Alkhamisi tarehe 22 Septemba 2022
Leo ni Alkhamisi tarehe 25 Safar 1444 Hijria sawa na 22 Septemba 2022.
Siku kama ya leo miaka 1685 iliyopita, yaani sawa na tarehe 22 Septemba mwaka 337, vilianza vita vya miaka 13 kati ya Iran na Roma katika utawala wa Shapur II (Dhul Aktaf), wa silsila ya watawala wa Sasani na ambavyo katika historia vilifahamika kama vita vya duru ya kwanza. Vita vya duru ya pili vilianza mwaka 359, ambapo katika duru zote, Wairani waliibuka na ushindi. Katika duru ya kwanza ambapo vita hivyo vilidumu hadi mwaka 350, Waroma walipoteza kila kitu walichokuwa wakikidhibiti eneo la mashariki mwa Bahari ya Mediterranean, na mfalme wao aliuawa katika duru ya pili ya vita hivyo.
Siku kama ya leo miaka 194 iliyopita yaani tarehe 22 Septemba mwaka 1828, Shaka Zulu kiongozi na muasisi wa utawala wa Kifalme wa Zulu nchini Afrika Kusini aliuawa na ndugu zake wawili wa kambo. Shaka aliliongoza kabila kubwa la Zulu tangu mwaka 1815 na katika kipindi kifupi aliweza kuyaweka chini ya uongozi wake maeneo mengi ya Afrika Kusini. Baada ya kuuawa Shaka, kaka yake mmoja alichukua hatamu za uongozi na kuanzia mwaka 1830 hadi 1839 akapigana na wahamiaji wa Kiholanzi waliojulikana kama Boers. Hatimaye serikali ya Shaka ilipata pigo kutoka kwa Uingereza mwaka 1880 na kugawanyika katika serikali kadhaa zisizo na mamlaka kamili.
Katika siku kama ya leo miaka 114 iliyopita, nchi ya Bulgaria ilijipatia uhuru kutoka kwa utawala wa Othmania. Bulgaria ilianza kutawaliwa na utawala huo mwishoni mwa karne ya 14. Wakati huo maudhi dhidi ya Wakristo yalianza na kuendelea kwa karibu miaka 500 ya udhibiti wa Othmania kwenye nchi hiyo na suala hilo liliibua uasi wa mara kwa mara wa raia wa Bulgaria. Hatimaye mwaka 1878 nchi hiyo ilipata uhuru na kujitangazia mamlaka ya ndani. Tarehe 22 Septemba mwaka 1908 mfalme wa wakati huo wa Bulgaria alitangaza uhuru kamili wa nch hiyo.
Siku kama ya leo miaka 62 iliyopita, nchi ya Mali iliyo kaskazini magharibi mwa Afrika ilipatia uhuru. Karibu miaka elfu mbili iliyopita nchi ya Mali ilikuwa na utamaduni mkubwa na uliong'ara. Hata hivyo nchi hiyo tangu karne ya 18 hadi ya 19 Miladia ilikuwa moja ya tawala za ufalme wa Sudan. Baada ya Morocco kutwaa baadhi ya maeneo yaliyokuwa chini ya tawala za ufalme wa Sudan ikiwemo Mali, tawala mbalimbali za kikabila nchini Mali zilifanikiwa kuingia madarakani. Satwa ya Wafaransa nchini Mali ilianza mnamo karne ya 19 na hadi kufikia mwaka 1898 nchi hiyo ilikuwa chini ya usimamizi wa Ufaransa. Hata hivyo Mali ambayo ilikuwa ikiitwa Sudan ya Ufaransa, mwaka 1958 ilianza kujitawala na mwaka 1960 ikajipatia uhuru wake kamili.
Siku kama ya leo miaka 42 iliyopita, majeshi ya dikteta wa zamani wa Iraq Saddam Hussein yalianza kufanya mashambulio makubwa ya anga na nchi kavu dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na hivyo vita vya miaka minane vya kulazimishwa vya Iraq dhidi ya Iran vikawa vimeanza. Jeshi la Iraq lilikuwa limefanya uvamizi na mashambulizi kadhaa katika maeneo ya mpakani ya Iran miezi kadhaa nyuma. Magari ya deraya na vikosi 12 vya jeshi la nchi kavu la Iraq viliyashambulia maeneo ya mipaka ya kusini magharibi mwa Iran. Mapambano makali ya wananchi wa Iran yaliwalazimisha askari wa Saddam kurejea nyuma hadi kwenye mipaka inayotambulika kimataifa.