Sep 03, 2022 04:27 UTC
  • Jumamosi, 3 Septemba, 2022

Leo ni Jumamosi mwezi 6 Mfunguo Tano Safar 1444 Hijria mwafaka na tarehe 3 Septemba 2022 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 810 iliyopita mwafaka na tarehe 6 Mfuunguo Tano Safar 634 Hijria, alizaliwa mwanafalsafa, mnajimu na tabibu mashuhuri wa Kiislamu Qutbuddin Mahmoud Shirazi katika mji wa Shiraz nchini Iran. Alianza kujifunza tiba akiwa bado mdogo na alianza kutibu wagonjwa katika moja ya hospitali za Shiraz baada ya kufariki dunia baba yake. Katika kipindi cha miaka kumi ya kazi ya utabibu, Qutbuddin Shirazi alitalii vitabu mbalimbali vya tabibu mwingine wa Kiislamu Bin Sina na vitabu vingine vya tiba na falfasa.Baada ya kuasisiwa kituo cha utafiti wa elimu ya nujumu katika eneo la Maraghe kaskazini magharibi mwa Iran, Qutbuddin Shirazi aliishi kipindi kirefu na mwanazuoni mashuhuri wa Kiislamu Khaja Nasiruddin Tusi na kujifunza elimu ya nujumu. Katika kipindi chote cha umri wake, tabibu huyo wa Kiislamu alitembelea miji na nchi mbalimbali na kukutana na wasomi na maulamaa wa maeneo hayo. Ameandika vitabu vingi kikiwemo kile cha Jaamiul Usul.Alifariki dunia mwaka 710 Hijria. ***

Qutbuddin Mahmoud Shirazi

 

Miaka 364 iliyopita katika siku kama ya leo, Oliver Cromwell Rais wa kwanza na wa mwisho wa Uingereza aliaga dunia. Alianza harakati za kisiasa na kijamii katika rika lake la ujana na mwaka 1640 alichaguliwa kuwa mwakilishi wa Bunge. Katika zama hizo Charles I ndiye aliyekuwa mfalme wa Uingereza. ***

Oliver Cromwell

 

Katika siku kama ya leo miaka 107 iliyopita aliuawa shahidi Rais Ali Delvari, kiongozi wa mapambano dhidi ya uvamizi wa Uingereza huko kusini mwa Iran. Mwanzoni mwa Vita vya Kwanza vya Dunia vikosi vya majeshi ya Urusi kutokea kaskazini na majeshi ya Uingereza kutokea kusini viliivamia na kuikalia kwa mabavu ardhi ya Iran. Wakati huo Rais Ali Delvari alitoa wito kwa wananchi kukabiliana na wavamizi wa Uingereza kwa kutegemea fatuwa ya vita vya jihadi iliyokuwa imetolewa na maulama wa Kiislamu ya ulazima wa kulinda nchi mbele ya maadui. Rais Ali Delvari na wapiganaji wenzake shupavu walikabiliana na mashambulizi ya mara kwa mara ya majeshi ya kigeni yaliyokuwa yamejizatiti kwa silaha na kuzuia kutekwa mji wa Busher. Mapambano ya wananchi wa Tengestan karibu na mji wa kuisni wma Iran wa Busher dhidi ya majeshi vamizi ya Uingereza yaliendelea kwa kipindi cha miaka 7.  ***

Rais Ali Delvari

 

Siku kama ya leo miaka 104 iliyopita, Damascus mji mkongwe na wa kihistoria wa Kiislamu ulikaliwa kwa mabavu na vikosi vya majeshi ya Uingereza. Moja kati ya malengo makuu ya serikali za Ulaya wakati wa kujiri Vita vya Kwanza vya Dunia ilikuwa kuugawa utawala wa Othmania, lengo ambalo baadaye lilifanikiwa. Wakati utawala wa Othmania ulipokuwa ukigawanywa, maeneo yaliyokuwa chini ya utawala huo, nayo moja baada ya jingine yalidhibitiwa na Ufaransa na Uingereza, ambapo mji wa Damascus katika Syria ya leo, pia ulishambuliwa na katika siku kama ya leo ukakaliwa kwa mabavu. Hata hivyo kwa mujibu wa makubaliano ya hapo kabla kati ya London na Paris, Syria ukiwemo mji mkuu wake, Damascus, ilidhibitiwa na Ufaransa. ***

