kupunguza cholesterol mwilini.
Kutokana na kuwa samaki ina virutubisho maalumu, husaidia sana katika kuchoma mafuta mwilini na hivyo kupunguza mafuta mabaya au lehemu katika mwili wa mwanadamu. Kwa msingi huo kutumia samaki katika lishe mara kadhaa kwa wiki husaidia kupunguza unene na kufanya uzito wa mwili uwe wa kiwango cha wastani. Aidha samaki huwa na nafasi muhimu katika kupunguza shinikizo la damu mwilini.
Samaki ana protini nzuri ambayo inaweza kuvunjwavunjwa kirahisi tumboni. Kama tulivyotangulia kusema samaki wana virutubisho aina ya Omega 3 ambavyo huulinda moyo dhidi ya maradhi. Samaki pia wana virutubisho vinavyomuongezea mlaji uwezo wa kukumbuka (memory), kuna virutubisho vyenye uwezo wa kupambana na kansa mwilini, kuongeza kinga ya mwili na kuondoa mafuta mabaya mwilini (Bad cholesterol). Baadhi ya virutubisho muhimu vinavyopatikana kwenye samaki ni pamoja na vitamini D, vitamin 12, vitamini B3, vitamini B6, Omega 3 Fatty acids, protini na madini mengine mengi. Virutubisho hivyo na vingine vingi katika samaki huwa na umuhimu mkubwa katika kulinda afya ya mwanadamu. Hali kadhalika wataalamu wanasema utumizi wa samaki pia huweza kuimarisha uwezo wa kuona na kuimarisha nuru ya macho. Hapa watu wenye umri wa juu au wazee wanashauriwa kutumia samaki kuboresha macho yao na kuyazuia yasidhoofike.
Hali kadhalika kuwepo samaki au vyakula vingine vinavyotokana na wanyama wa baharini pia husaidia mwili kupata nguvu na kinga ya kukabiliana na baadhi ya magonjwa.
Uchunguzi uliofanywa umebaini kuwa, utumizi wa samaki katika lishe huwa na taathira za kimuujiza katika kutibu maradhi mengi kama vile shinikizo la damu, rheumatism au ugonjwa baridi, Pneumonia, maumivu makali ya kichwa na ugonjwa wa pumu au asthma.
Watafiti wa Chuo Kikuu cha Kuopio nchini Finland wanasema kuwa, watu ambao hula samaki mara mbili kwa wiki, hupunguza kwa asilimia 37 uwezekano wa kupata ugonjwa wa msongo wa mawazo au depression huku wakipunguza kwa asilimia 43 fikra za kujidhuru. Katika utafiti mwingine uliofanyiwa watu 265,000 nchini Japan kwa muda wa miaka 17, ilithibitika kuwa, hatari ya kujiua miongoni mwa wanaotumia samaki kila siku ni ndogo ikilinganishwa na wale wasiotumia samaki.
Watafiti wa Kitivo cha Tiba cha Chuo Kikuu cha Havard Marekani wanaamini kuwa watu wanaoishi katika visiwa na ambao hutumia samaki mara kwa mara katika kitoweo chao huwa wamesalimika pakubwa na hatari ya kupata tatizo la kiakili la hofu iliyopitiliza au anxiety disorder.
Kwa mujibu wa tafiti mbali mbali, wataalamu, wamefikia natija kuwa ili kuondoa matatizo mbali mbali ya kiakili kama vile msongo wa mawazo, hofu, iliyopitiliza, fikra za kujidhuru n.k , watu wote wanashauriwa kutumia samaki au mafuta ya samaki mara kwa mara.
Kutumia samaki na wanyama wengine wa baharini katika lishe pia ni muhimu na dharura kwa wanawake wenye mimba na wanaonyonyesha.
Hii ni kwa sababu aina hiyo ya lishe huwa na nafasi muhimu katika kustawisha na kuimarisha ubongo wa vijusi na watoto wanaonyonya.
Iwapo wanawake wenye mimba watatumia kiasi cha kutosha cha samaki katika lishe ya kila siku, basi wataweza kuleta mlingano mzuri katika uzito wao.
Athari nyingine muhimu ya samaki na wanyama wa baharini kwa kina mama wajawazito ni kuwa uzito wa kijusi kilicho tumboni huwa wa wastani na hivyo mtoto anapozaliwa hawi mnene kupita kiasi. Wataalamu wa lishe wanashauri kuwa, katika kuchagua samaki wa kula, wale wenye kuenda kwa kasi huwa bora zaidi. Aidha samaki hapaswi kuwa mgumu sana na inafadhilishwa kutumia samaki aliye freshi ambaye hajagandishwa. Aidha njia bora zaidi ya kumpika samaki ni kumchoma au kumpika kwa mvuke badala ya mapishi ya kutumbukiza ndani ya mafuta mengi ya moto au deep frying.
Ni matumaini yangu kuwa tutaweza kuzingatia na kula chakula salama chenye kulinda afya ya familia na jamii nzima kwa ujumla.