Aug 30, 2022 06:48 UTC
  • Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (50)

Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Karibuni kujiunga nami tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu. Kipindi chetu kilichopita kilimzungumzia Sayyid Muhammad Tabatabai anayejulikana pia kama Ayatullah Mujahid. Tulisema kuwa, alizaliwa 1180 Hijria katika mji wa Karbala, Iraq. Tulibainisha kwamba, kutokana na hima na idili kubwa aliyokuwa nayo Sayyid Muhammad Mujahid katika kujifunza elimu aliweza kwa haraka mno kukwea daraja za kielimu. Zama za Umarjaa wa Ayatullah Sayyid Muhammad Tabatabai zilisadifiana na kipindi cha kuanza duru ya pili ya vita vya Iran na Russia na Maulamaa chini ya uongozi wake walikuwa na nafasi na mchango mkubwa na athirifu. Sehemu ya 50 ya mfululizo juma hili itamzungumzia Sayyid Abdallah Shubbar mmoja ya Maulamaa wa Kishia aliyeishi katika karne ya 13 Hijria. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

 

Sayyid Abdallahh Shubbar alizaliwa mwaka 1188 Hijria katika mji wa Najaf Iraq. Yeye ni mmoja wa Maulama ambaye kizazi chake kinaishia kwa kizazi kitakatifu cha Imam wa nne wa Ahlul-Beiti (as), Imam Hussein bin Ali Zeinul Abidin (as).

Baba yake yaani Sayyid Muhammad Ridha alikuwa miongoni mwa wasomi, Maulamaa na wachamungu watajika mjini Najaf ambapo watu walimpa lakabu ya "Swahib al-Da'wat al-Mustajabah" kwa maana ya mtu ambaye dua yake ilikubaliwa. Mkasa wa dua iliyokubaliwa unarejea katika zama za utawala wa Othmnia ambapo mji wa Baghdad ulikumbwa na ukame mkubwa. Katika zama hizo, Said Pasha kiongozi wa utawala wa Othmania mjini Baghdad aliwataka watu wafunge Swaumu kwa muda wa siku tatu na waende nje ya mji kwa ajili ya kuswali Swala ya kuomba mvua. Watu walitekeleza agizo hilo ambapo wakiwa pamoja na mtawala Said Pasha waliswali Swala ya kuomba mvua katika ardhi ya jangwa nje ya mji.

Lakini siyo siku hiyo tu bali hata siku zilizofuata mvua haikunyesha. Kukawa kumejitokeza ghamu, huzuni na wasiwasi miongoni mwa watu. Baada Sayyid Muhammad Ridha kuona juhudi za Said Pasha hazijazaa matunda alichukua hatua ya kusimamisha Swala ya kuomba mvua. Aliwataka wananchi wa mji wa Kadhmein wafunge tena Swaumu kwa muda wa siku tatu na wafuatane naye nje ya mji kwa ajili ya kusimamisha Swala ya kuomba mvua (al-Istisqaa). Wakazi wa mji wa Kadhmein wakatekeleza agizo hilo na mara hii wakaswali Swala ya kuomba mvua nyuma ya fakihi na msomi mchamungu zaidi katika mji huo. Wakanyoosha mikono yao mbinguni na wakiwa na unyenyekevu mkubwa wakaomba Allah awape neema ya mvua. Sayyid Muhammad Ridha akiwa katika hali ya kuomba dua, mara mawingu ya mvua yakaanza kutanda na matone ya mvua yakaanza kudondoka. Tukio hilo lisilosahaulika, lilipelekea watu wampe Sayyid huyu mchamunguu kutoka familia ya Shubbar lakabu ya "Swahib al-Da'awat al-Mustajabah" na wakazidi kumheshimu na kumtukuza.

Sayyid Abdallah Shubbar

 

Sayyid Abdallah Shubbar alikulia na kuinukia chini ya usimamizi wa malezi ya baba yake na kusoma kwa mzazi wake huyo. Sayyid Muhammad Ridha ambaye ni baba wa Sayyid Abdallah Shubbar daima alikuwa akimnasihi mwanawe kutumia vyema wakati na lahadha za maisha na alikuwa akimshajiisha kuwa mchamungu na kusoma. Aidha alikuwa akimuandalia suhula na nyenzo kwa ajili ya kufikia malengo haya. Hata hivyo alimuwekea sharti mwanawe kwa kumwambia kwamba: "Endapo itatokea ukazembea japo siku moja tu, katika kutafuta elimu na kuwasomesha wengine, basi sitakuwa radhi utumie kile ambacho nimekuandalia".

