Nov 06, 2022 11:22 UTC
  • Akhlaqi Katika Uislamu (16)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yako mpendwa msikilizaji popote pale ulipo wakati huu. Nakukaribisha kusikiliza sehemu hii ya 16 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu nikiwa na matumaini kuwa, mimi pamoja na wewe tutanufaika na yale tutakayoyasikia katika kipindi hiki. Endelea kuwa nami basi hadi tamati ya mazungumzo yetu, ambayo kwa leo yatahusu umuhimu wa kutimiza ahadi na kujiepusha na mwenendo wa kuvunja ahadi na mapatano.

Mpendwa msikilizaji, kielezo na sifa nyingine muhimu ambayo imepewa uzito na kutiliwa mkazo sana katika utamaduni wa kiakhlaqi wa Uislamu ni kuheshimu ahadi na makubaliano ya kiitikadi, kijamii, kiuchumi, kisiasa na kijeshi. Mtu hata awe mfuasi wa dini, taifa, imani au fikra yoyote ile, lakini hupendezwa na tabia ya kuheshimu ahadi na makubaliano; na kwa sababu hiyo, huwa anahisi ahadi, makubaliano au mkataba wowote unaofungwa baina ya mataifa mawili, serikali mbili au hata baina ya watu wawili inapasa uthaminiwe na kuheshimiwa. Isitoshe, kuheshimu ahadi, mkataba na makubaliano huzidisha uaminifu na kuimarisha uhusiano; na kama jamii, serikali au watu binafsi hawatahisi kuwa wana dhima na masuulia ya kuheshimu ahadi na makubaliano au wakayadharau na kuyakhalifu, huwa wanajiharibia heshima na uaminifu wao.

Katika kufunga mikataba na makubaliano ya kijamii, kisiasa, kiuchumi, kijeshi na ya mambo mengine, inapasa tuzingatie na kutilia maanani pia kiwango cha nguvu na uwezo tulionao, ili tusije baadaye kuingia lawamani kwa kushindwa kuyatekeleza tuliyoyaahidi.

Lakini kama tulivyotangulia kueleza katika vipindi vilivyopita, inatupasa tufahamu kwamba, wenzo madhubuti na wa uhakika zaidi kwa ajili ya kutekeleza thamani za kiakhlaqi na kujiepusha na sifa zinazokinzana na akhlaqi njema ni imani na itikadi za dini za watu. Sababu ni kwamba, tajiriba chungu za karne zilizopita na hata za zama zetu hizi zimeonyesha kuwa, wenye nguvu za mali na madaraka huwa wako tayari kuheshimu ahadi na makubaliano, pale tu yanapodhamini maslahi yao; lakini kama watahisi kuendelea kuheshimu mikataba na makubaliano kuna madhara na wao, hawasiti kuvunja ahadi na mapatano. Tab'an katika hali na mazingira kama hayo, akili na dini pia zinatutaka tusikae vivi hivi tu pale adui anapokhalifu ahadi na makubaliano, bali tuchukue hatua kukabiliana na kitendo chake hicho.

Kuhusiana na nukta hiyo, kuna hata aya ya Qur'ani inayoeleza kwamba, mtakapohisi adui ana dhamira ya kuvunja ahadi na makubaliano, nyinyi tangulieni kuchukua hatua kiimara na kwa uwezo kamili; na kabla wao hawajachukua hatua ya kuvunja makubaliano, watangulieni kwa kuhakikisha mnawarejeshea wenyewe mkataba mliofungiana nao, wala msiwaachie wakakutangulieni kuvunja makubaliano.

Mkataba wa kwanza kabisa wa kifitra na wa tauhidi ya kivitendo, ambao wanadamu wote, bila kujali sifa za utaifa, jiografia na asili zao, walifunga na Mwenyezi Mungu, ni mkataba ambao Yeye mwenyewe Mola Muumba ameuzungumzia kama ifuatavyo katika aya ya 60 na 61 za Suratu-Yaasin: Je! Sikuagana nanyi, enyi wanaadamu, kuwa msimuabudu Shet'ani? Hakika yeye ni adui dhaahiri kwenu. Na ya kwamba mniabudu Mimi? Hii ndiyo Njia Iliyo Nyooka.

Mkabala wa wanadamu kutekeleza ahadi hiyo waliyowekeana na Mwenyezi Mungu, Yeye Mola amewaahidi wao, hasa wale waliomwamini kikwelikweli, mambo mengi sana, kama kuwapa nusra yake, kuwalinda, kuwapa ushindi dhidi ya maadui zao, kuwafanya wawe na izza, heshima na utukufu hapa duniani na kwenda kuwaingiza peponi huko akhera wakiwa pamoja na mawalii wake makhususi. Na kama isemavyo Qur'ani: "Ni nani aliye na mwamana zaidi wa kutekeleza ahadi yake kuliko Mwenyezi Mungu?"

