Nov 06, 2022 07:32 UTC
  • Akhlaqi Katika Uislamu (5)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yako mpendwa msikilizaji popote pale ulipo wakati huu. Nakukaribisha kusikiliza sehemu hii ya tano ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu ambapo katika mwendelezo wa mada ya kipindi chetu kilichopita, leo pia tutazungumzia sifa nyingine maalumu za akhlaqi za Kiislamu, nikiwa na matumaini kuwa tutaweza kushikamana nazo katika hali zote tulizonazo, za shida na raha na huzuni na furaha katika maisha yetu.

Mpendwa msikilizaji, naamini utakubaliana nami kuwa, hata kama sifa na majina yote ya Mwenyezi Mungu, ambayo yanatokana na chemchemi moja ya dhati yake isiyobadilika, ni mazuri mno na ni mwongozo unaomuelekeza mja kwenye ukamilifu, lakini tunaweza pengine kusema kwamba, inayotoa mguso mkubwa zaidi ya zingine kwenye nukta kuu ya mjumuiko huo adhimu wa majina na sifa hizo tukufu, ni sifa ya rehma zisizo na ukomo za Mola aliyetukuka. Sababu ni kwamba, sura 113 za Quráni tukufu zimeanza kwa kutaja sifa mbili tukufu za rehma, yaani “Rahman na Rahiim”. Zaidi ya hayo, rehma za Mwenyezi Mungu zimezungumziwa mara 104 katika aya za Quráni, ambayo ni ishara ya nafasi na umuhimu wake katika utamaduni wa kumjenga mwanadamu, wa kitabu cha mbinguni cha Quráni. Rehma zinatoka kwa Mwenyezi Mungu, ambaye ni Mfalme Mtawala na Mola Muumba halisi katika ulimwengu wa maumbile, ambaye ni mwenye ni uwezo na ukwasi mutlaki usio na kikomo. Quráni tukufu imeyazungumzia hayo kama ifuatavyo katika aya ya 65 na 66 za Suratu-Sáad: Sema: Hakika mimi ni mwonyaji tu; na hapana mungu ila Mwenyezi Mungu Mmoja, Mtenda nguvu, Mola Mlezi wa mbingu na ardhi na vilivyomo baina yake, Mwenye nguvu, Mwenye kusamehe.

 

Naam mpendwa msikilizaji, Mwenyezi Mungu ni mwenye uwezo mutlaki na hakuna yeyote awezaye kuzuia atakalo Yeye katika irada yake lisiwe. Mwenyezi Mungu anaweza asisamehe makosa na madhambi ya waja wake. Anaweza asifumbie macho makosa na kuteleza kwao, wala asiwarehemu na kuwa raufu na mpole kwao; lakini kwa sababu ya kutaka mlango wa matarajio na matumaini uendelee kuwa wazi kwa waja wake, amemwamuru Mtume wake ambaye amemfanya kuwa rehma kwa walimwengu wote, atamke haya yafuatayo kuwatangazia watu wote, kama isemavyo aya ya 53 ya Suratu-Zumar: Sema: Enyi waja wangu walio jidhulumu nafsi zao! Msikate tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu husamehe dhambi zote. Hakika Yeye ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu. 

Mwenyezi Mungu huyu mwenye huruma na rehma, ambaye rehma zake zisizo na ukomo zinauenea ulimwengu wa mbingu na ardhi, katika kuwazidishia moyo wa matumaini ya kupata rehma na fadhila zake waja waliokata tamaa ya kupata rehma zake, katika aya mbili za Quráni, ambazo ni aya ya 87 ya Suratu-Yusuf na aya ya 56 ya Suratul-Hijr, amewataja waja wa aina hiyo wanaokata tamaa kuwa ni watu waliokufuru na watu waliopotea.

Pamoja na hayo mpendwa msikilizaji, ajabu ni kwamba, Mwenyezi Mungu ana uraufu na usamehevu wa kiasi hicho kwa waja wake waliomwasi, ilhali Yeye Mola si mhitaji wa chochote kwao, bali ni mkwasi mutlaki kama anavyotueleza katika aya ya 8 ya Suratu-Ibrahim ya kwamba: Na Musa alisema: Mkikufuru nyinyi na wote waliomo duniani, hakika Mwenyezi Mungu ni Mkwasi, Anajitosha, Msifiwa. 

