Nov 06, 2022 10:12 UTC
  • Akhlaqi Katika Uislamu (8)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yako mpendwa msikilizaji popote pale ulipo wakati huu. Nakukaribisha kusikiliza sehemu hii ya nane ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu nikiwa na matumaini kuwa, mimi pamoja na wewe tutanufaika na yale tutakayoyasikia katika kipindi hiki. Endelea kuwa nami basi hadi tamati ya mazungumzo yetu .

Kama unavyokumbuka mpendwa msikilizaji, katika vipindi vilivyopita tumezungumzia kwa muhtasari sifa chanya za chuo cha fikra cha akhlaqi za Kiislamu na kuchambua na kukosoa vyuo vingine vya fikra vya akhlaqi pamoja na kasoro na mapungufu viliyonavyo. Lakini pamoja na hayo, yamkini likatupitikia akilini mwetu suali kwamba, tufanye nini basi ili tusitumbukie kwenye shimo la yoyote kati ya hali mbili za kufurutu mpaka wa kupaparikia mambo au kuamua kujikhini nayo kikamilifu? Ili kupata jawabu la suali hili la msingi, na tuipitie kwa pamoja misingi na miongozo mitatu mikuu katika utamaduni wa kimantiki wa Uislamu; misingi ambayo kama tutaitekeleza na kuifanyia kazi, tutaweza kukifikia kigezo aali na kilichotukuka cha akhlaqi za Kiislamu.

Msingi wa kwanza mpenzi msikilizaji, ni kuhakikisha tunaweka hali ya uwiyano na mlingano katika kujijenga na thamani za kiakhlaqi. Kwa kutoa mfano ni kwamba kwa upande mmoja, tusiwe kama wale wanaopaparikia na kuiabudu dunia, ambao hima yao na malengo yao yote yamejikita katika kujali thamani za kimaada tu; na kila kitu wanakitathmini kwa kuzingatia maslahi yao katika vitu hivyo. Na kwa upande mwingine, tusiwe kama wale waliofurutu mpaka kwenye masuala ya kimaanawi na kiroho, ambao wameyapa mgongo mambo yote ya dunia kwa kujinyima na kujikhini na hata raha na starehe halali za kidunia; na kuamua kuishi maisha yanayokinzana na fitra na maumbile ya mwanadamu. Badala yake tunatakiwa tuitumie dunia na suhula zake zote kwa ajili ya kujijenga kimaanawi.

Siku moja Imam Ali AS alikutana na mtu anayeishutumu na kuisema vibaya dunia. Palepale mtukufu huyo alimkabili mtu yule na kumwambia: “Ewe unayeisema vibaya dunia ilhali imekuteka na kukuhadaa, wewe ndo wa kuishtaki na kuilalamikia dunia, au ni dunia ambayo inapasa ikulalamikie kwa mwenendo wako potofu? Wakati gani dunia imekuhadaa wewe….Baada ya kumwasa hivyo, Imam Ali akaanza kumtajia yule mtu baadhi ya fursa ambazo dunia imemwandalia kwa ajili ya kuwahudumia wanadamu wenzake na kumwambia “ni kwa kiwango gani umeweza kuwahudumia wagonjwa? Basi kuwa pembeni yao na uwape maangalizi. (Umewaombea kwa Allah) wapate shifaa na kuwataka matabibu wawapatie dawa (za kuwaponya)? Kisha baada ya kumuuliza na kumueleza hayo, Imam Ali AS akaanza kumtajia yule mtu fursa muhimu na adhimu zinazopatikana duniani kwa ajili ya kujijenga kimaanawi, kwa kumwambia: “Hii dunia ni fursa ya ukweli na usadikishaji kwa mtu atakayekuwa mkweli katika kuamiliana nayo; na ni mahali pa kupatia ukwasi na kujivua na uhitaji. Ni mahali pa mtu kujikusanyia masurufu na kupatia nasaha na mafunzo kwa kuaidhika na matamu na machungu yake. Kisha Imam Ali akambainishia yule mtu matukufu ya kimaanawi ya dunia kwa kumwambia: dunia ni sujudio la wampendao Mwenyezi Mungu, mahali pa Sala na minong’ono ya dua za malaika, mahali pa kuteremshiwa wahyi wa Mwenyezi Mungu na eneo la biashara kwa mawalii na waipendao haki; wao wamejichumia rehma na baraka zisizo na kifani za Mola papa hapa duniani na kujiandalia Pepo ya milele. (Nahjul-Balaghah, Hikma 131)

Sifa nyingine maalumu ya akhlaqi za Kiislamu ni kwamba, huwa zinamtengeneza mtu mwenye shakhsia za pande na hali kadhaa. Mtu aliyelelewa na kukulia kwenye chuo cha fikra cha akhlaqi za Uislamu, kwa upande mmoja huwa ni dhihirisho la mvuto, huba na upendo kwa wanadamu wenzake; na kwa upande mwingine huwa mkali na mwenye msimamo thabiti usiolainika mbele ya watu wasiojali na kuheshimu hata chembe thamani za kiitikadi, kiakhlaqi na kiutu. Kwa upande mmoja huwa ni mtu mwenye bidii kubwa na matumaini, na kwa upande mwingine hupiga vita kila hisia za kuvunjika moyo na kukata tamaa. Katika dunia ya ufanyaji ibada, huwa ni mkeshaji usiku kwa Sala na dua na katika medani ya jihadi huwa ni shujaa mkubwa wa kupambana na vinara wa shirki, ukafiri na unafiki. Anaujali kikamilifu upande wa akhalqi za binafsi kama kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu, kushika mafundisho ya dini na kuitakasa batini na nafsi yake; na anazipa umuhimu mkubwa pia akhlaqi za kijamii kama kuwapenda na kuwajali wanadamu wenzake na kuishi nao kwa amani na masikilizano. Kwa muhtasari ni kwamba chuo cha fikra cha akhlaqi za Kiislamu hakimfanyi mtu awe kiumbe wa upande mmoja tu, bali kinamlea na kumkuza kwa namna inayomfanya awe na nafasi na mchango mkubwa na wa maana katika nyuga zote za maisha.

Kuhusiana na suala hili, Bwana Mtume Muhammad SAW na Maimamu watoharifu AS waliotokana na kizazi chake ni vigezo sahihi kabisa na ruwaza zilizokamilika za akhlaqi za Kiislamu; kwa sababu katika ulimwengu wa ibada, hakukuwa na aliyefanana nao; na katika medani ya jihadi, hawakuwa watu wa kutawa na kujitenga, bali walikuwa mstari wa mbele katika kujishughulisha na masuala yote ya kijamii. Hawakuwa na chembe ya uchu wa madaraka, lakini kwenye ulingo wa siasa, walikuwa viongozi weledi na wenye ufanisi wa kiwango cha juu kabisa.Kwa hakika tunaweza kuthubutu kusema kuwa, moja ya sifa za kipekee za chuo cha fikra cha akhlaki za Kiislamu ni kwamba, mbali na kuleta uwiyano na mlingano katika malezi na makuzi ya watu waliopambika kwa shakhsia kadhaa, huwawezesha pia watu hao kukwea na kufikia daraja na upeo wa juu kabisa wa thamani za kiakhlaqi.

Dondoo za ufunguzi wa dua ya Makaarimul-Akhlaq ya Imam Sajjad AS, zinabainisha nukta hiyo ya msingi kabisa. Baada ya mtukufu huyo kumsalia na kumtakia rehma na amani Bwana Mtume SAW na Ahlul-Bayt zake watoharifu, anamuelekea na kumwomba Mola kwa kusema: "Ewe Mola wangu, ifikishe imani yangu kwenye upeo wa juu kabisa wa imani, na uifanye yakini yangu ifikie kiwango cha juu kabisa cha yakini, na uifanye nia yangu iwe nia iliyo njema zaidi na zifanye amali zangu ziwe amali bora kabisa.

Maneno hayo ya upeo wa juu zaidi wa imani, kiwango cha juu kabisa cha yakini, nia iliyo njema zaidi na amali zilizo bora kabisa yanadhihirisha ubora usio na kifani wa misingi ya akhlaqi katika utamaduni uliokamilika na kutukuka wa chuo cha malezi cha Uislamu.

Na kwa maelezo hayo mpendwa msikilizaji niseme pia kwamba, sehemu ya nane ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu imefikia tamati. Hivyo sina budi kukuaga hadi wakati mwingine inshallah, tutakapokutana tena katika sehemu ya tisa ya kipindi hiki. Namuomba Mola wa haki akubariki; na amani, rehma na baraka zake ziendelee kuwa juu yako…/