IRGC yaonya kuwa vita vipya dhidi ya Iran vitavuka mipaka ya eneo
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i138518-irgc_yaonya_kuwa_vita_vipya_dhidi_ya_iran_vitavuka_mipaka_ya_eneo
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limetoa onyo kali kwamba endapo vita dhidi ya Iran vitaanzishwa tena, basi vita vya kikanda vilivyoahidiwa hapo awali safari hii vitapanuka kuvuka eneo la Asia Magharibi, na kwamba mapigo mazito yataelekezwa kutoka maeneo ambayo adui hawezi kuyadhania.
(last modified 2026-05-21T04:42:32+00:00 )
May 21, 2026 04:40 UTC
  • IRGC
    IRGC

Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limetoa onyo kali kwamba endapo vita dhidi ya Iran vitaanzishwa tena, basi vita vya kikanda vilivyoahidiwa hapo awali safari hii vitapanuka kuvuka eneo la Asia Magharibi, na kwamba mapigo mazito yataelekezwa kutoka maeneo ambayo adui hawezi kuyadhania.

Katika taarifa iliyotolewa Jumatano, IRGC iliwahutubia moja kwa moja viongozi wa Marekani, ikisema kwamba “adui Mmarekani-Mazayuni” haujajifunza kutokana na kushindwa mara nyingi kimkakati mbele ya Mapinduzi ya Kiislamu na sasa umerejea katika lugha ya vitisho. Taarifa hiyo ilieleza: “Ingawa walitushambulia kwa uwezo kamili wa majeshi mawili,  majeshi yenye bajeti kubwa zaidi duniani , sisi hatukutumia uwezo wote wa Mapinduzi ya Kiislamu dhidi yao.”

Taarifa iliendelea kusema kuwa: “Lakini sasa, iwapo uchokozi dhidi ya Iran utarudiwa, basi vita vya kikanda tulivyotabiri awali vitapanuliwa nje ya eneo hili, na mapigo yetu ya kusambaratisha yatawaangusha katika vumbi jeusi katika sehemu msizoweza kuzifikiria.”

Taarifa hiyo, iliyowekwa chini ya Aya ya Qur’ani Tukufu isemayo: “…basi piganeni na waongozi wa ukafiri. Hakika hao hawana viapo vya kweli. Huenda (kwa hayo) wakaacha. (Surat At-Tawbah, aya ya 12), ilisisitiza kwamba IRGC haitatoa maonyo kupitia maneno matupu bali itaonyesha uwezo wake “katika uwanja wa mapambano.” Waliongeza kuwa: “Sisi ni watu wa uwanja wa vita, na mtauona uwezo wetu huko, si katika maneno matupu au kurasa za mtandaoni. Na ushindi hautoki ila kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Mwenye hekima.”

Onyo hilo limetolewa wakati matamshi ya kivita yakiongezeka kutoka kwa Rais wa Marekani, Donald Trump, ambaye katika siku za karibuni ametishia kufanya mashambulio mapya dhidi ya Iran endapo mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja ya kidiplomasia hayatokamilika kwa makubaliano.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, naye mapema Jumatano alionya kwamba kurejea katika vita dhidi ya Iran “kutaleta mshangao zaidi na mkubwa.”

Mashambulio makali ya Marekani na Israel dhidi ya Iran yalizinduliwa tarehe 28 Februari kupitia mashambulizi ya anga yaliyolenga shule ya msingi Minab, na kusababisha kufariki kwa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Seyyed Ali Khamenei, pamoja na viongozi na makamanda waandamizi wa Iran.

Jamhuri ya Kiislamu ilijibu mashambulizi hayo kwa kurusha mamia ya ndege zisizo na rubani na makombora dhidi ya malengo ya kijeshi na ya kibiashara ya Marekani na Israel katika maeneo mbalimbali ya kanda.