Akhlaqi Katika Uislamu (2)
Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yako mpendwa msikilizaji popote pale ulipo wakati huu. Nakukaribisha kusikiliza sehemu hii ya pili ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu nikiwa na matumaini kuwa, mimi pamoja na wewe tutanufaika na yale tutakayoyasikia katika kipindi hiki. Endelea kuwa nami basi hadi tamati ya mazungumzo yetu.
Katika kipindi kilichopita tulieleza kwamba hatua ya kwanza ya “mtu kuijua nafsi yake” ni kuelewa sifa muhimu na za kipekee ambazo Mola Muumba amelipamba kwazo bango la mchoro, wa nakshi za nafsi ya mwanadamu. Kuhusiana na sifa ya kwanza tulisema, Mwenyezi Mungu, Muumba wa ulimwengu amemuumba mtu kwa kumjaalia umbo jamili, lenye ukadirifu na mlingano kamili katika hali zake zote, kisha akampulizia roho yake. Akamfanya ni mwenye asili iliyotukuka ili kubainisha hakika kwamba, mwanadamu si kiumbe anayetokana na udongo tu bali thamani na utukufu wake umefungamana na hali ya kimalakuti na kiungu aliyojaaliwa. Kwa maneno mengine ni kuwa, mwanadamu ana sura na sira. Wahakiki wa akhlaqi katika Uislamu wanayaeleza maumbile ya kimwili ya mtu kama hali ya “dhahiri” ya kiumbe huyo; na wanaitaja hali ya ndani ya maumbile hayo kama “sira” na “khulka” yake, ambapo katika kuitathmini hadhi yake, wanasema, shakhsia halisi na ya kudumu ya mtu imefungamana na khulka na tabia yake, kwa sababu si hasha watu wengi wanaoonekana kuwa na sura jamili na dhahiri za kupendeza, wakwa hawana thamani yoyote ya kiutu kutokana na kutokuwa na maadili ya akhlaqi za kibinadamu; na kinyume chake, wale wasio na dhahiri zenye kupendeza wakawa na hadhi na daraja ya juu kutokana na kupambika kwao kwa sifa na khulka njema za tabia na akhlaqi.

Kwa masikitiko mpendwa msikilizaji, katika zama zetu hizi za mawasiliano na maendeleo ya kustaajabisha, yaongezekayo kila uchao ya sayansi na teknolojia, hakuna kitu kinachopewa thamani zaidi kama sura na dhahiri ya mtu, wakati uzuri wa tabia na wa kimaanawi, ambao ndio unaojenga shakhsia na asili yake, havipewi thamani inayotakiwa. Na kwa sababu hiyo, ndio maana katika karne ya sasa thamani za kiutu na kiakhlaqi zinazidi kufifia siku baada ya siku; na hapana shaka kuwa, bila mwanadamu kuchukua hatua ya kulirekebisha hilo, hatoweza kuishi kwa utulivu hata kama atalala na kuamka ndani ya majumba marefu ya ghorofa na kujistarehesha na kila aina ya suhula za maisha ya kisasa. Kwa kuacha kufanya hivyo tu, mwanadamu anaporomoka kutoka kwenye hadhi tukufu ya “Khalifa”, yaani mfuwatizi wa Mwenyezi Mungu ulimwenguni, ambayo ni moja ya sifa kuu zinazosarifu bango la nakshi zilizopamba nafsi yake. Ni hadhi hiyo iliyotukuka, ambayo kwa mujibu wa aya ya 30 hadi 34 za Suratul Baqarah, iliwafanya malaika waliojikurubisha kwa Allah waporomoke chini kumsujudia kwa amri yake Yeye Mola, khalifa wa huyo wa ardhini. Qur’ani tukufu inalisimulia tukio hilo kama ifuatavyo:
Na pale Mola wako Mlezi alipo waambia Malaika: Mimi nitamweka katika ardhi Khalifa (mfwatizi), wakasema: Utaweka humo atakaye fanya uharibifu humo na kumwaga damu, hali sisi tunakutakasa kwa sifa zako na tunakutaja kwa utakatifu wako? Akasema: Hakika Mimi nayajua msiyo yajua. Na akamfundisha Adam majina ya vitu vyote, kisha akaviweka mbele ya Malaika, na akasema: Niambieni majina ya hivi, ikiwa mnasema kweli. Wakasema: Subhanaka, Wewe umetakasika! Hatuna ujuzi isipokuwa kwa uliyo tufunza Wewe. Hakika Wewe ndiye Mjuzi Mwenye hikima. Akasema: Ewe Adam! Waambie majina yake. Basi alipo waambia majina yake alisema: Sikukwambieni kwamba Mimi ninajua siri za mbinguni na za duniani, na ninayajua mnayo yadhihirisha na mliyo kuwa mnayaficha? Na tulipo waambia Malaika: Msujudieni Adam, wakamsujudia wote isipo kuwa Iblis, alikataa na akajivuna na akawa katika makafiri.