Sayyid Abdallah Shubbar kivitendo alifanya kila awezalo tena kwa hima kubwa kutekeleza maneno haya ya baba yake, kiasi kwamba, ikitokea siku ameugua na hivyo kushindwa kusoma alikuwa akijuzuia kutumia suhula alizoandaliwa na baba yake. Hima na kutokuwa na mzaha hata kidogo namna hii katika njia ya elimu na uchajimungu, ndiko kulikomjenga msomi huyu na kumfanya aondokee kuwa shakhsia mkubwa katika kumcha Mwenyezi Mungu na msomi aliyebobea na kutabahari katika elimu ya fikihi.

Baada ya kuaga dunia baba yake mwaka 1208 Hijria, Sayyid Abdallah alianza kuhudhuria darsa na masomo yaliyokuwa yakitolewa na Sayyid Muhsin A'raji mtafiti na mhakiki mtajika wakati huo mjini Baghdad. Akiwa chini ya mafundisho yake, akachomoza na kuwa alimu na msomi mtajika.

Mwanazuoni huyo mchamungu wa Kadhmein hakuwa mahiri tu katika elimu ya fikihi, bali alifanikiwa pia kulea wanafunzi na wafuasi wake katika maadili mema na uchajimungu. Alikuwa mashuhuri kwa kujipaka manukato yenye harufi nzuri na alifahamika pia kwa kauli njema na kuzungumza kwa lugha nzuri na maneno matamu nay a kuvutia na watu. Kwa hakika hayo ni mambo ambayo yaliwafanya watu wamuelekea. Mmoja wa wanafunzi wake anasema hivi kuhusiana na mwalimu wake huyu: Wakati mtu alipokuwa akiitazama sura yake na kusikiliza maneno yake ya kutua moyoni, hakuwa tebna akiweza kutengana naye. Sayyid Abdallah Shubbar alikuwa akizingatia mno suala la dua na ibada.

 

Inanukuliwa kwamba, alikuwa akisimama na kufanya ibada kwa ajili ya Mola wake kwa muda mrefu kiasi kwamba, miguu yake ilikuwa ikipata maumivu, lakini ladha ya ibada ilikuwa ikiondoa mchoko wote. Aidha kufundisha na kufanya ibada kwa wingi kwa mwanazuoni huyu, hakukumghafilisha na suala la kushughulikia mambo ya Waislamu. Alikuwa akilipa umuhimu maalumu suala la kukidhi mahitaji ya wasiojiweza, alikuwa akiwatembelea wagonjwa kama ambavyo alikuwa akifanya hima kubwa kwa ajili ya kuachiwa huru watumwa.

Katika kipindi cha umri wake wa miaka 54 Sayyid Abdallah amefanikiwa kuvirithisha vizazi vilivyokuja baada yake zaidi ya vitabu 70 katika uga wa fikihi na tafsiri. Maulamaa na Mamujtahidi wanalinganisha orodha kubwa ya vitabu vya Sayyid Abdallah na Allama Muhammad Baqir Majlisi na ndio maana wanamtaja msomi huyu kama ni Majlisi wa Pili. Mwanazuoni huyu alikuwa makini mno katika uandishi wa vitabu na daima alikuwa akiwaacha vinywa wazi wasomi na wanazuoni wakubwa katika zama hizo kutokana na kuwa makini katika uandishi. Kuna wakati alikuwa akitumia masaa kadhaa au nusu siku na kuandika maandiko yenye kubeba maana na muhtawa wa hali ya juu.

 

Moja ya vitabu vyake mashuhuri ni tafsiri za pande tatu zinazijulikana kama Tafisrul Kabir au Safwat al-Tafsiri, Tafsiril Wasiyt au al-Jawhar Thamin na Tafsirul Wajiz. Sayyid Muhammad Maasum mmoja wa wasomi na wanazuoni wakubwa wa elimu ya fikihi katika karne ya 13 anaandika katika utangulizi wa tafsiri ya Shubbar: Imam Shubbar ni mmoja wa shakhsia waliokuwa na kheri na baraka nyingi ambapo historia itambakisha milele. Ana mtaji mkubwa wa elimu, kipaji nadra cha kuhifadhi mambo na ufahamu mpana wa mambo. Sisi hatuna kingine cha kufanya mbele ya shakhsia yake ghairi ya kuinamisha kichwa cha taadhima na heshima.

Sayyid Abadllah Shubbar hatimaye aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 54. Ilikuwa ni katika moja ya masiku ya mwezi wa Rajab mwaka 1242 Hijria. Mwanawe yaani Sayyid Hassan ambaye naye alikuwa fakihi na msomi mkubwa akiwa pamoja na kundi kubwa la watu, walimswalia mzazi wake huyu Swala ya Maiti na kisha kumzika katika Haram ya Imam Mussa al-Kadhim (AS).

Tunakamilisha kipindi chetu cha leo kwa hadithi ya Imam Ali bin Abi Talib AS ambapo amenukuliwa akisema: Alimu yu hai hata akiwa amekufa, mjinga ni mfu hata akiwa yu hai.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.