Kwa hivyo mikataba bora na yenye kuwapa utulivu zaidi watu ni ile wanayofunga waumini na Muumba wa ulimwengu. Kwa sababu utekelezaji wake ni wa uhakika na katu haikhalifiwi. Na ndipo Mwenyezi Mungu Mtukufu akasema katika sehemu ya mwisho ya aya ya 111 ya Suratu-Tawba ya kwamba: Basi furahini kwa biashara yenu mliyo fanya naye. Na huko ndiko kufuzu kukubwa.

Alaa kulli hal, kuheshimu na kutekeleza ahadi na makubaliano ni moja ya misingi iliyotiliwa mkazo sana katika utamaduni wa kiakhlaqi wa Uislamu. Kwa mujibu wa mafundisho ya dini hiyo yanayomjenga mwanadamu na kumpa ukamilifu wa kiutu, uchamungu ni jambo la lazima kwa mtu kuweza kuheshimu makubaliano. Yaani nguvu maalumu ya ndani ya nafsi, ambayo humzuia mtu kuvunja na kuhalifu ahadi na makubaliano yoyote aliyofunga.

Katika aya ya 76 ya Suratu-Aal Imran, Qur'ani tukufu inabainisha hivi kuhusu thamani za kuheshimu ahadi na makubaliano: " Ndivyo hivyo, anaye timiza ahadi yake na akamchamngu basi Mwenyezi Mungu huwapenda wachamngu."

Kwa hivyo kwa mtazamo wa Uislamu halisi, kuheshimu ahadi na mapatano ni jukumu zito na masuulia makubwa anayobeba mtu. Na hasa kama mtu atajua kwamba, lazima atakwenda kusailiwa na kuwajibika kesho Kiyama mbele ya mahakama ya uadilifu ya Mwenyezi Mungu. Na hilo linazungumziwa hivi katika aya ya 34 ya Suratu-Israa: Na timizeni ahadi. Kwa hakika ahadi itasailiwa.

Kwa hivyo hitimisho tunalofikia hapa mpendwa msikilizaji ni kwamba, misingi miwili ya imani juu ya Mwenyezi Mungu na kufufuliwa ni mwega imara na msukumo madhubuti wa kutekelezea mikataba na mapatano; kwa sababu ni jambo lisilo na shaka kuwa mtu anayeamini kwamba Mwenyezi Mungu anamwangalia pale atoapo ahadi na anaamini kwamba lazima atakwenda kujieleza kesho Kiyama kuhusu ahadi alizotoa, hatofikiria katu kuvunja ahadi na makubaliano na hasa kama atajua kuwa, Bwana Mtume SAW amesema: "Mwenye kuvunja makubaliano hana dini". (Mizanul-Hikmah, uk, 742)

Pamoja na miongozo hii na vielezo vyote hivi vilivyo wazi kabisa, kuna baadhi ya watu wanaofikiria maslahi na manufaa yao tu, ambao hujaribu kutumia visingizio visivyo na msingi, kama kupambanua baina ya watu wema na waovu ili kuvunja ahadi na kukataa kutekeleza mapatano waliyofikia na watu.

Imam Muhammad Baqir AS ameubatilisha kikamilifu mtazamo huo aliposema: "Kuna mambo matatu ambayo Mwenyezi Mungu hajampa idhini mtu yeyote ayakhalifu: Kutunza au kurejesha amana, kutekeleza ahadi na makubaliano na kuwatendea wema wazazi, wawe ni watu wema au waovu." (Al-Kafi Juzuu: 2 Uk. 162)

Katika kuhitimisha mazungumzo yetu ya leo tunaweza kusema kuwa, kuthamini ahadi na makubaliano ni thamani tukufu ya kidini kiakhlaqi na kiutu na moja ya alama za kuwa mkweli katika maneno na matendo. Sifa mbili hizi ni mizani nzuri ya kupimia shakhsia za watu na pia ni kipambanuzi cha kuwatafautisha wafuataji dini wa kweli na wanafiki wanaojinasibu kwa ndimi zao tu. Na kwa maelezo hayo niseme pia mpendwa msikilizaji kwamba sehemu ya 16 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu imefikia tamati. Hivyo sina budi kukuaga hadi wakati mwingine inshallah, tutakapokutana tena katika sehemu ya 17 ya kipindi hiki. Namuomba Mola wa haki akubariki; na amani, rehma na baraka zake ziendelee kuwa juu yako…/