Mola mwenye sifa kama hizi, za kuwa kwenye kilele cha ukwasi, angali anaamua kutia mwanga wa matumaini ndani ya nyoyo na roho za waja wake na kupanda mbegu za rehma ndani ya nafsi zao kwa kulitangaza suala la kuwarehemu waja wake kuwa ni jambo aliyoiwajibishia nafsi yake, kwa kuwaelezea kupitia kinywa cha Mtume wake wa rehma, kama isemavyo aya ya 54 ya Suratul-Anáam ya kwamba: Na wanapo kujia wanao ziamini Ishara zetu waambie: Assalamu alaikum! Amani iwe juu yenu! Mola wenu Mlezi amejilazimisha rehema, ya kwamba atakaye fanya uovu miongoni mwenu kwa ujinga, kisha akatubu baada yake na akatengenea, basi hakika Yeye ni Mwenye maghfira na Mwenye kurehemu.

 

Upeo wa rehma za Mwenyezi Mungu unafikia kwenye kilele, pale Yeye Mola anapoamua, si tu kusamehe madhambi na maovu ya waja waliomkosea, lakini pale waja hao wanapojuta na kutubia kwa matendo yao hayo na wakaamua kwa dhati kuyafidia kwa mema, mabaya waliyotenda. Kwani mbali na kuwasamehe na kuwarehemu kwa kuyafuta madhambi yao kwenye madaftari ya amali zao, huyapamba madaftari hayo kwa mema na ya thawabu mpaka kufika hadi ya kutosalia hata chembe ya athari za maovu waliyofanya huko nyuma. Aya ya 70 ya Suratul-Furqan inaielezea taswira hiyo isiyo na kifani ya rehma za Mwenyezi Mungu kama ifuatavyo: Isipo kuwa atakaye tubu, na akaamini, na akatenda vitendo vyema. Basi hao Mwenyezi Mungu atayabadilisha maovu yao yawe mema. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu. 

Tukumbushane tena mpendwa msikilizaji, kwamba wema na rehma hizi zote zisizotasawirika za Mwenyezi Mungu zinatoka kwake Yeye Mola na kuwateremkia watu kila upande, wakati Yeye ndiye Mfalme halisi na mutlaki wa ulimwengu na Yuko kwenye kilele cha uwezo na ujuzi wa kila kitu. Lakini pamoja na yote hayo anawaamuru Malaika wake wateule waliojikurubisha Kwake wawaombee maghufira na msamaha wake waja wake walioteleza na kufanya madhambi. Hayo yanaelezwa na Qur’ani tukufu kama ifuatavyo katika aya ya 5 ya Suratu-Shuura: Zinakaribia mbingu kupasuka juu huko, na Malaika wakimtakasa Mola wao Mlezi na kumhimidi, na wakiwaombea maghfira waliomo kwenye ardhi. Ama hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.

 

Tukiyatafakari yote haya mpendwa msikilizaji ndipo tutakapobaini kuwa, kwa wale wenye imani ya kweli juu ya misingi miwili, ya kuamini kuwepo kwa Mwenyezi Mungu na kufufuliwa, inastahiki wayafanye madhihirisho hayo yasiyo na kifani ya rehma za Mwenyezi Mungu za moyo wa kusamehe na kufumbia macho makosa kuwa ni ilhamu kwao ya kufufua ndani ya nafsi zao sifa za huruma na urehemevu kwa ajili ya kuimarisha mahusiano na wanadamu wenzao; na kwa njia hiyo kufikisha ujumbe wa amani na urafiki duniani, kwa kuwaonyesha walimwengu tofauti ya utamaduni wa Uislamu halisi uliolinganiwa na Bwana Mtume Muhammad SAW mkabala na tamaduni zisizo za Kiislamu, ambazo mbali na kushamirisha ukatili, udhalimu, jinai na mauaji ya watu wasio na hatia zinakanyaga pia misingi yote ya ubinadamu.

Kwa maelezo hayo mpendwa msikilizaji niseme pia kwamba, sehemu ya tano ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu imefikia tamati. Hivyo sina budi kukuaga hadi wakati mwingine inshallah, tutakapokutana tena katika sehemu ya sita ya kipindi hiki. Namuomba Mola wa haki akubariki; na amani, rehma na baraka zake ziendelee kuwa juu yako…/