Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (55)
Ni wasaa na wakati mwingine tunapokutana tena wapenzi wasikilizaji katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu ili kwa pamoja tuweze kufungua ukurasa mwingine katika kurasa za historia ya Maulamaa na wanazuoni wa Kishia pamoja na mchango wao katika Uislamu.
Kipindi chetu kilichopita kilitupia jicho maisha ya Ayatullah Sheikh Muhammad Taqi Baraghani mmoja wa wanazuoni wakubwa aliyeishi katika karne ya 13 Hijria. Tulisema kuwa, Mulla Muhammad Taqi Baraghani alizaliwa mwaka 1172 Hijria katika kijiji cha Baraghan Taleghan Iran. Aidha tulibainisha kwamba, miongoni mwa vitabu vyake ni "Majalis al-Mutaqin", "Uyun al-Usul", na "Manhaj al-Ijtihad". Kipindi chetu cha wiki hii ambacho ni sehemu ya 55 ya mfululizo huu, kitatupia jicho historia na maisha ya Muhammad Sharif Mazandari mashuhuri kwa lakabu ya Sharif al-Ulamaa Mazandarani. Jiungeni nami hadi mwisho wa dakika hizi chache za kipindi hiki.
Sharif al-Ulamaa ambaye jina lake kamili ni Muhammad Sharif bin Hassan Ali Amoli Mazandarani Hairi alizaliwa takribani mwaka 1200 Hijria katika mji wa Karbala Iraq. Baba yake ni Mullah Hassan Ali Amoli aliyekuwa mmoja wa wanazuoni wachamungu katika zama zake ambaye asili yake ilikuwa mji wa Mazandaran wa kaskazini mwa Iran aliyehajiri kwa ajili ya masomo na kutafuta elimu na kwenda kuishi katika mji wa Karbala kando ya Haram ya Imam Hussein bin Ali (as), ambaye ni mmoja wa wajukuu mashuhuri wa Bwana Mtume (saw). Muhammad Sharif alisoma masomo ya awali na ya msingi kwa baba yake huko Karbala na baada ya hapo akaanza kuhudhuria darsa za Sayyid Muhammad Mujahid na Sayyid Ali Tabatabai na kukamilisha masomo yake kwa walimu na wanazuoni hao.
Kutokana na kiu kali ya elimu aliyokuwa nayo akiwa pamoja na baba yake alifanya safari katika Hawza na vyuo mbalimbali vya kidini Iraq na Iran lengo likiwa na kunufaika na elimu ya wasomi na walimu watajika wa zama hizo.
Kwa msingi huo alifanya safari katika miji ya Najaf, Baghdad, Mash'had, Qum na Tehran na wakati mwingine akibakia katika baadhi ya miji hiyo kwa miezi kadhaa akisoma na kustafaidi na elimu ya wanazuoni wa miji hiyo.
Safari zake zilifikia tamati kwa kuutembelea mji wa Mash'had ilipo Haram ya Imam Ali bin Mussa Ridha (as) ambapo baada ya kufanya ziara alirejea tena katika mji wa Karbala huko Iraq. Baada ya safari ndefu ya kutafuta elimu, Muhammad Sharif Mazandarani alitulia na kuanza kufundisha. Haukupita muda ambapo kulianza kushuhudiwa wimbi kubwa la watu wenye kiu ya elimu likimuelekea mwanazuoni huyo kwa ajili ya kunufaika na bahari ya elimu yake.
Kwa mujibu wa wana historia ni kuwa, idadi ya wanafunzi wake ilifikia elfu moja. Katika zama za Mulla Muhammad Sharif Mazandarani, Chuo Kikuu cha Kiislamu (Hawza) cha Karbala kilikuwa katika kilele cha ustawi na kunawiri kielimu ambapo wasomi na wanazuoni wakubwa kama Sheikh Ansari, Fadhil Darbandi na makumi ya Mamujitahidi wengine wamemeleka katika darsa na masomo ya alimu huyo. Pamoja na hayo, alimu huyo aliendelea kusoma kwa mwalimu wake yaani Sayyid Ali na daima alikuwa akijitambua kama mtu ambaye bado anahitaji kusoma na kujifunza.
Kutambulika kwake kuwa mtu aliyebobea katika elimu na maarifa kulitokana na umahiri na ustadi wake mkubwa aliokuwa nao katika maudhui mbalimbali za fikihi, nguvu na uwezo wake mkubwa wa kufahamu masuala ya kielimu, kunyambua hukumu pamoja na nguvu kubwa na isiyo na mithili ya kuhifadhi mambo aliyokuwa nayo. Alitambulika miongoni mwa Marajii wa zama zake kuwa msomi wa aina yake. Hali hiyo ilimfanya apewe lakabu ya Sharif al-Ulamaa.
Kipaji hicho ambacho ni tunu kutoka kwa Mwenyezi Muungu sambamba na hima na bidii kubwa isiyo na kikomo ya Sharif al-Ulamaa ni mambo ambayo kwa hakika yalimfanya aondokee kuwa msomi na mwanazuoni mahiri na mtajika. Katika mahusiano yake na Mwenyezi Mungu alitambulika na kusifika pia kwa ibada na unyenyekevu wa hali ya juu sambamba na kujipamba kwake na sifa za kiumini na kiuja. Hatimaye hima na idili aliyokuwa nayo katika elimu vilimfanya afanikiwe kuasisi fikihi na usuli ya kisasa akitumia Kitabu cha Mwenyezi Mungu, Sunna za Bwana Mtume (saww), Akili na Ijimaa (makubaliano ya wanazuoni).
Sifa nyingine maalumu na ya kipekee ya Mulla Muhammad Sharif Mazandarani ni uwezo wake mkubwa na wa kustaajabisha katika midahalo na uzungumzaji wake mzuri na wa kuvutia. Alikuwa na ubobezi na uwezo usio na mithili katika elimu za fikihi, hadithi na elimu nyingne za kidini.
Nyaraka za histora zinaonyesha kuwa, alikuwa mahiri pia katika kujibu maswali na shubha mbalimbali katika vikao vya kielimu au katika uga wa kijamii. Kwa mujibu wa ushuhuda wa wana historia ni kuwa, hakuna msomi au mwanazuoni aliyekuja kufanya mdahalo na alimu huyu isipokuwa alishindwa. Hatimaye baada ya kuishi na kufanya hima kubwa katika kueneza mafundisho ya dini sambamba na kulea mamia ya Mamujitahidi wa Kishia, Sharif al-Ulamaa Mazandarani aliaga dunia mwaka 1245 Hijria. Katika zama hizo ugonjwa wa tauni ulikuwa umeenea katika mji wa Karbala na miji yote ya kando kando na mji huo nchini Iraq. Mke na watoto wake wawili pia waliaga dunia kwa maradhi hayo. Baada ya kuaga dunia alizikwa katika eneo la chini kwa chini la nyumba yake baada ya kuagwa kwa hamasa na Mashia katika mji wa Karbala.
Tunakamilisha kipindi chetu cha leo kwa kukunukulieni hadithi kutoka kwa Bwana Mtume (saw) inayobainisha umuhimu, fadhila na ubora wa Maulamaa ambapo mbora huyo wa viumbe anawataja Maulamaa kama taa inayomulikia ardhi na kwamba ni warithi wa Mitume.
Amirul-Muuminina Ali bin Abi Twalib (as) pia ameusia na kukokoteza mno suala la kuketi pamoja na Maulamaa ambapo Imam huyo wa mashariki na magharibi amenukuliwa akisema:
Keti na Maulamaa ili elimu yako iongezeke, adabu yako iwe njema na roho yako iwe safi.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh