Kulegeza kamba mara kwa mara Trump, ishara ya kuemewa mbele ya Iran
Pars Today - Rais wa Marekani Donald Trump, kwa mara ya kumi na moja katika kipindi cha wiki chache tu, amerudia tena majigambo yake ya kuishambulia Iran lakini baadaye anatafuta kisingizio cha kuakhirisha kushambulia.
Rais huyo wa Marekani mwenye ugonjwa wa wasiwasi, majigambo na kujiamini kupita kiasi, kwa mara nyingine siku ya Jumatatu alilazimika kulegeza tena kamba katika vitisho vyake vya kufanya shambulio kubwa dhidi ya Iran siku ya Jumanne. Kisingizio kilichotumiwa mara hii na Trump kujaribu kuhalalisha kushindwa kwake kuanzisha vita vipya dhidi ya Iran ni madai yake kwamba viongozi wa nchi za Kiarabu wameomba mazungumzo na Iran yaendelee. Mtindo huu wa kuweka tarehe za mwisho ya kushambulia na kutoa matamshi makali na vitisho vya kijeshi lakini hatimaye kurudi nyuma umekuwa ukirudiwa mara nyingi na Trump kiasi kwamba sasa hauhesabiwi tena kuwa ni mkakati wa kijeshi, bali umekuwa ni ushahidi wa kuemewa na kukata tamaa Trump mbele ya Iran.
Wiki tano za mashambulizi makubwa ya pamoja ya Marekani na utawala pandikizi wa Israel yameshindwa kufikia malengo yoyote yaliyotangazwa na Washington. Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kijeshi wa Magharibi wameyaelezea mashambulizi hayo kuwa ni mashambulio makali zaidi kuwahi kufanywa katika eneo hili tangu baada ya Vita vya Ghuba ya Uajemi. Hata hivyo pamoja na kwamba mashambulio hayo yalikuwa makubwa sana, lakini Iran haijaacha mpango wake wa amani wa nyuklia, wala makombora yake ya balestiki, inaendelea kuunga mkono kwa nguvu zote Muqawama wa Ghaza, Lebanon na Yemen na ushawishi wake si tu haujapungua katika eneo hili, bali pia umepanua mipaka yake na kuenea maeneo mengi zaidi. Ukweli huu mchungu kwa Pentagon unaonekana hata katika ripoti za siri za kijasusi za Marekani. Kwa mujibu wa tathimini ya Shirika la Kijasusi la Marekani CIA na wizara ya vita ya nchi hiyo Pentagon, Iran bado ina takriban asilimia 70 ya uwezo wake wa makombora iliokuwa nao kabla ya vita vya Ramadhani. Si hayo tu bali pia kizazi kipya cha makombora ya Iran ya kupiga na kusambaratisha meli pia kimejaribiwa kwa mafanikio na kupelekwa mstari wa mbele kulinda Lango Bahari la Hormuz.
Lakini jambo kubwa na muhimu zaidi katika mlingano huu ni kwamba Iran ina silaha kubwa ambayo hakuna hata mmoja wa waathiriwa wa awali wa sera ya kibeberu za Trump (kama vile Venezuela) aliyekuwa nayo. Naam, hiyo ni silaha ya Lango Bahari la Hormuz. Hicho ni kikwazo kikubwa ambacho Marekani ilidhani kwamba kwa kuweka meli zake za kivita upande wa pili wa lango hilo itaidhuru Iran lakini sasa imekwama kwenye kinamasi cha Hormuz kutokana na Jamhuri ya Kiislamu kulifunga kikamilifu lango hilo na kuruhusu tu kupita meli inazotaka.
Usafiri wa meli za mafuta kupitia Lango Bahari la Hormuz umesimama huku masoko ya kimataifa yakiendelea kupokea mshtuko mpya kila siku. Mafuta ghafi ya Brent yamepanda kwa zaidi ya $110. Wachambuzi wa Wall Street wanaonya kuhusu "kusambaratika usalama wa mafuta duniani." Lakini zito zaidi ni kwamba mashinikizo yanarejea haraka Marekani: mfumuko wa bei wa kila mwaka wa asilimia 3.8 na petroli kwa dola 4 kwa pipa imemtumbukiza Trump katika shimo la hatari kubwa wakati huu wa kuelekea kwenye uchaguzi wa katikati ya muhula.
Sasa kwa kuzingatia yote hayo, hatua ya Trump ya kuendelea kulegeza kamba haipasiwi kufikiriwa kwamba inatokana na kuwaheshimu viongozi wa nchi za Kiarabu bali ni hofu yake ya kushindwa vibaya zaidi katika vita vya pande zote. Wachocheaji wa vita huko Washington wanaozungumzia kukivamia Kisiwa cha Kharg au kupora akiba ya urani ya Iran wanadhani kwa ujinga wao kwamba Jamhuri ya Kiislamu itakata tamaa au itafunga mikono na haitotoa majibu ya haraka. Lakini makamanda wa medani ya mapambano wa Iran wamesisitiza kwamba wako tayari muda wote na sekunde yoyote kutoa majibu makali zaidi na ya haraka zaidi kwa uadui wowote ule. Iran inasema, kama adui atafanya kosa jingine lolote la kuivamia ardhi yake, majibu ya Jamhuri ya Kiislamu hayatakuwa kupiga tu maeneo ya kijeshi ya Marekani katika eneo hili, bali kila atakayeruhusu ardhi yake kutumika kuishambulia Iran hatosalimika na hii ndio maana washirika wa kikanda wa Washington wakaitangazia wazi Marekani kwamba wanaogopa matokeo ya vita vya pande zote.
Ni muhimu kukumbuka kwamba Trump mwenyewe ameshajua kwa yakini kwamba kuendelea na vita vya kijeshi kutapelekea azidi tu kukwama kwenye kinamasi cha matope yanayonasa zaidi. Awali Trump alikuwa ametabiri kuwa Vita vya Ramadhani alivyovianzisha vitachukua "wiki nne hadi tano," lakini huu sasa ni mwezi wa tatu na bado hajafikia "ushindi" alioahidiwa. David Schenker, naibu waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Marekani anasema kuwa, hali iliyomkumbwa Trum hivi sasa ni mkwamo kwa maana yake halisi na kwamba rais huyo wa Marekani anaogopa kuingia kwenye vita kamili.
Kiujumla ni kwamba kilichopo leo hii ni kushindwa vibaya Marekani na utawala wa Kizayuni na vibara wao. Vitisho na kurudi nyuma mara kwa mara kunazidi kumfedhehesha tu adui. Adui hataki kukiri nguvu kubwa za Iran lakini ukweli ni kwamba haijalishi Trump ataendelea mara ngapi kutishia kuanzisha vita na halafu kurudi nyuma, lililo muhimu ni kwamba Iran imejipanga kutoa majibu makali zaidi kwa uchokozi wa adui. Madamu Iran inaendelea kutumia vizuri nafasi yake ya kujiografia kama Lango Bahari la Hormuz, Muqawama na ustahimilivu wa kimkakati, Marekani kamwe haitokuwa na njia rahisi ya kutoka kwenye mgogoro huu wa kihistoria iliyojitumbukiza ndani yake isipokuwa ikubali ukweli kuhusu nguvu za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.