Nov 06, 2022 05:44 UTC
  • Akhlaqi Katika Uislamu (4)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yako mpendwa msikilizaji popote pale ulipo wakati huu. Nakukaribisha kusikiliza sehemu hii ya nne ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu nikiwa na matumaini kuwa, mimi pamoja na wewe tutanufaika na yale tutakayoyasikia katika kipindi hiki. Endelea kuwa nami basi hadi tamati ya mazungumzo yetu ya leo ambapo tutaangazia sifa nyingine maalum za akhlaqi katika Uislamu.

Katika vipindi vilivyopita tulieleza kwamba, kwa mujibu wa mafundisho ya dini, hatua ya kwanza kuelekea kwenye lengo la kupambika kwa sifa njema za kiakhlaqi na kujiweka mbali na hulka chafu ni mtu "kuitambua nafsi yake". Tukaitolea ufafanuzi nukta hiyo ya msingi kwa aya za Qur'ani, ambayo ni utangulizi wa "kumjua Mwenyezi Mungu" na tukaona kwamba, katika mfumo wa ulimwengu, mwanadamu ni kiumbe aliyepewa hadhi maalum na ya juu. Kupulizwa roho ya Mwenyezi Mungu katika uumbaji wa mwanadamu, kutukuzwa, kuumbwa katika umbo la kadiri na mlingano, kutunukiwa nguvu adhimu ya akili, kutiishiwa vilivyomo mbinguni na ardhini, kuletewa Mitume na kuteremshiwa vitabu vya mbinguni kwa ajili ya uongofu na kuufikia ukamilifu, yote hayo yanadhihirisha kuwa Mola Mwenye Enzi amemuumba mwanadamu kwa lengo maalum; na kwamba kiumbe huyo anao uwezo wa kufikia kilele cha utukufu wa kumkurubisha kwa Mola wake. Na sababu ni kwamba, dhihirisho jumuishi zaidi, lililokamilika zaidi, na lililotukuka zaidi la thamani za kiakhlaqi, limeipamba dhati iliyotakasika ya Mwenyezi Mungu, ambayo imekamilika kwa sifa zote jamili na zilizotukuka. Yeye ni Mola mwenye upeo usio na kikomo wa uzuri na anayapenda yaliyo mazuri. Na hiyo ndiyo sababu ya sisi kutakiwa tujipambe kwa sifa zisizo na kifani za akhlaqi njema alizopambika nazo Yeye Mola wetu. Ukweli ni kwamba, "kuitambua nafsi" ni daraja la kutuunganisha sisi na "kumtambua Mwenyezi Mungu". Kwa hivyo tujitahidini ili tuwe dhihirisho la sifa bora za kiakhlaqi za Mola wa walimwengu.

Kuitambua mtu nafsi yake ni utangulizi wa kumjua Mola wake

 

Kutokana na hayo, kuna nukta kadhaa muhimu na za msingi ambazo inapasa tuzizingatie. Mojawapo ya nukta hizo ni kwamba, katika chuo maalum cha akhlaqi cha Uislamu inatakiwa matendo yote anayofanya mtu, yawe na sura, nia na madhumuni ya kidini ya kutaka radhi za Mwenyezi Mungu; na si kwa lengo la kujitafutia umaarufu, kujifaharisha, kutafuta maslahi ya binafsi au kujionyesha kwa sababu za kibinafsi, kijamii, kiutaifa na kisiasa. Imam Jaafar Sadiq (as) amesema: “Mtu anayependa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na anayeghadhibika kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, na akawa na uadui (na mtu) kwa sababu ya Mwenyezi Mungu na akatoa (alichonacho) kuwapa wengine kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, huyo ni miongoni mwa watu ambao imani yake imekamilika.”

Ikiwa tabia na mwenendo wetu wa kiakhlaqi utaendana na nia na imani ya tawhidi, si tu haitakuwa na ila wala kasoro yoyote kutokana na kujielekeza kikamilifu kwa Mwenyezi Mungu ambaye ni dhihirisho la ukamilifu usio na ukomo; lakini pia hatutajenga dhana ya kujiwekea mpaka na kikomo katika suala la kujijenga kwa thamani za kiakhlaqi; badala yake tutakuwa muda wote tunapigania kufikia kilele cha sifa za akhlaqi njema pa sina kutosheka na hatua au marhala yoyote ile tutakayoifikia. Kuhusiana na hilo, Mwenyezi Mungu Mtukufu amemfanya Bwana Mtume SAW kuwa ruwaza na kigezo cha daraja ya juu kabisa cha kuigwa cha akhlaqi njema alipomhutubu katika katika aya ya 4 ya Suratul Qalam kwa kumwambia: Na hakika wewe una tabia tukufu.