Haram ya Bibi Zaynab (as) katika mji wa Damascus

 

Miaka 83 iliyopita katika siku kama ya leo, Ufaransa na Uingereza ziliitangazia vita Ujerumani na kwa utaratibu huo Vita Vikuu vya Pili vya Dunia vikaanza. Baada ya jeshi la Ujerumani kuishambulia Poland, serikali ya Uingereza iliitumia Ujerumani ujumbe ikiitaka iondoke haraka katika maeneo inayoyakalia kwa mabavu ya Poland. Hata hivyo Ujerumani ilipuuza takwa hilo la Uingereza. Baadaye Uingereza iliipatia Ujerumani makataa ya kuhitimisha operesheni zake za kijeshi. Hata hivyo Adolph Hitler kiongozi wa wakati huo wa Ujerumani ya Kinazi alikataa kutekeleza takwa hilo. Hatimaye katika siku kama ya leo, Uingereza na Ufaransa zikaitangazia vita Ujerumani. Sio Adolph Hitler pekee ambaye hakutaraji kama Ufaransa na Uingereza zingeingia vitani kwa ajili ya Poland bali hata Joseph Stalin kiongozi wa wakati huo wa Umoja wa Kisovieti pia hakutarajia hilo. ***

Vita vya Pili vya Dunia

 

Katika siku kama ya leo miaka 79 iliyopita, mkataba wa kusalimu amri Italia katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia ulitiwa saini baina ya wawakilishi wa Italia na nchi waitifaki. Kwa mujibu wa mkataba huo, Benito Mussolini Waziri Mkuu wa Italia alikubali bila masharti kusalimu amri nchi yake na kwa utaratibu huo, mmoja wa waitifaki muhimu wa Ujerumani ya Kinazi katika vita hivyo, akawa ameondoka katika medani ya vita. ***

Benito Mussolini

 

Siku kama ya leo miaka 51 iliyopita, nchi ya Qatar ilipata uhuru toka kwa mkoloni Mwingereza. Qatar iliwahi kudhibitiwa na Ufalme wa Othmania. Hata hivyo kufuatia kudhoofika utawala huo, Qatar ambayo kuanzia mwaka 1882 na kuendelea kivitendo ilikuwa ikiendeshwa na Uingereza, mwaka 1916 nchi hiyo ya Kiarabu ikawa imetambuliwa rasmi kuwa koloni la Muingereza. Hadi mwaka 1971 Qatar ilikuwa bado inakoloniwa na Uingereza ambapo mwaka huo huo, kwa ushirikiano wa viongozi wa eneo la pambizoni mwa kusini mwa Ghuba ya Uajemi, likaundwa Shirikisho la Umoja wa Falme za Kiarabu. Hata hivyo mnamo Septemba mwaka huo huo, yaani 1971, Qatar ilijiondoa katika Shirikisho la Umoja wa Falme za Kiarabu na kujitangazia uhuru. ***

Bendera ya Qatar

 

Na miaka 30 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia, aliaga dunia Dkt. Mahmoud Hesabi mwanafizikia mashuhuri wa Iran anayejulikana kama baba wa fizika ya kisasa ya Iran. Alizaliwa mwaka 1281 katika mji wa Tehran. Profesa Mahmoud Hesabi alikuwa na bidii kubwa masomoni na daima kuanzia masomo yake ya msingi hadi ya juu alikuwa akishika nafasi ya kwanza darasani. Sambamba na masomo shuleni, Mahmoud Hesabi alikuwa akijihusisha pia na kujifunza na kusoma dafina na hazina ya maarifa ya Kiislamu na Kiirani. Hakutoshoka na taaluma moja tu, bali alifanya hima ya kusoma fani mbalimbali. Alipofikisha umri wa miaka 17, Mahmoud Hesabi alikuwa tayari amefikia daraja za juu za masomo. Mbali na kuwa mahiri katika taaluma kama za uhandisi wa barabara, majengo, madini, umeme, fizikia na kadhalika, msomi huyu alikuwa amebobea pia katika lugha za kigeni zilizoenea duniani kama Kiarabu, Kiingereza, Kijerumani na Kifaransa. Profesa Mahmoud Hesabi aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 90 baada ya kuishi maisha yaliyojaa hima na juhudi za kielimu. ***

Dkt. Mahmoud Hesabi