Irada hiyo ya Mwenyezi Mungu kuhusiana na hadhi hii ya ukhalifa imefanyika katika uumbaji wa mwanadamu peke yake, na inahusiana na kiumbe huyo tu. Kama ni hivyo, inalaiki kweli kwa mwanadamu kuiporomosha nafsi yake kwa kuifanya hadhi hiyo aliyotukuzwa nayo, mhanga wa sifa chafu za kiakhlaqi, ufuska, hawaa na matamanio ya kupita ya nafsi kwa vitu vya kimaada? Au ni kinyume chake; yaani, inampasa mwanadamu ajitahidi kufanya kila lililo kwenye uwezo wake, kwa kuchunga thamani aali na tukufu za kiutu na kiakhlaqi, kwa ajili ya kuitunza hadhi na amana hiyo na kutoruhusu hata chembe ndogo ya doa ichafue at’iya na hidaya hiyo adhimu ya hadhi tukufu aliyotunukiwa na Mwenyezi Mungu?
Lakini mbali na sifa mbili hizi maalumu, yaani kupuliziwa mwanadamu roho ya Mwenyezi Mungu na kupewa hadhi ya juu na tukufu ya kuwa Khalifa na mfwatizi wake hapa ardhini, ambavyo vinang’arisha bango la maumbile ya mwanadamu na kulifanya liwe na thamani nyingi sana, nakshi nyingine muhimu iliyomo kwenye ujudi wa kiumbe huyo ni fitra na hali ya maumbile ya kutaka kumjua na kumuelekea Mwenyezi Mungu. Kwa maneno mengine ni kwamba, katika asili yake, mwanadamu ameumbwa kwa namna ambayo, imani safi ya tauhidi, ya kuwepo Mola mmoja pekee wa kumtegemea, inaandamana naye kila wakati, katika milima na mabonde na kila anapotingwa na kila dhiki na misukosuko katika maisha yake.

Lakini pia tusiache kutanabahisha hapa kwamba, sababu na athari za kifamilia, kijamii, kiutamaduni, kiuchumi, kisiasa na hata kijeshi zinaweza zikawa mithili ya vumbi lenye kutanda juu ya kioo safi cha maumbile hayo ya mwanadamu, lakini haziwezi katu kubadilisha kikamilifu fitra ya tauhidi iliyojengwa ndani ya nafsi ya kiumbe huyo. Kuliko wakati wowote ule, hakika hii hujitokeza, pale mwanadamu anapofikwa na masaibu mazito ya kumkatisha tamaa, ya kupata msaada wa mtu au kitu chochote kile; na ndipo anapomuelekea na kumuomba Mwenyezi Mungu. Kwa hiyo maumbile ya kumtambua Mwenyezi Mungu, ni kitu kingine muhimu na athirifu, ambacho kama mwanadamu atakitumia kunadhimu tabia na milahaka yake ya binafsi na ya kijamii, na kuifanya kuwa dira yake, itamwezesha kila wakati kushikamana na misingi ya thamani za kiutu na kiakhlaqi na katu hatovutwa na kutekwa na mambo potofu yaliyo dhidi ya thamani hizo.
Mpendwa msikilizaji sehemu ya pili ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu imefikia tamati. Hivyo sina budi kukuaga hadi wakati mwingine inshallah, tutakapokutana tena katika sehemu ya tatu ya kipindi hiki. Namuomba Mola akubariki; na amani yake iendelee kuwa juu yako…/