Akhlaqi Katika Uislamu (1)
Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yako mpendwa msikilizaji popote pale ulipo wakati huu. Nakukaribisha kusikiliza sehemu hii ya kwanza ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu nikiwa na matumaini kuwa, mimi pamoja na wewe tutanufaika na yale tutakayoyasikia katika kipindi hiki. Endelea kuwa nami basi hadi tamati ya mazungumzo yetu.
Ni jambo lisilo na shaka mpendwa msikilizaji, kwamba kuijenga batini, yaani upande wa ndani wa nafsi ya mtu, kwa kuirekebisha na kuitakasa roho na nafsi yake kuna nafasi kuu katika saada, fanaka na ukamilifu wa mtu mwenyewe binafsi na wa jamii na pia katika upande wa kimaada na kimaanawi. Kiasi kwamba, hata kama mwanadamu atafikia kwenye vilele vya elimu zote na kuweza kuutiisha vyovyote apendavyo ulimwengu wote wa maumbile, lakini kama atashindwa kuzidhibiti nguvu haribifu za ndani ya nafsi yake, hatoweza kufikia kilele cha saada na ukamilifu wa kiutu. Ni kwa sababu hiyo, ndiyo maana ikiwa maendeleo yote ya kisayansi na kiufundi hayatoenda sambamba na utakasaji na ujengaji wa batini ya mwanadamu, huwa mithili ya kasri lililojengwa kwa barafu kisha likaanikwa juani! Kwa hiyo kumlea na kumjenga mwanadamu kiroho na kitabia ni jambo la lazima na lenye umuhimu mkubwa mno kwa jamii yoyote ile na katika kila zama na wakati.

Kwa masikitiko inabidi tuseme kuwa, katika dunia yetu hii ya leo inayoonekana ya kisasa na iliyopiga hatua kubwa mno kimaendeleo, si tu hazichukuliwi hatua zozote za kuyapa uzito mafunzo ya kiutu na kiakhlaqi, lakini inavyoonekana, ni kama kwamba mwanadamu tayari ameshatimiza ndoto zake za kufikia ukamilifu wa yote aliyokuwa akitamani na kuyataraji. Wakati mwanadamu wa zama hizi, anayeonekana kuwa amestaarabika, ameshindwa vibaya sana katika suala la kuidhibiti nafsi yake pamoja na changamoto za hawaa na matamanio ya nafsi, bado hajawa tayari kukiri suala hilo, utadhani hakuna maafa yoyote yale yaliyomfika. Lakini hebu tujiulize, ni mtu gani mwenye akili timamu na mwenye insafu, ambaye hawezi kutiwa wasiwasi na hali ya kutisha na kusikitisha ya kushamiri ufuska na maingiliano haramu ya kingono, vitendo vya ubakaji na vya kishenzi, upotokaji wa tabia, ubaguzi, dhulma na uonevu pamoja na uporomokaji wa misingi ya kiakhlaqi na kiutu tunaoshuhudia duniani leo?
Katika baadhi ya jamii za kisasa zinazoonekana kuwa zimeendelea za madola ya watumiaji mabavu, ustaarabu hauna tafsiri nyingine zaidi ya unyang'anyi, uporaji, jinai na mauaji ya watu wa mataifa manyonge na kunyamazisha mbiu yoyote ya kupigania haki na uadilifu. Isitoshe, ukubwa wa mporomoko wa kiakhlaqi na kiutu, haujakomea tu kwenye ongezeko linaloshuhudiwa kila leo la dhulma na jinai zinazofanywa na wenye nguvu dhidi ya haki za mataifa madhulumu na manyonge duniani, lakini hata ndani kabisa ya nchi hizo zinazoonekana kuwa zimeendelea, kufa kwa thamani za kiakhlaqi kumesababisha maafa makubwa kwa mtu binafsi na jamii, kiasi cha kuiporomosha hadhi na thamani ya wanadamu katika zama hizi.
Kutozipa uzito thamani za kiakhlaqi hakuhusiani na ulimwengu wa Magharibi pekee, bali kwa masikitiko, katika baadhi ya mataifa ya Kiislamu, nako pia thamani za kiakhlaqi zimefifia pia na hakuna hali ya kuridhisha ya kuonyesha kuwa watu wanashikamana na maadili ya akhlaqi njema. Huko nyuma jamii ya Kiislamu ilipokuwa ikikabiliana na upotokaji wa kimaadili wa Ulimwengu wa Magharibi ilikuwa ikitumia kaulimbiu "Kwanza maadili yetu, kisha ustaarabu wao"; kaulimbiu ambayo inabainisha risala na ujumbe mzito uliobebwa na Ulimwengu wa Kiislamu, ambao kwa mujibu wa Qur'ani ni wa sisi kuwa mashuhuda na kigezo kwa wengine katika tabia na matendo yetu. Na maana yake ni kwamba, tunatakiwa tuuonyeshe ulimwengu na kudhihirisha vile namna hasa zilivyo, thamani za kiakhlaqi katika matendo yetu. Kwa hiyo kila Muislamu ana jukumu na masuulia mazito ya kufanya juhudi za kuhuisha tena thamani za kiakhlaqi na kiutu za dini ya Uislamu.

Hatua ya mwanzo, ambayo mimi na wewe mpendwa msikilizaji tunapaswa kuichukua katika safari hii ya kufikia lengo hilo ni kuupa umuhimu mkubwa msingi muhimu sana na wenye nafasi kuu wa "kuitambua nafsi". Mwanadamu ni mithili ya bango zuri na lenye thamani kubwa la mchoro, ambalo tunapaswa kuzitambua nakshi na mistari iliyotumika kulifanya liwe na thamani hiyo. Ni kwa kuyaelewa hayo tu ndipo tutaweza kujitahidi kwa uwezo wetu wote kulitunza na kulihifadhi ili lisije likaingia doa lolote. Hapa sasa ni mahali pa kujiuliza suali hili; ni zipi hizo sifa maalumu na za kipekee za bango hilo lenye thamani kubwa la kiumbe mwanadamu?
Mwenyezi Mungu Muumba aliyetukuka wa ulimwengu analizungumzia hivi katika sura ya 95 ya Attin: "Kwa Jina la Mwenyeezi Mungu Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu. Naapa kwa tini na zaituni! Na kwa Mlima wa Sinai! Na kwa mji huu wenye amani! Bila ya shaka tumemuumba mtu kwa umbo lilio bora kabisa."
Kuhusu maana ya Ahsani Taqwiim, baadhi ya wafasiri wa Qur’ani wamesema: Maana yake ni kwamba, Mwenyezi Mungu amemuumba mtu kwa mlingano kamili katika hali zake zote, iwe ni ya kimwili au kiroho na kiakili. Kwa maneno mengine ni kwamba, Mwenyezi Mungu Mtukufu ameweka kwenye maumbile ya mtu kila aina ya kipawa na uwezo ili kumwezesha kufika kwenye vilele vya kila aina ya ukamilifu.
Lakini mbali na hayo, na ili kuutilia mkazo zaidi ukweli na uhakika huo, Muumba wa ulimwengu ameuelezea ubora wa mwanadamu na jinsi alivyofadhilishwa na Yeye Mola kama aya ya 70 ya Suratul-Israa inavyosema: "Na hakika tumewatukuza wanaadamu, na tumewapa vya kupanda nchi kavu na baharini, na tumewaruzuku vitu vizuri vizuri, na tumewafadhilisha kwa fadhila kubwa kuliko wengi miongoni mwa tulio waumba."

Sifa nyingine maalumu ya uumbwaji wa mwanadamu ni kupuliziwa roho ya Mola baada ya kukamilika umbo lake katika hali zote za uumbwaji. Aya ya 7 hadi ya 9 ya Suratu-Sajdah inaielezea hali hiyo hivi: "Ambaye ametengeneza vizuri umbo la kila kitu; na akaanzisha kumuumba mtu kwa udongo. Na kisha akajaalia uzao wake utokane na kizazi cha maji madhaifu. Kisha akamtengeneza, na akampulizia roho yake, na akakujaalieni kusikia na kuona, na nyoyo za kufahamu. Ni uchache mnavyo shukuru."
Kwa mujibu wa aya hizi, hakika ya mwanadamu, mbali na upande wake wa kimwili na kimaada, unaofanana na viumbe wengine wote, ana upande wa kimalakuti na kiungu unaomfanya awe bora zaidi kuliko viumbe vingine vyote vilivyomo katika ulimwengu wa viumbe. Upande huo ni wa roho inayotokana na irada ya Mwenyezi Mungu, na ndio maana roho hiyo ni kitu kinachobakia milele na kisichoweza kutoweka. Ni kinyume na ulivyo mwili wa mtu, ambao baada ya kupita muda huwa unachakaa na hatimaye kuoza na kupotea. Mpendwa msikilizaji tusite hapa kwa leo, lakini tutakuja kuifafanua zaidi nukta hii katika kipindi chetu kijacho inshaallah. Ahsante na kwaheri…/