 

Imam Sajjad (as), ambaye amelelewa na kukulia kwenye ukoo na kitovu cha Utume, ametubainishia sira na mwongozo huo katika sehemu ya kwanza ya dua yake maarufu ya Makaarimul-Akhlaq aliposema: Ewe Mola Mwenye Enzi, mteremshie rehma na amani Muhammad na Aali zake na uifikishe imani yangu kwenye ukamilifu wa juu kabisa wa imani, na yakini yangu, kwenye daraja ya juu kabisa ya yakini na uifanye nia yangu nia iliyo njema zaidi, na uzielekeze amali zangu kwenye bora ya amali. Katika sehemu nyingine ya dua hiyo hiyo, mtukufu huyo anamwomba Mwenyezi Mungu akisema: ”Nijaalie kuwa na thamani za juu na zilizotukuka zaidi za akhlaqi njema.”

Hapana shaka kwamba, hakuna chuo chochote cha fikra za kiakhlaqi duniani chenye mtazamo na mueleko kama huu wa Uislamu wa kiu ya kufikia kwenye ukamilifu wa akhlaqi njema. Kwa sababu, kutokuwapo na ukomo ni katika sifa maalum za mtazamo wa kitawhidi kuhusu ulimwengu, ambao unamuonyesha mwanadamu muelekeo huo kwa kumwambia kama isemavyo aya ya 6 ya Suratul-Inshiqaq:  Ewe mtu! Hakika wewe unajikusuru kwa juhudi kumwendea Mola wako Mlezi, basi utamkuta.

Lakini mbali na msingi huu, suala la kushikamana na akhlaqi njema huwa na thamani linapokuwa endelevu na likawa limejikita na kurasimika ndani ya nafsi ya mtu; na si kuwa jambo la kupita na la muda maalum. Na ndiyo kusema kwamba, akhlaqi za kimaonyesho na za mambo ya kupita hazina hadhi wala thamani yoyote katika mwongozo wa akhlaqi wa Uislamu; na njia pekee ya kujiokoa na madhara hayo na kuzifanya sifa za kiakhlaqi zijikite na kurasimika ndani ya nafsi ya mtu ni kulifungamanisha suala hilo na Mwenyezi Mungu Mtukufu ambaye sifa zake za akhlaqi, za dhati yake zenye nuru ya uhai, zinadhihirika na kutawala daima, kila wakati na kila mahala.

 

Nukta ya mwisho ya kuhitimishia mazungumzo yetu ya leo ni kwamba, ili kuweza kujengeka na kupambika na akhlaqi njema inalazimu kuwepo na mwega imara na wa uhakika utakaokuwa chachu ya kutoa msukumo mkubwa kwa mtu na jamii wa kushikamana na thamani za akhlaqi njema. Tajiriba imeonyesha kuwa hakuna kitu chochote chenye dhamana ya utekelezaji wa kumfanya mtu na jamii ziheshimu misingi ya akhlaqi kama imani juu ya Mwenyezi Mungu, ambaye ni mshuhudiaji na mdhibiti wa mienendo na matendo yetu yote tuyafanyayo hadharani na faraghani. Ni Yeye Mola ambaye amewahutubu waja wake katika aya ya 105 ya Suratu-Tawbah kupitia kinywa cha Mtume wake kwa kuwaambia:  Na sema: Tendeni vitendo. Na Mwenyezi Mungu, na Mtume wake, na Waumini wataviona vitendo vyenu. Na mtarudishwa kwa Mwenye kujua siri na dhaahiri; naye atakuambieni mliyo kuwa mkiyatenda.

Kwa hivyo tuelewe kwamba, mbali na taathira za duniani, matendo yetu ya kiakhlaqi yatakuwa na malipo pia huko akhera, yatakapotathminiwa na kuhesabiwa katika ulimwengu huo wa baada ya kifo. Sifa mbili hizi maalum za imani juu ya Allah na imani juu ya kufufuliwa ndizo zinazokipambanua chuo cha fikra za kiakhlaqi cha Uislamu na kukifanya kiwe bora na cha kipekee kuliko vyuo vingine vyote vya fikra za kiakhlaqi duniani.

 Mpendwa msikilizaji sehemu ya nne ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu imefikia tamati. Hivyo sina budi kukuaga hadi wakati mwingine inshallah, tutakapokutana tena katika sehemu ya tano ya kipindi hiki. Namuomba Mola wa haki akubariki; na amani, rehma na baraka zake ziendelee kuwa juu yako…/